Tuesday, June 25, 2013

June 30 siku ya Jumapili mkutano mkuu wa wana Coastal Union. Usikose...

 Mashabiki wa Coastal Union wakijadili hali ya timu baada ya kufungwa na frican Lyon uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam ligi kuu mzunguko wa pili.

             Mashabiki Coastal Nyumba hawa. Chini ya uongozi wa Pius, naye ana mpira mwingi huyu...


Uongozi wa Coastal Union unawatangazia mashabiki wake walio ndani na nje ya nchi kuwa siku ya jumapili wiki hii June 30 kutakuwa na mkutano mkuu wa wanachama utakaofanyika mjini Tanga.

Mkutano huo ni muhimu kuhudhuria hata kama huna kadi ya uanachama, kwani itakuwa ni fursa pekee ya kupanga mikakati ya msimu ujao wa soka 2013/14 ili kuhakikisha kikosi imara cha wana Mangush kinaweka heshima ya soka nchini kwa kuchukua ubingwa kama walivyofanya mwaka 1988.

Uongozi unaweka wazi kuwa kwa yeyote ambaye ana malalamiko ama ushauri juu ya kuendesha timu ili kufikia mafanikio, basi ahudhurie kwenye mkutano ili kumaliza kiu yake na si kusema pembeni bila tija.

Siku hiyo mbali ya ajenda za kujenga timu pia kutakuwa na mikakati ya viongozi na kugawa majukumu kwa wanachama, pia kutajadiliwa namna ya kuhakikisha mashabiki walio mikoani na nje ya nchi wanatambulika rasmi na kukaribisha michango ya hali na mali kwa lengo moja tu, kuleta ushindi msimu ujao.

Tayari timu yetu imesharudi nyoyoni mwa wapenda soka, kilichobaki ni kuhakikisha hatuwavunji moyo wapenzi wetu cha kufanya ni kupata kadi ya uanachama ambazo zitatolewa siku hiyo, na pia kutawekwa utaratibu bora wa kuhakikisha timu inatunisha mfuko wa maendeleo.

Wanachama wengi wanawasiliana katika mitandao lakini hawajuani kwa sura hii itakuwa nafasi ya kipekee kuweza kujuana na kubadilishana mawazo, tayari wanachama wengi kutoka mikoa ya jirani wamethibitisha kuhudhuria mkutano huo, umebaki wewe tu.

Tuache kusemasema vipembeni tuelekee kwenye mkutano mkuu tarehe 30 June, 2013.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
25 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Monday, June 24, 2013

Anaitwa Douglas Muhani 'Kitimua vumbi nguvu kurukundu'

Huyu munayemuona kwenye picha ni LEGEND kati ya mabeki waliowika Tanzania bara na visiwani, ni mchezaji aliyefanya vizuri kwenye mashindano Afrika Mashariki na kati yaliyofanyika nchini Kenya! Naye ndiye aliyeipa COASTAL UNION ubingwa 1988, kama hiyo haitoshi ni mchezaji aliyekua anajua wajibu wake kabla ya mechi, alikuwa akifanya sana mazoezi ya viungo na alikuwa hachoki kwenye mechi, ana pumzi nyingi sana. Anaitwa DOUGLAS MUHANI.


Muhani atakumbukwa kuwa mchezaji tegemeo kwa mipira ya vichwa, mbali ya ufupi wake lakini mzuri kwa kuruka vichwa kama ni mpira wa kona kwa timu piinzani ujue watu watarudi wanacheka na kama ni mpira wa kona langoni kwake ujue washambuliaji waroho watarudi vichwa chini.       


Kuna kituko ambacho hakitasahaulika baada ya kupewa pesa ili acheze chini ya kiwango timu pinzani ipate urahisi wa kufunga. Sasa lilipokuja jambo la albadir kabla ya mechi ndipo aliposema jamani mimi hela nimepewa lakini kupewa hela kwangu musinitilie shaka nitaupiga mwanzo mwisho tena zaidi ya uwezo wangu ili siku nyingine wakome tabia za kuhonga honga watu! Tena aliongeza kwa kusema yeye ni Coastal kwanza na mambo mengine nyuma.

Maana siku hiyo ilikuwa muhimu timu ishinde wazee wakaamua kufanya kisomo ili ambaye ameuza mechi limfike la kumfika, Mzee Mwamsagala akamuuliza Mzee maliki sasa muda wa kisomo umefika umeshawauliza vijana wako? Muhani akaona isiwe tabu akaamua kujiweka peupeni, mdhamini wa Coastal Union Said Soud akamwambia usijali pesa kula na mpira ucheze.

Taarifa zinasema jina lake halisi ni Hamisi Omar Muhani, mwenyeji wa Rufiji ameshika dini ya Kiislamu nyakati ya sala haimpiti tangu anacheza soka mpaka sasa amekuwa mtu mzima anakaribia uzee na wala hajawahi kugusa pombe. Hussein Mwakuluzo, anasema hajawahi kuona mchezaji anayefanya mazoezi kama Muhani, maana walipokuwa wanakwenda mazoezini wanamkuta tayari ameshafika na amefanya mazoezi mpoaka jasho linamtoka. Mazoezi ya pamoja yakianza na yeye yumo.

Razak Careca anamuita kwa majina ya utani 'Kitimua vumbi nguvu kurukundul' hata sijui maana yake nini lakini nadhani ni kutokana na nguvu alizokuwa nazo mpaka akicheza anatimua vumbi. Careca anaongeza kuwa "ni mcheshi akiwa nje ya uwanja ila akiwa uwanjani hataki mchezo anajituma sana akitoka uwanjani amechafuka mwili mzima wacha bwana Doglas alikua mashine."

       
COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
25 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Je unamjua huyu? Ameifanyia makubwa Coastal Union.

Nassor Yoga.
Huyu munaemuona hapo ndie aliyekua mchoraji mkubwa wa COASTAL UNION mwaka 1988, Mungu alimpa kipaji cha kuchora picha nyingi lakini mchoro wake maarufu ni nembo ya Coastal Union yenye sura ya mbwa mwitu 'FOX,' na pia alileta sana changamoto pale maskan ya vijana wa mjini SWEET CORNER! alifanya vi2ko vingi sana na pia mashabiki wa African Sports walikua wakimjua kwa ufedhuli wake.

Hata hivyo alijivunia kuonekana adui namba moja wa African Sports, atakumbukwa baada ya COASTAL UNION kuchukua ubingwa alichora picha ya SINGA SINGA wa African Sports kisha akaandika kofi la mpenzi haliumi/

Bendera zote za timu alikua akizichora yeye, vilevile ana kumbukumbu nyingi sana picha za timu, alikuwa hakosi katika misafara timu inapocheza mikoani. Mpaka sasa ni msabiki mkubwa wa wagosi wa kaya hakosi uwanja wa Mkwakwani Coastal Union inapocheza. Anaitwa Nassor Yoga, ni mwana Tanga kindakindaki.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
25 June, 2013
Tanga, Tanzania

Sunday, June 23, 2013

Hatimaye Coastal Union yanasa saini ya mchezaji kutoka Kenya.

 Mwakilishi wa Coastal Union nchini Kenya Hussein Tawakkal akikamilisha zoezi la usajili la mchezaji kutoka Bandari ya Mombasa na Harambee Stars ya Kenya CRISTIN ODULA WADENYE kwa mkataba wa kuwachezea Wagosi kwa miaka miwili jana jijini Mombasa.......huyu ni mchezaji ambae kocha wetu Hemed Morocco akililia kwa udi na uvumba apatikane tena kwa gharama yoyote ili aje kutengeneza 'combination' hatari katikati wakisaidiana na  Jerry Santo na Haruna Moshi 'Boban'.............wapinzani kaeni mkao wa kuliwa.........!!!!!

Mkurugenzi wa ufundi wa Wagosi wa Kaya Nassor Ahmed 'Binslum' mwenye kofia akiwa na kiungo mshambuliaji kutoka Bandari ya Mombasa aliyesaini kuungana na kikosi cha Coastal Union CRISTIN ODULA (katikati), kulia ni mwakilishi wa Coastal Union jijini Mombasa Kenya ndugu Hussein Tawakkal.

Coastal Union sasa imebakisha mchezaji mmoja tu katika safu ya ushambuliaji baada ya kufanikiwa kunasa saini za wachezaji kumi watatu wakitoka timu ndogo. Msimu ujaoo mmhhh we acha tu.

COASTAL UNION
23 JUNE, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA.

Friday, June 21, 2013

Hii ndiyo kambi itakayotumika na Coastal Union msimu ujao.

Ni Raskazone Hotel ipo Bombo Area Tanga, ina ofisi ya kocha na nyumba za walimu wote, vyumba vya wachezaji wote na ukumbi mkubwa wa mikutano. Kuanzia sasa hii ni mali ya timu kwa mwaka mzima.

Thursday, June 20, 2013

Coastal Union yaingia mkataba na Raskazone Hotel na kuigeuza kambi.

 Ally Kiraka akimkabidhi fedha hundi na taslim jumla ya milioni 15 kwa Hornest Macha ambaye ni mtoto wa marehemu Mzee Macha aliyekuwa mmiliki wa Raskazone Hotel iliyo Tanga. Coastal Union imeingia mkataba na familia ya Mzee Macha, kuitumia Hotel hiyo kwa kambi ya timu msimu mzima 2013/14. Gharama za pango ni milioni 25 kwa msimu.

 Ally Kiraka akiweka saini kuwa shahidi upande wa Coastal Union huku kwa mbali ndugu Hornest akiweka saini upande wa familia jijini Dar es Salaam leo..

Makamu mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mnguto 'mwenye tai kushoto' akibadilishana nyaraka za mkataba wa Raskazone Hotel kwa mtoto wa marehemu Mzee Macha, Hornest Macha leo jijini Dar es Salaam.

Coastal Union imeamua kutafuta kambi kwa msimu ujao baada ya msimu uliopita wachezaji kukosa uangalizi baada ya kila mmoja kukaa kwa kujitegemea. Raskazone Hotel ambayo ipo Bombo Area jijini Tanga kwa muda mrefu imesimama kufanya kazi hivyo uongozi wa timu umeamua kuitumia nafasi hiyo vema kwa faida ya timu na wachezaji.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
20 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Wednesday, June 19, 2013

Kikosi cha Coastal Union kilichotwaa ubingwa wa soka Tanzania mwaka 1988.


Yassin Abuu Napili 'Garagaregwa'

Abuu Yassin Napili, mchezaji wa zamani wa Coastal Union ambaye alijulikana kwa jina maarufu Valmet au kumbakumba kutokana na kujaaliwa mwili mkubwa wenye nguvu. Alikuwa beki mzuri enzi za kucheza kwake soka.

Kutokana na nguvu alizojaaliwa kuna mechi katika uwanja wa Mkwakwani dhidi ya watani wa jadi kutoka barabara ya 12 African Sports, Napili aliupiga mpira mpaka ukapasuka. Wengi wanaamini kilikuwa ni kitendo cha bahati nasibu, wengine wanaamini ilikuwa uchawi na wapo wanaoamini ni uwezo na nguvu za miguu.

Hussein Mwakuluzo anasema wakiwa kambini walikuwa wakimuita Napili kwa jina la utani la Garagaregwa kwa namna alivyokuwa na uchungu na mpira hataki utani mpaka mazoezini mipira yote ya adhabu ndogo anataka kupiga yeye. Na kitu cha kuchekesha Ally maumba naye alikuwa anapenda kupiga mipira iliyokufa 'adhabu' ikawa ugomvi baina ya Maumba na Napili.

Mchezaji huyu anahitaji heshima ya hali ya juu, maana Coastal Union baada ya kupata ubingwa mwaka 1988 wachezaji wazuri wote walipata soko nchi za Kiarabu, kipindi hicho Arabuni kulikwenda wachezaji wengi kutoka Afrika Mashariki. Lakini aliporejea miaka ya tisini yeye akiwa na Hilal Hemed, Juma Mgunda waliamua kujiunga tena na kikosi kijabahatika kupanda ligi kuu lakini baada ya msimu mmoja timu ikashuka.

Mwaka 2007 ikapanda tena lakini msimu huo huo ikashuka tena mpaka ilipopanda mwaka 2010 ambapo ilirudi kwa kishindo ikashiriki ligi kuu msimu wa 2011/12 na kushika nafasi ya tano, halafu msimu ulioisha wa 2012/13 imeshika nafasi ya sita.

COASTAL UNION
19 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA



Aggrey Chambo 'Mkombozi'

Aggrey Chambo akionekana alivyo sasa amedhoofu tofauti na kipindi alichokuwa akicheza mpira.

Aggrey Chambo, miongoni mwa vifaa vilivyosaidia kupeleka heshima ya soka mkoani Tanga alikuwa mzuri katika kuchungulia nyavu.

Itakumbukwa goli lake la kusawazisha dhidi ya Miembeni kombe la muungano msimu wa 1988/89 ndilo lililotupa nafasi ya pili nyuma ya African Sports na kutupatia ticket ya kushiriki kombe la washindi barani Africa na kutolewa na Ferraviaro ya msumbiji.

Hussein Mwakuluzo anaeleza kuwa "Hiyo mechi na miembeni naikumbuka vizuri sana, nilicheza mechi nikiwa na malaria, zikiwa zimesalia dakika tano mpira kwisha nikawa siwezi kuendelea na mechi, ndiyo nikatoka akaingia Aggrey! Mpira wa kwanza alioupata akampiga kanzu Riffat Said akafunga goli."

Mwakuluzo anaongeza kuwa "Nakumbuka mechi hiyo ilikuwa na ushindani sana nakumbuka nilibaki na Riffat Said, mara kadhaa na zote aliokoa, mwaka uliofuata Riffat akasajiliwa na Coastal Union."

Jina jingine la Aggrey aliitwa Mkombozi, kwasababu alikuwa akiingia lazima abadili matokeo, Ally Kiraka anasema "Nakumbuka mechi na Simba uwanja wa Mkwakwani Mohammed Mwameja ndiyo amesajiliwa Simba, mechi hii Aggrey alibishana sana na Mwameja na hiyo mechi ilikua na vurugu sana nje ya uwanja mpaka ndani ya uwanja.

"Tulipata penati Kassa Mussa kwa presha akakosa ndipo 'Mkombozi' Aggrey Chambo akasawazisha tukatoka suluhu na Simba ya 1-1 tukawatibulia ubingwa wao ndipo vurugu kubwa watu wa 'sweat corner' wakapigana na wachezaji wa simba pamoja na washabiki wao. Buma, alipigana na watu kama 10 ila alikua na nguvu ndiyo siku tuliyovunja undugu na Simba."

Kudhihirisha ukombozi wake Aggrey Chambo katika mechi dhidi ya African Sports, Mombasa Stadium alikomboa goli halafu Juma Mgunda akafunga goli la kuongoza mpaka mpira unaisha Coastal Union 2 African Sports 1, ilikua ni kwenye sherehe za Uhuru wa Kenya mwaka 1990 timu zote zilialikwa.

Kwa sasa legend huyu Aggrey Chambo anasumbuliwa na maradhi, mwili wake ni dhaifu sana, kwa sasa mtu pekee anayemsaidia ni golikipa wa zamani wa Coastal Union, Simba na timu ya Taifa Mohammed Mwameja ambaye ametoa pesa katika hoteli mojawapo eneo la karibu analoishi Chambo jijini Dar es Salaam ambapo anapata chakula kila siku.

Ukijisikia kumsaidia kwa hali na mali piga namba hizi 0714392601 ukipiga atapokea kijana mmoja anaitwa Uledi ndiye anayekaa na Aggrey, useme nataka kuongea na Aggrey ataitwa maana hana simu.

COASTAL UNION
19 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA


Menye, kocha msaidizi wa Coastal Union mwaka 1988.


Huyu alikuwa kocha msaidizi wa Coastal Union anaitwa Jumbe Ahmed Menye, alimsaidia Zakaria Kinanda mwaka 1988, pia katika kombe la Afrika Mashariki.

Tuesday, June 18, 2013

Habari picha sign ya Abdi Banda.

 Abdi Banda akimwaga wino kuitumikia Coastal Union kwa miaka mitatu, ambapo alipewa milioni 3 papo hapo leo asubuhi jijini Dar es Salaam, pembeni ni meneja wake Abdul Bosnia 'Father'.

 Makamu mwenyekiti Steven Mnguto akimweleza mawili matatu Banda kabla ya kutia saini mkataba wake.

 Banda akiwa na ndugu yake Meddy ambaye ni mtoto wa Abdul Bosnia, hapa wanapitia mkataba kabla ya kuutia saini.

 Hapa akihakikisha anaweka saini kila kurasa ya mkataba ili isiweze kughushiwa kwa namna yoyote ile iwe kuongezwa kurasa ama kunyofolewa kurasa.

 Mzee Mnguto mzuka ulikuwa umempanda wakati akitoa somo kwa Banda umuhimu wake katika timu.

 Hii ni hatua nzito kufikiwa, kupeana mikono ndiyo njia sahihi ya kuonmyesha wamekubaliana.

 Father naye alitoa mkono kuonyesha kuafikiana na kila kitu kuhusu mtoto wake kuendelea kuwa mpinzani, kwani yeye ni African Sports damu huku kijana wake atakuwa Coastal Union damu.

Pesa sabuni ya roho
Hatimaye yule beki ywa kushoto kutoka timu ya vijana Abdi Banda, ambaye alikuwa akisuasua kusaini na Coastal Union amekubali kufanya hivyo huku akiwa na furaha tele.

Banda ambaye ameonyesha uwezo wa hali ya juu amekubaliana kukitumikia kikosi cha wagosi wa kaya kwa miaka mitatu ambapo makamu mwenyekiti wa Wagosi Steven Mnguto alikuwa shahidi upande wa timu na shahidi wa beki huyo alikuwa meneja wake Abdul 'Bosnia' Father ambaye ni mchezaji wa zamani wa Afrcan Sports 'Wana kimanumanu' ambao ni mahasimu wakubwa wa wagosi wa kaya.

Akizungumza baada ya kutiliana saini Abdul Bosnia 'Father' alisema Banda amefurahi sana kucheza tena katika kikosi cha wagosi kwani hakuna namna nyingine bora itakayomwezesha kuonekana zaidi ya kucheza timu ya hadhi ya Coastal Union.

"Mimi nilikuwa Sports damu lakini hilo halikuzuii wewe kuwa Coastal damu kwani haya ni maisha yako, mwenzio nilikuwa naipenda timu yangu kwasababu ndiyo iliyonilea hivyo nakuomba ufanye hivyohivyo," alisema Father kumwambia mwanawe Banda na kuongeza.. "Waheshimu wachezaji wenzako, waheshimu walimu, viongozi na mashabiki, hakika utafanikiwa.

"Wakati marafiki zangu Hussein Mwakuluzo na Razack Yusuf 'Careca' walipohamia Coastal Union kutoka African Sports nami nilitaka kuwafuata, lakini wazee wa timu waliniambia nibaki African Sports kwani hapo ndipo nilikuwa na uhakika wa kupata namba kikosi cha kwanza, hivyo hata wewe hapa Coastal Union ndipo nyumbani kwako."

Katika hatua nyingine baada ya kuonekana suala la Banda kusaini Coastal Union limekuwa gumu wadau waliamua kuhaha na kufanya kila jitihada kuhakikisha kijana huyo anamwaga wino. Miongoni mwa mashabiki waliowasiliana na blog hii kutoka Tanga ni Miraji Wandi 'Shoka' ambaye alieleza juhudi zake na kusema:

"Mimi namfahamu Banda tangu akiwa mdogo, tangu anaanza kujiunga na kikosi B chini ya kocha Bakari Shime, nilifanya naye mazungumzo ya ana kwa ana lakini bado alionekana mgumu, nikajua kuna watu wanamshauri vibaya kwakuwa nafahamu banda anamuheshimu sana kocha wake Hemed Morocco nikaamua kufanya 'conference call' tukaanza kuzungumza mimi, Banda na Morocco.

"Morocco alizungumza maneno mazito sana, na nadhani ndiyo sababu ya banda kuamua kutumia akili yake badala ya akili za kuambiwa, na leo amesaini hakika ni furaha kubwa kwangu," alisema Wandi.

Naye mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo Nassor Binslum aliweka wazi kuwa alishaanza kuudhika kutokana na kitendo cha Banda kuonekana anashauriwa vibaya na kusahau fadhila za timu yake iliyomlea tangu akiwa hajui mpaka sasa anatajika katika soka la Tanzania.

"Mimi nilishamwambia kama anaringa basi mwisho jumatatu wiki hii, tayari tulishakuwa na mipango mizito ya kutafuta mtu wa nafasi yake tena kutoka nje. Unajua Banda sisi tunamchukulia kama kijana wetu anacheza vizuri ndiyo lakini hana uzoefu, anahitaji uzoefu lakini lazima watu wafahamu hata sisi tunataka kunufaika si wao tu wanufaike Banda tunampenda na yeye anajua. Hivyo tumwache kijana acheze soka na nina hakika atafika mbali,"alisema.

Banda anakuwa mchezaji wa tisa kusaini kwa msimu ujao ambapo katika kikosi cha vijana anatimiza idadi ya wachezaji watatu baada ya Yusuf Chuma anayecheza beki wa kati, hamad Juma anayecheza beki ya kulia na Abdi Banda anayecheza beki ya kushoto.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
DAR ES SALAAM, TANZANIA
18 June, 2013

Monday, June 17, 2013

Binslum atangaza donge nono kwa atakaye leta striker kwenye kikosi cha Coastal Union.

 Juma Mgunda akipozi huku anakula njugu, enzi zake huo mwili ulikuwa tishio sana kwa mabeki dhaifu.

Hussein Mwakuluzo Ruga akiwa na familia yake nchini Uingereza anakosihi kwa sasa baada ya kustaafu soka.

Mkurugenzi wa ufundi Coastal Union Nassor Ahmed 'Binslum' ametangaza donge nono kwa shabiki ama mtu yoyote atakaye fanikiwa kuleta mshambuliaji mwenye uchu wa magoli katika kikosi cha wagosi wa kaya.

Alizungumza hayo jana wakati wa kuchangia picha ya mshambuliaji hatari wa timu hiyo Juma Mgunda iliyowekwa katika ukurasa wa facebook na mwanahistoria wa Wagosi Ally Kiraka, ambapo alionyesha kuunga mkono maneno ya mwanandinga mwingine wa zamani wa timu hiyo Hussein Mwakuluzo aliyesikitishwa na viwango vya uchezaji kwa sasa barani ulaya.

"Tokea ligi imeisha natafuta 'striker' mmoja tu na mpaka sasa sijapata si hapa kwetu wala Kenya au Uganda, mmoja tu wa ukweli anayejua kufunga japo nusu ya mgunda sijaona...........sasa natoa nafasi miongoni mwetu Kama kuna striker unafikiri unamjua atakae tufungia goli 15 TU tuletee na wewe utakayetuletea bakhsish juu utapata, haya tusaidiane wadau...!!!!," alisema Binslum.

Awali akichangia mada katika picha hiyo Hussein Mwakuluzo Ruga aliyewika na kikosi kilichotwaa ubingwa wa soka Tanzania mwaka 1988 ambaye kwa sasa anaishi nchini Uingereza na familia yake alisema:

"Mimi nasikia uchungu nikiwaangalia hawa wachezaji wanaosifiwa huku, Wakati uwezo wao ni Wa kawaida sana, wanalipwa hela za ajabu, wanaishi maisha ya ajabu! Wanaendesha magari ya ajabu na wanakaa kwenye nyumba hazina mfano....
Uwezo wao ni Wa kawaida sana Nassor , mchezaji hata kuzuia mpira hawezi! Yaani ....IF I HAD A CHOICE, I WOULD'VE LIKE TO PLAY NOW....THAN IN THE PAST!!," alisisitiza Ruga.

Kutokana na kumfahamu sana Mgunda, Ruga alileta historia fupi ya mchezaji huyo ambaye alikuwa  kama ndugu yake maana kila siku alikuwa akienda naye kwa barabara ya sita Tanga na familia ya kina Ruga ilimchukulia kama ndugu yao hasa ikizingatiwa alikuwa mgeni mjini Tanga.

"Juma Mgunda !!!!! Alitokea cda ya Dodoma bonge la mchezaji alikuwa na vitu vyote alikuwa ana nguvu, anapiga mashuti na ni hodari Wa kupiga vichwa! Pamoja na yote hayo huyu jamaa ni mstaarabu sana ndani na nje ya uwanja, naona ni hadhi kubwa kuweza kucheza na huyu kaka.

"Mimi nimeshaona mechi nyingi hapa England na nimeona wachezaji wanaosifiwa kwamba ni wazuri na wanalipwa mamilioni ya paundi, lakini kila nikiwaangalia hawamfikii huyu jamaa. Ni bahati mbaya kazaliwa Afrika  hivi jamani nisaidieni iwapo wellbeck anachezea Man United na England, na kwa maoni yangu hamfikii Juma hata nusu. Na ninathubutu kusema angekuwa Coastal ile ya kwetu miaka ile huyu wellbeck asingepata nafasi ya kupangwa....." Ruga.

Katika hatua nyingine Coastal Union imeshafanya usajili wa nguvu wa wachezaji wanane wanaotokea timu za hapa nyumbani, ingawa kwa maelezo ya Mwenyekiti wa timu hiyo Hemed Hilal 'Aurora, wamebakisha nafasi mbili tu za kusajili ambapo wanatafuta striker na kiungo mshambuliaji.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
18 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

unamjua mzee Azgar, alikuwa golikipa wa Coastal union. Coastal ikicheza mkwakwani anakwenda kujificha Jet.





Huyu mzee ninaewaletea hapo juu ni mshabiki wa Coastal Union wa miaka hiyo na hadi sasa amekua mzee bado anaipenda Coastal Union kwa moyo wote. Nyumba yake inatazamana na club barabara 11, yeye ndiye alikuwa akiwapa wanachama habari za timu ilipokuwa ikicheza mikoani, kipindi hicho hakukuwa na simu za mikononi na vituo vya radio vilikuwa vichache.

Nakumbuka katika shamrashamra za ubingwa hapo club 1988 huyu mzee alijitolea nyumba yake ikafanywa sherehe, akitegemewa sana kutoa habari kwa njia ya simu timu ikisafiri mikoani simu zilikua za kukoroga.

Anaitwa Azgar, ni Bohora kutokana na mapenzi na timu alikuwa na presha sana timu ikicheza Mkwakwani alikuwa anakwenda baharini Jet mpaka ikifika jioni anasubiri watu wanaorudi kutoka Mkwakwani akisikia 'Mohammed Salim lile goli la 3 kalifunga vizuri sana,' hapo na yeye anarudi haraka kuja kushangilia na wapenzi wenzake alikua na presha sana.

Kwa mujibu wa mchezaji wa zamani wa Coastal Union, Razack Yusuf 'Careca' mzee huyu kipindi cha ujana wake aliwahi kuichezea Coastal Union nafasi ya golikipa.

Imeeandikwa na Ally Kiraka, mwanahistoria wa Coastal Union.
COASTAL UNION
TANGA TANZANIA
17 June, 2013

Mlinzi wa kambi ya timu aliyetokea Singida.

Nikisema wazee wa club basi huyo naweza sema ndo mwenye funguo za club! Huyu mzee hadi leo yupo hapo jirani na club anafanya biashara zake nje ya MINI RESTAURANT.

Huyu mzee alikua ni CLUB TEAM MANAGER miaka ya nyuma, mwenzie wa karibu aliyeshirikiana naye ni marehemu KARABAI MWAKO. Leo nilimtembelea na amefurahi sana, mwenyewe akiiniita we MMAHARA upo?.

Jina lake anaitwa Mzee juma, hata kambi ya karibu na shule ya bombo alikuwepo ni mlinda kambi wa zamani sana alikuja Coastal Union akitokea Singida alikuja kama TX, NI MTU SPESHELI KWA MAMBO YA ULINZI WA KAMBI HATA SASA ANAENDELEA NA ULINZI WA CLUB NA PIA HANA HAJA YA KUJUA LUHA YENU RAZAKI ANAITA RASHAKI.

Imeeandikwa na Ally Kiraka, mwanahistoria wa Coastal Union.
COASTAL UNION
TANGA TANZANIA
17 June, 2013

Sunday, June 16, 2013

Kutana na Binslum, mdau wa soka aliyepania kuinyanyua Coastal Union ya Wagosi wa Kaya

Nassor Ahmed Binslum akiwa ofisini kwake Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
                    Hili ni gazeti la leo la Mtanzania, mwandishi Kambi Mbwana anaandika......

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
ILI timu iweze kufanya vizuri, kunahitaji vitu vingi, kama vile uongozi bora, sambamba uwezo wa kuingiza chochote kitu, maana mpira wa siku hizi ni fedha.

Zipo timu ambazo zinashindwa kutikisa, maana zinakabiriwa na njaa katika mifuko yao, kama vile Villa Squad, Ashanti FC, Toto African na nyinginezo zinazowania nafasi ya kucheza ligi kuu, ukiacha zile zinazomilikwia na
Kampuni au taasisi, kama vile Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, JKT Orjolo, Ruvu JKT, Mgambo Shooting na nyinginezo.

Hali hii kwa sasa haipo tena ndani ya Coastal Union, yenye maskani yake jijini Tanga, maana ina mdau, Nassor Ahmed ‘Bin Slum’, ambaye kwa kupitia moyo wake, mapenzi yake dhidi ya Wagosi wa Kaya hao, mambo yanaonekana mazuri.

Tangu mwaka 2008 alipoongeza mapenzi na msaada kwenye timu hiyo, haijashuka tena daraja, sanjari na kusajili au kutumia kila wanachohitaji, ikiwa ni pamoja na kumudu kuwalipa mishahara wachezaji wote wanaokipiga Coastal Union.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, Bin Slum ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi pamoja na Mdhamini wa Coastal Union, mdau huyo na mnazi mkubwa wa timu hiyo anasema alianza zamani kuisaidia timu hiyo kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo.

Anasema kuwa hapo awali alitaka kukipiga Coastal Union, lakini baada ya kupata ajali yaa kuumia goti uwanjani, ndoto yake ilitoweka rasmi na kubaki kama shabiki mkubwa wa mpira wa miguu, hususan kwenye timu hiyo ya nyumbani kwao.

“Coastal Union ni timu yangu ya nyumbani, nimezaliwa na kusomea Tanga, hivyo nadhani bado nahitaji kufanya kila niwezalo katika kuhakikisha kuwa inasonga mbele.

“Hapo zamani nilikuwa nafanya siri, lakini ukimya huo uliondoka na kuona nijitangaze tu kuwa msaada unatoka ndani ya Kampuni yangu ya Binslum Tyres Company Ltd, ingawa nakiri kuwa siisaidii Coastal nikiangalia faida kwa muda huu, maana ni wazi haiwezi kupatikana,” alisema BinSlum.

Mdau huyo anasema msimu wa 2011 na 2012 waliweza kufanya vizuri na kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi licha ya malengo yao kulilia wasishuke daraja, ila msimu wa 2012/2013 hali imebadilika baada ya kuambulia naafsi ya sita.

Anasema si matokeo mabaya kwa timu yao, maana timu kama Coastal Union ina changamoto nyingi, ikiwamo uwezo wa kifedha, malengo na ushirikiano kwa wachezaji wake.

BinSlum anasema kuwa tayari wameanza kufanya usajili wenye dhamira ya kuifanya Coastal inyakuwe ubingwa msimu ujao, wakimsajili Haruna Moshi Boban na Juma Nyosso wote kutoka Simba.

Wengine waliosajiliwa Coastal Union ni pamoja na Markus Ndehele na Said Lubao wote kutoka JKT Orjolo, wakati Abdallah Athuman Ally huyu anatokea Jamhuri ya mjini Pemba, ambaye pia ni mchezaji bora katika soka la Zanzibar na Kennet Masumbuko aliyesajiliwa kutoka Polisi Morogoro.

Msimamo wa Coastal Union ni kuwa hawana udugu kabisa na timu za Simba na Yanga, kama baadhi yao wanavyofikiri, isipokuwa uswahiba huo utakuwapo katika masuala ya Kitaifa.

Anasema wapo baadhi ya watu wanasema kuwa timu ya Coastal Union ina urafiki na Simba, jambo ambalo halina ukweli wowote, hivyo .
Said Lubao, wua wakati soka u wa Benchi la
 Chanzo: Handeni kwetu blog.

Friday, June 14, 2013

Picha hii ilitolewa wiki chache kwenye ukurasa wa facebook wa Coastal Union

Leo nimewaletea picha ya kambi ya coastal union iliyokua jirani na shule ya msingi bombo!angalieni vizuri hiyo picha mutaniona ally kiraka huyo alovaa kishati cha bahama!nilianza kuipenda coastal toka utoto wangu na nilikua karibu sana na timu, naijua vizuri Coastal, hehehe mimi ndiyo Coastal Union bwana! Hapo nilikua napiga makofi kuwapa hamasa wachezaji na sipendi majungu. Hayo ni maneno ya Ally Kiraka.

Baadaye akaingia Hussein Mwakuluzo katika ukurasa akaandika hivi "Hapo namuona mzee mbunge aliyesimama, na huyu aliyekuwa karibu na Ali ni Ali Haniu, na aliyekuwa kushoto kwa mzee mbunge ni Mohammed Mwameja, na yule anaefunga viatu ni Jangalu!'
Asante kwa kumbukumbu!

Kumbukumbu za Ally Kiraka zinaanza kuingia kwenye blog...


Wadau mnawakumbuka hawa? kutoka kushoto ni Said Salim 'Kolongo,' Ali Mwaliza na Mohammed Kampira 'Kaball'.


Hawa ni wachezaji wa coastal union! watakumbukwa sana hawa wachezaji kwa heshima waloileta 1988!kila mchezaji alikua na heshima yake na jina lake la utani!kuna anaeitwa kaball,kuna anaitwa hapitiki,ila huyo wa kati alikua na cfa ya mtibuaji mipira,alikua akicheza no.4,huyo ndie alimchana nyama KURWA shabaan wa african sports na akala RED CARD!haya nimeanza tena kuleta kumbukumbu!


Kiraka
Tanga Ngamiani.

Bunduki za Coastal Union msimu ujao, hizo ni bunduki nane bado mbili ambazo zitakuwa kutoka nchi za nje..

 Kiungo machachari wa Simba na timu ya Taifa wakati fulani Haruna Moshi 'Boban' akitia saini kuichezea Coastal Union msimu ujao mbele ya kocha mkuu wa Wagosi wa kaya Hemed Morocco.

 Yusuf Chuma kutoka timu B naye akisaini mkataba wa miaka mitatu kuichezea Coastal Union mbele ya makamu mwenyekiti Steven Mnguto.

 Hamad Juma akikokota mpira katika mechi ya mzunguko wa pili dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Ingawa matokeo yalikuwa 2-1 na Simba kutoka kifua mbele lakini kijana huyu wa timu B alifanya vizuri sana mpaka kocha Hemed Morocco akaamua kumsainisha mkataba wa miaka mitatu kuichezea Coastal Union.

 Makamu mwenyekiti wa wagosi wa kaya Steven Mnguto akishikana mkono na golikipa kutoka JKT Oljoro, Said Lubawa.

 Marcus Ndehele kutoka JKT Oljoro akitia saini kuichezea Coastal Union kwa msimu ujao.

 Juma Said 'Nyosso' kutoka Simba akiwa na makamu mwenyekiti wa Coastal Union Steven Mnguto mara baada ya kumwaga wino kuichezea timu yetu kwa msimu ujao.

 Abdullah Othman Ally kutoka Jamhuri ya Pemba akiwa na kocha mkuu wa Coastal Union Hemed Morocco, punde baada ya kusaini kuichezea Coastal kwa msimu ujao.

Keneth Masumbuko kutoka Polisi Morogoro akishikana mkono na Makamu Mwenyekiti wa Coastal Union Steven Mnguto mara baada ya kuahidi kufanya vema msimu ujao akiwa kikosini.



"Utakumbuka msimu uliopita timu yetu imevutia mashabiki wengi wa soka kutokana na aina ya uchezaji tuliouonyesha, tulikuwa na malengo makubwa lakini hayakutimia mwalimu (Hemed Morocco) ameliona hilo na ndiyo maana wachezaji tuliowasajili yeye ndiye aliyewapendekeza hivyo msimu ujao ni burudani tupu hizi timu zinazopenda kujisifia tunaziomba zijiandae kwa mvua ya mabao," alisema Aurora.

Aidha kwa mujibu wa Aurora katika wachezaji wanane ambao wanategemewa kuingarisha Coastal Union, watatu ni vijana wa timu ndogo ya Wagosi ambao waliwika wakati wa kombe la Uhai chini ya miaka 20 mwaka jana, wachezaji wawili wanatoka Simba wakati wawili wengine wanatoka JKT Oljoro, mmoja anatoka Zanzibar katika timu ya Jamhuri ya Pemba ambaye katika msimu ulioisha alikuwa mchezaji bora wa michuano na mmoja anatoka Polisi Morogoro.

"Tumefanikiwa kunasa wachezaji wawili kutoka Simba, Haruna Moshi 'Boban', Juma Said 'Nyosso', JKT Oljoro tumenasa wawili ambao ni beki Marcus Ndehele na golikipa Said Lubawa, kuna mchezaji wa Jamhuri ya Pemba ni kiungo anaitwa Abdullah Othman Ali, wakati Polisi Morogoro tumemnasa Kenneth Masumbuko huyu ni mshambuliaji, katika timu B tumewapandisha Hamad Juma na Yusuf Chuma kuna mtoto mmoja wa timu B bado hatujamalizana naye lakini pia tutampandisha," alisema.

Naye msemaji wa timu hiyo Eddo Kumwembe, amewataka mashabiki wa Coastal Union kuwa na umoja wakati wa kipindi hiki cha usajili kwani kutazungumzwa mengi ambayo yanalenga kuleta siasa za soka, kwani hakuna timu ambayo inapenda kuona inapoteza mchezaji mzuri lazima watatengeneza fitina ili aonekane mkorofi ama hafai.

"Katika huu usajili nitazungumzia kuhusu wachezaji wawili Juma Nyosso na Boban 'Haruna Moshi', Boban ni kiungo wa uhakika tumemchukua ili kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji, tayari tumeshazungumza naye tunaamini ni mtu mzima hatuangalii maisha yake ya nje ya uwanja bali tunahitaji msaada wake ndani ya dimba wakati wa dakika tisini za mchezo.

"Yatazungumzwa mengi lakini tunaamini Boban ametuelewa na ametuahidi kucheza soka la uhakika, na kuhusu Nyoso, heheheeeeee (anacheka) ninashangaa sana watu wanaotubeza kwa kumsajili Nyoso kuna timu inamtaka ipo Afrika Kusini, kama hiyo haitoshi Libolo ya Angola nayo inamuhitaji tunataka nini tena," aihoji Eddo.

Coastal Union ambayo ilirudi katika ramani ya soka katika msimu wa 2011/12 ambapo ilimaliza nafasi ya tano katika msimu ulimalizika wa 2012/13 imeshika nafasi ya sita lakini imeleta ushindani kwa timu ambazo zimekuwepo katika ligi kwa muda mrefu, hivyo wanaamini msimu ujao utakuwa mzuri kwa usajili uliofanyika chini ya kocha mkuu wa timu hiyo Hemed Morocco na msaidizi wake Ally Mohammed 'Kidi' pamoja na kocha wa walinda mlango Juma Pondamali 'Mensah'.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
Tanga Tanzania
14 June, 2013

blogu imerejea mitamboni, poleni wadau mliokuwa mkiikosa.

Kunradh mashabiki wetu,

Kwa kipindi kirefu blogu yetu imekuwa kimya, ni kutokana na matatizo ya kiufundi. Lakini tunashukuru kwa sasa hali imetengemaa na tutaendelea kuwaletea taarifa za kila siku kuhusiana na klabu yetu tunayoipenda.

Hasa ukizingatia hiki ni kipindi cha usajili na maandalizi ya msimu ujao wa 2013/14 hivyo tutaendelea kuwaletea mambo mazuri kuhusiana na shughuli za kila siku zinazohusiana na klabu.

Kadhalika tunategemea kuwa na mkutano mkuu wa wanachama, yatajadiliwa mengi kadhalika picha nyingi tutaziweka humu kwa kumbukumbu kwa wale waliohudhuria mkutano huo. Punde baada ya kupata taarifa kamili kutoka kwa viongozi juu ya ajenda na mambo mengine yanayohusiana na mkutano tutawaarifu.

Vilevile ukurasa wetu wa facebook umeanzisha utaratibu wa kuwakumbuka wachezaji wa zamani wa Coastal Union, pamoja na vibweka vya mashabiki wakiwa uwanjani. Tutakuwa pamoja na mwanahistoria wetu Ally, almaaruf Ally Mmahara au Kiraka. Yeye atakuwa na nafasi maalum katika blogu hii kutuletea historia pamoja na picha.

Wenu katika ujenzi wa chama kubwa, Coastal Union 'Wagosi wa kaya'.

COASTAL UNION
TANGA, TANZANIA
14 June, 2013