YANGA imemponza mwamuzi,
Martin Saanya wa Morogoro aliyechezesha mechi yao na Coastal Union ambaye
amefungiwa mwaka mmoja kwa kuchezesha mchezo huo chini ya kiwango.
Saanya amepewa adhabu
hiyo ya kutochezesha mechi yoyote ya soka ndani ya kipindi hicho sawa na mshika
kibendera namba moja wa mechi hiyo, Jesse Erasmo ambaye alishindwa kutoa uamuzi
sahihi wa adhabu ya penalti waliyopewa Coastal ndani ya dakika za nyongeza
kabla ya mpira kumalizika na kusababisha sare ya bao 1-1.
Penalti hiyo ndiyo
ilisababisha vurugu ambazo zilifanywa na mashabiki wa Yanga ambao ,
walimshambulia mwamuzi kwa chupa za maji na kuvunja kioo cha basi la wachezaji
wa Coastal na kumjeruhi kichwani beki wa timu hiyo, Hamis Hamad aliyelazimika
kuwahishwa hospitali.
Adhabu hizo zimekuja
baada ya Bodi ya Ligi kupitia taarifa ya kamishna wa mechi hiyo, Omary Walii
kutoka Arusha.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Saanya na
Erasmo wamefungiwa mwaka mmoja kuchezesha mechi za ligi baada ya bodi kupitia
ripoti ya kamishina wa mchezo huo.
Saanya ameadhibiwa kwa
kuchezesha chini ya kiwango na alitoa adhabu ya penalti iliyofungwa na Coastal
akiwa mbali na tukio,” alisema Mwakibinga na kufafanua kuwa posho za waamuzi wa
mechi kwa sasa ni Sh 250,000 mbali na nauli na teksi tofauti na zamani
walipokuwa wanalipwa shilingi 170,000.
“Kwa upande wa Erasmo
ndiye alikuwa eneo la tukio ilipotokea penalti, lakini alishindwa kumsaidia
mwamuzi wa kati na kubaki ameduwaa kama asiye na uhakika.”
Mwakibinga alisema mbali
na adhabu hizo kwa waamuzi, Kamati imemfungia kocha wa makipa wa Coastal Union,
Juma Pondamali muda wa miezi mitatu na faini ya Sh1 milioni kwa kutoa lugha ya
matusi kwa mashabiki wanaodaiwa ni wa Simba.
Katika hatua nyingine,
Coastal imetozwa faini ya Sh100,000 kwa kuchelewa kikao cha maandalizi ya mechi
asubuhi kwa dakika 23 huku Yanga ikitozwa faini ya Sh1 milioni kwa mashabiki
wake kurusha chupa uwanjani na pia kumvamia mwamuzi huku viongozi wakishindwa
kuwadhibiti.
Kuhusu basi la Coastal
hakukuwa na taarifa kwani tukio lilitokea nje ya uwanja.
SOURCE: GAZETI LA
MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment