Tuesday, November 19, 2013

Coastal Union yakubali uteja mbele ya Yanga mechi za Uhai U20.












LEO vijana wa Coastal Union wamekubali uteja kwa kuchapwa bao 1-0 na vijana wa Yanga kwenye michuano ya Uhai inayoshirikisha timu za vijana zinazoshiriki Ligi kuu ya Vodacom, katika uwanja wa Karume Ilala jijini Dar es salaam.
Mechi hiyo iliyochezwa asubuhi saa mbili na kukamilika saa tatu na nusu, ilikuwa na ushindani mkubwa katika kipindi cha kwanza ambapo vuta nikuvute kati ya timu hizo ilikuwa kali, na hakukuwa na timu iliyotabiriwa kutoka kifua mbele kutokana na wote kucheza mchezo wa kujihami.
Kipindi cha pili kilianza kwa Coastal Union kulikamia lango la Yanga lakini mabeki wa timu hiyo walikuwa makini kuhakikisha golikipa wao hapati kashkash zozote.
Coastal Union walianza kuonekana kukata tama ya ushindi baada ya kushindwa kutumia vema nafasi nyingi walizopata katika dakika ya 50 na 60 ya mchezo.
Ilipofika dakika ya 65 Yanga waliliandama lango la Coastal Union hali iliyowafanya mabeki wa pembeni kupoteza mwelekeo hasa beki wa kulia Aoub, alionekana kuzidiwa nguvu.
Nahodha wa timu hiyo Nzara Ndaro, naye alionekana kucheza chini ya kiwango hali iliyomfanya kupoteza mwelekeo na kufanya nafasi aliyokuwepo, beki wa katikati kuonekana kamaa haina mwenyewe.
Ilipofika dakika ya 68 Hamis Issa wa Yanga aliipatia bao la kwanza na la pekee katika mechi ya leo baada ya piga nikupige katika lango la Wagosi na kumuacha golikipa akiwa peke yake mabeki wameanguka pembeni. Hamis akautumbukiza mpira wavuni baada ya kupokea krosi kutoka upande wa kushoto.
Hali iliendelea hivyo mpaka dakiak tisini za mchezo kukamilika, ubao ukawa unasomeka Yanga 1-0 Coastal Union.
Kutokana na matokeo hayo Yanga wamejizolea point sita na mabao mawili baada ya mechi ya kwanza kuwafunga Mbeya City bao 1-0. Coastal Union wataendelea kubaki na point tatu na mabao mawili baada ya mechi ya juzi kuwafunga mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC mabao 2-1 katika uwanja huohuo wa Karume.
Mechi ijayo ya Coastal Union katika kundi lao itachezwa katika uwanja wa Chamazi Saa kumi alasiri siku ya Jumamosi Novemba 23.
Hii ni mara ya pili Coastal Union, wanashiriki michuano hiyo ya Uhai ambapo mwaka jana walifika mpaka hatua ya fainali wakatolewa kwa matuta na Azam FC.
COASTAL UNION
NOVEMBA 19, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment