Saturday, March 8, 2014

Coastal Union 0-0 Ashanti UTD

 Kocha wa Ashanti UTD, Abdallah King Kibadeni akifuatilia mchezo wa jana, baada ya mechi alisema amefurahishwa na suluhu kwani aliipokea timu ikiwa taaban kazi yake ni kuhakikisha haishuki daraja ili ajipange kwa msimu ujao.

 Vifaa hivi vya Wagosi, kutoka kushoto Haruna Moshi 'Boban', Mbwana Kibacha, Abdi Banda, Juma Nyoso, Jerry Santo na Shaaban Kado.

                                                        Mamaaaa Aminaaaaaa '...'

 Crispian Odula akipiga shuti langoni mwa Ashanti, huku Danny akijiandaa kuenda kuleta mishemishe langoni.

 Mwamuzi wa jana Alex Mahagi akimwangalia Ally Nassor 'Ufudu' na mchezaji wa Ashanti wakiminyana katika uwanja wa Mkwakwani jana.

 Kenneth Masumbuki akitafuta mbinu za kumtoka mchezaji wa Ashanti jana.

                                                "Niachie bwanaaaa" Danny Lyanga

                                            Haruna Moshi 'Boban' akiwa amevurugwa jana.

 Mkurugenzi wa Ufundi Coastal Union Nassor Binslum(mwenye kofia)  akionyeshwa kitu na Katibu wa timu hiyo Kassim Siagi uwanja wa Mkwakwani jana.

 Mwenyekiti wa Coastal Union (kushoto) akiwa na mwenyekiti wa chama cha soka Dar es Salaam, ambae pia ni shabiki mkubwa wa Ashanti UTD, Almas Kasongo jana Mkwakwani.

                                                           Masumbuuukooo... in the move.

              Abdi Banda akiwa na mpira huku akiwa hajui afanye nini, apige pasi ama aombe Mungu.



TIMU ya soka Tanzania Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ wamelazimisha suluhu ya bila kufungana na Ashanti UTD katika dimba lao la kujidai la Mkwakwani jijini Tanga.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Wagosi walionekana kuwa makini kuanzia dakika ya kwanza baada ya kipyenga cha mwamuzi kutoka Mwanza, Alex Mahagi kupulizwa huku mashabiki wa timu hiyo wakiwa na hamasa ya ushindi.
Aidha, kudhihirisha Wagosi walikuwa na nia ya kuwaumiza vijana wa Ilala Ashanti UTD iliyoanzishwa mwaka 2004, dakika ya kwanza walipata kona iliyochongwa na winga hatari Danny Lyana lakini kwa bahati mbaya haikuzaa matunda.
Mchezo wa jana uliendelea hivyohivyo kwa Wagosi kulisakama lango la Ashanti, huku wapinzani wao wakifanya mashambulizi ya kushtukiza lakini umakini wa mabeki wazoefu na uimara wa golikipa Shaaban Kado, alietoka kuitumikia nchi yake nchini Namibia uliwanyima mabao Ashanti.
Ilipotimu dakika ya 33, kipindi cha kwanza beki wa kati wa Wagosi, Juma Nyoso alipata pasi muru akutoka kwa Abdi Banda ambae nae alikuwa nchini Namibia katika kikosi cha Taifa Stars waliotoka suluhu ya 1-1. Nyoso aliupokea vizuri mpira huo na kuwazidi ujanja mabeki wa Ashanti akabaki na golikipa akaupiga kiufundi lakini ulipaa juu sentimeta chache mashabiki wa Wagosi wakainuka.
Dakika chache baadae Haruna Moshi ‘Boban’ alikosa bao la wazi baada ya kuwekewa na Crispian Odula lakini shuti lake alilolipiga kiufundi lilitoka nje.
Hata hivyo baada ya mishemishe nyingi katika lango la Ashanti ambazo hazikuzaa matunda, vijana hao wa Ilala walibadilika na kuanza kulisakama lango la Wagosi ambapo walipata nafasi tatu za harakaharaka lakini ilikuwa bahati tu wala si ufundi wa Kado uliosaidia kutotikisika nyavu katika lango la Wagosi walioonyesha kuishiwa mbinu.
Kipindi cha kwanza kiliisha hivyo bila timu yoyote kuona lango la mwenzake. Wachezaji walikwenda mapumziko wakisindikizwa na makocha wao King Abdallah Kibaden wa Ashanti na Yusuf Chipo wa Coastal Union.
Kipindi cha pili Coastal Union walifanya mabadiliko kwa dakika tofauti ambapo walitoka Crispian Odula na Ally Nassor ‘Ufudu’, na kuingia Yayo kato na Mohammed Mtindi.
Mabadiliko hayo yaliamsha ari ya ushambuliaji lakini dakika ya 49 kipindi cha pili Danny Lyanga aliwanyima furaha mashabiki wa Coastal Union, baada ya kushindwa kumalizia kazi nzuri na Kenneth Masumbuko aliewazidi mbio mabeki wawili wa Ashanti na kupiga krosi muru iliyomkuta Danny yeye na golikipa wa Ashanti lakini akapiga fyongo.
Hali iliendelea kuwa ya piga nikupige mpaka ilipotimu dakika ya 65 golikipa wa Wagosi Shaaban Kado aligongana na mchezaji wa Ashanti akaumia mkono hivyo kushindwa kuendelea na mchezo akaingia golikipa namba mbili Said Lubawa, ambae alimudu kulinda lango hilo.
Kosa kosa zilikuwa nyingi kwa pande zote mbili ambapo Yayo Kato alishindwa kucheka  na nyavu mara mbili akiwa eneo la hatari.
Kwa matokeo hayo ya 0-0, Ashanti watoto wa jiji wameambulia point moja na kuendelea kudunduliza point zao ambapo kwa sasa wana point 18, katika nafasi ya 12 wakigombania kutoshuka daraja.
Wagosi wa Kaya nao wameshuka mpaka nafasi ya saba kutoka ya sita baada ya kuambulia point 26, wakiwa nyumba ya Kagera Sugar wenye point 29 nafasi ya tano, huku Ruvu Shooting wakikwea mpaka nafasi ya sita kutoka ya nane baada ya kuwachapa Tanzania Prisons, bao 1-0 mjini Mbeya jana na kujizolea point 28.
Mechi ijayo Wagosi watasafiri mpaka Dar es Salaam, kumenyana na Simba katika uwanja wa Taifa. Lakini mpaka sasa haijajulikana mechi hiyo itachezwa lini ambayo katika ratiba inaonyesha ni Jumatano Machi 12, lakini zipo taarifa kuwa viongozi wa Simba na Coastal Union wameiomba TFF kupitia kamati ya ligi, kuwa meci hiyo isogezwe mpaka Jaumamosi Machi 15 kwa lengo la kupata mashabiki wengi.
COASTAL UNION
TANGA, TANZANIA
9 MACHI, 2014   


1 comment:

  1. Mwandishi, timu gani Upo? nani (timu) alielazimisha suluhu? hariri kwanza tafadhali kabla kuiposti habari.

    ReplyDelete