Makocha wa Coastal Union Kocha mkuu Hemed Morocco (mwenye kofia), Kocha msaidizi Ally Kido (katikati), na kocha wa magolikipa Juma Pondamali 'Mensah' wakijadiliana kitu.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea katika
raundi yake ya 25 kesho (Mei Mosi) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya
Dar es Salaam, Turiani, Morogoro na Mlandizi.
Licha ya kuwa tayari Yanga imetawazwa kuwa
mabingwa wa VPL msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union
itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam ni moja kati ya zitakazovuta macho na masikio
ya washabiki wa mpira wa miguu nchini.
Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na mwamuzi
Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa
Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam . Kamishna wa mechi hiyo ni
David Lugenge kutoka Iringa.
Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza saa 10.15
jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya
rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.
Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa African Lyon
katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa
Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi
ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na wenye
uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa mechi kati ya JKT Ruvu na
Tanzania Prisons. Nayo Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake
Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro JKT kutoka Arusha.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
Aprili 30, 2013