Wednesday, June 19, 2013

Aggrey Chambo 'Mkombozi'

Aggrey Chambo akionekana alivyo sasa amedhoofu tofauti na kipindi alichokuwa akicheza mpira.

Aggrey Chambo, miongoni mwa vifaa vilivyosaidia kupeleka heshima ya soka mkoani Tanga alikuwa mzuri katika kuchungulia nyavu.

Itakumbukwa goli lake la kusawazisha dhidi ya Miembeni kombe la muungano msimu wa 1988/89 ndilo lililotupa nafasi ya pili nyuma ya African Sports na kutupatia ticket ya kushiriki kombe la washindi barani Africa na kutolewa na Ferraviaro ya msumbiji.

Hussein Mwakuluzo anaeleza kuwa "Hiyo mechi na miembeni naikumbuka vizuri sana, nilicheza mechi nikiwa na malaria, zikiwa zimesalia dakika tano mpira kwisha nikawa siwezi kuendelea na mechi, ndiyo nikatoka akaingia Aggrey! Mpira wa kwanza alioupata akampiga kanzu Riffat Said akafunga goli."

Mwakuluzo anaongeza kuwa "Nakumbuka mechi hiyo ilikuwa na ushindani sana nakumbuka nilibaki na Riffat Said, mara kadhaa na zote aliokoa, mwaka uliofuata Riffat akasajiliwa na Coastal Union."

Jina jingine la Aggrey aliitwa Mkombozi, kwasababu alikuwa akiingia lazima abadili matokeo, Ally Kiraka anasema "Nakumbuka mechi na Simba uwanja wa Mkwakwani Mohammed Mwameja ndiyo amesajiliwa Simba, mechi hii Aggrey alibishana sana na Mwameja na hiyo mechi ilikua na vurugu sana nje ya uwanja mpaka ndani ya uwanja.

"Tulipata penati Kassa Mussa kwa presha akakosa ndipo 'Mkombozi' Aggrey Chambo akasawazisha tukatoka suluhu na Simba ya 1-1 tukawatibulia ubingwa wao ndipo vurugu kubwa watu wa 'sweat corner' wakapigana na wachezaji wa simba pamoja na washabiki wao. Buma, alipigana na watu kama 10 ila alikua na nguvu ndiyo siku tuliyovunja undugu na Simba."

Kudhihirisha ukombozi wake Aggrey Chambo katika mechi dhidi ya African Sports, Mombasa Stadium alikomboa goli halafu Juma Mgunda akafunga goli la kuongoza mpaka mpira unaisha Coastal Union 2 African Sports 1, ilikua ni kwenye sherehe za Uhuru wa Kenya mwaka 1990 timu zote zilialikwa.

Kwa sasa legend huyu Aggrey Chambo anasumbuliwa na maradhi, mwili wake ni dhaifu sana, kwa sasa mtu pekee anayemsaidia ni golikipa wa zamani wa Coastal Union, Simba na timu ya Taifa Mohammed Mwameja ambaye ametoa pesa katika hoteli mojawapo eneo la karibu analoishi Chambo jijini Dar es Salaam ambapo anapata chakula kila siku.

Ukijisikia kumsaidia kwa hali na mali piga namba hizi 0714392601 ukipiga atapokea kijana mmoja anaitwa Uledi ndiye anayekaa na Aggrey, useme nataka kuongea na Aggrey ataitwa maana hana simu.

COASTAL UNION
19 June, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA


No comments:

Post a Comment