Makamu mwenyekiti Steven Mnguto akimweleza mawili matatu Banda kabla ya kutia saini mkataba wake.
Banda akiwa na ndugu yake Meddy ambaye ni mtoto wa Abdul Bosnia, hapa wanapitia mkataba kabla ya kuutia saini.
Hapa akihakikisha anaweka saini kila kurasa ya mkataba ili isiweze kughushiwa kwa namna yoyote ile iwe kuongezwa kurasa ama kunyofolewa kurasa.
Mzee Mnguto mzuka ulikuwa umempanda wakati akitoa somo kwa Banda umuhimu wake katika timu.
Hii ni hatua nzito kufikiwa, kupeana mikono ndiyo njia sahihi ya kuonmyesha wamekubaliana.
Father naye alitoa mkono kuonyesha kuafikiana na kila kitu kuhusu mtoto wake kuendelea kuwa mpinzani, kwani yeye ni African Sports damu huku kijana wake atakuwa Coastal Union damu.
Pesa sabuni ya roho |
Banda ambaye ameonyesha uwezo wa hali ya juu amekubaliana kukitumikia kikosi cha wagosi wa kaya kwa miaka mitatu ambapo makamu mwenyekiti wa Wagosi Steven Mnguto alikuwa shahidi upande wa timu na shahidi wa beki huyo alikuwa meneja wake Abdul 'Bosnia' Father ambaye ni mchezaji wa zamani wa Afrcan Sports 'Wana kimanumanu' ambao ni mahasimu wakubwa wa wagosi wa kaya.
Akizungumza baada ya kutiliana saini Abdul Bosnia 'Father' alisema Banda amefurahi sana kucheza tena katika kikosi cha wagosi kwani hakuna namna nyingine bora itakayomwezesha kuonekana zaidi ya kucheza timu ya hadhi ya Coastal Union.
"Mimi nilikuwa Sports damu lakini hilo halikuzuii wewe kuwa Coastal damu kwani haya ni maisha yako, mwenzio nilikuwa naipenda timu yangu kwasababu ndiyo iliyonilea hivyo nakuomba ufanye hivyohivyo," alisema Father kumwambia mwanawe Banda na kuongeza.. "Waheshimu wachezaji wenzako, waheshimu walimu, viongozi na mashabiki, hakika utafanikiwa.
"Wakati marafiki zangu Hussein Mwakuluzo na Razack Yusuf 'Careca' walipohamia Coastal Union kutoka African Sports nami nilitaka kuwafuata, lakini wazee wa timu waliniambia nibaki African Sports kwani hapo ndipo nilikuwa na uhakika wa kupata namba kikosi cha kwanza, hivyo hata wewe hapa Coastal Union ndipo nyumbani kwako."
Katika hatua nyingine baada ya kuonekana suala la Banda kusaini Coastal Union limekuwa gumu wadau waliamua kuhaha na kufanya kila jitihada kuhakikisha kijana huyo anamwaga wino. Miongoni mwa mashabiki waliowasiliana na blog hii kutoka Tanga ni Miraji Wandi 'Shoka' ambaye alieleza juhudi zake na kusema:
"Mimi namfahamu Banda tangu akiwa mdogo, tangu anaanza kujiunga na kikosi B chini ya kocha Bakari Shime, nilifanya naye mazungumzo ya ana kwa ana lakini bado alionekana mgumu, nikajua kuna watu wanamshauri vibaya kwakuwa nafahamu banda anamuheshimu sana kocha wake Hemed Morocco nikaamua kufanya 'conference call' tukaanza kuzungumza mimi, Banda na Morocco.
"Morocco alizungumza maneno mazito sana, na nadhani ndiyo sababu ya banda kuamua kutumia akili yake badala ya akili za kuambiwa, na leo amesaini hakika ni furaha kubwa kwangu," alisema Wandi.
Naye mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo Nassor Binslum aliweka wazi kuwa alishaanza kuudhika kutokana na kitendo cha Banda kuonekana anashauriwa vibaya na kusahau fadhila za timu yake iliyomlea tangu akiwa hajui mpaka sasa anatajika katika soka la Tanzania.
"Mimi nilishamwambia kama anaringa basi mwisho jumatatu wiki hii, tayari tulishakuwa na mipango mizito ya kutafuta mtu wa nafasi yake tena kutoka nje. Unajua Banda sisi tunamchukulia kama kijana wetu anacheza vizuri ndiyo lakini hana uzoefu, anahitaji uzoefu lakini lazima watu wafahamu hata sisi tunataka kunufaika si wao tu wanufaike Banda tunampenda na yeye anajua. Hivyo tumwache kijana acheze soka na nina hakika atafika mbali,"alisema.
Banda anakuwa mchezaji wa tisa kusaini kwa msimu ujao ambapo katika kikosi cha vijana anatimiza idadi ya wachezaji watatu baada ya Yusuf Chuma anayecheza beki wa kati, hamad Juma anayecheza beki ya kulia na Abdi Banda anayecheza beki ya kushoto.
COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
DAR ES SALAAM, TANZANIA
18 June, 2013
No comments:
Post a Comment