COASTAL Union, wameudhihirishia umma kuwa mwaka jana walipoingia fainali ya Uhai Cup, hawakubahatisha baada ya kuwatoa Azam FC, katika mechi ya leo hatua ya nusu fainali ya kombe hilo uwanja wa Chamazi, Azam Complex jioni hii.
Kufungwa kwa Azam FC bao 1-0, imekuwa pigo kubwa kwa timu hiyo hasa ikizingatiwa katika mechi ya ufunguzi walitandikwa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Karume Ilala jijini.
"Sisi kwa sasa tumeshafuta rekodi yao ya kutufunga mara mbili, walitufunga katika mechi ya fainali michuano hii hii mwaka jana baada ya dakika tisini wakatufunga kwa matuta. Baadaye mwaka huu katika michuano ya Rollingstone jijini Arusha wakatutoa kwa matuta kwenye hatua ya nusu fainali.
"Sasa sisi tumelipiza vipigo vya katika michuano hii hii, wao walitufunga katika michuano miwili tofauti tena kwa matuta, lakini sisi tumewafunga mara mbili mfululizo kwa tofauti ya wiki moja tu tena kwa dakika tisini," alijitapa beki wa kushoto wa Coastal Union Ayoub Masudi.
Bao la Wagosi lilipatikana dakika ya 32 kipindi cha kwanza baada ya Ally Nassor 'Ufudu' kukimbia na mpira kitokea katikati na kumpenyezea Mohammed Rajab ambaye aliwekwa kati na mabeki wawili wa Azam FC, lakini akawashinda nguvu na mbio, mwisho akabaki yeye na kipa, akapiga shuti hafifu ambalo lilipita juu ya goikipa huyo ambaye aliinua macho bila msaada huku mpira ukitinga wavuni.
Baada ya hapo Coastal Union, walicheza mpira wa kasi na kuonana hali iliyozidi kuwachanganya Azam ambao walikuwa wakizomewa na uwanja mzima.
Mpaka mapumziko matokeo yalibaki hivyohivyo 1-0, kipindi cha pili Azam walirudi na ari wakacheza nusu uwanja kwa takriban dakika ishirini, Coastal Union walionekana kupoteza mwelekeo na hawajui cha kufanya.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya kocha wa Azam kuingiza wachezaji wannne ndani ya dakika tano, hali iliyowafanya Wagosi kuzidi kuelemewa na kuamua kurudi nyuma kulnda lango badala ya kuongeza bao la pili.
Awali wakati kipindi cha pili kinaanza Kocha Joseph Lazaro alimtoa Mohammed Issa 'Banka' na kumuingiza Hussein Amir 'Zola. baadaye ilipotimia dakika ya 40 alitoka Mahadhi Juma, ambaye leo alicheza chini ya kiwango na kuingia Dihile Said, kabla ya mchezo kuisha aliingia Ramadhan Juma 'Batisata' na kutoka Mohammed Rajabu.
Coastal Union dakika kumi za mwisho walicheza soka la kuvutia na kujiamini kiasi walishangiliwa na uwanja mzima.
Mechi ya fainali itakayochezwa Jumapili wiki hii saa tisa alasiri uwanja wa Chamazi, inasubiri mshindi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar ambayo itapigwa kesho uwanja wa Chamazi.
COASTAL UNION
28 NOVEMBA, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA
No comments:
Post a Comment