Thursday, October 10, 2013

Coastal Union kuvaana na Ashanti bila Boban, Hamadi.



JINAMIZI la kadi nyekundu linazidi kuiandama klabu kongwe ya Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' baada ya wiki iliyopita beki kinda Hamadi Juma 'Basmat', kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba, baada ya kupishana maneno na mchezaji wa Azam FC Kipre Tchetche.

Hali hiyo inamfanya Hamadi kuungana na kiungo mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban', ambaye alionyeshwa kadi nyekundu mjini Mbeya katika mechi baina ya Wagosi wa Kaya na Mbeya City.

Kukosekana wachezaji hao katika mechi itakayochezwa Octoba 12, siku ya Jumamosi kati ya Ashanti United na Coastal Union kwenye uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, kutamlazimisha mwalimu wa Wagosi, Hemed Moroco kubadili mfumo wa ushambuliaji kwa mara nyingine baada ya awali kumtumia Boban kucheza nafasi ya kiungo namba nane, lakini baadaye akawa anamtumia kama mshambuliaji wa kati, katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Tanga ambapo iliisha kwa sluhu ya bila kufungana mwalimu Moroco aliwatumia mganda Yayo Kato na Pius Kisambale lakini mfumo huo haukuonekana kuleta uhai.

Kwa mujbu wa mwalimu msaidizi wa timu hiyo, Ally Ahmed 'Kidi' Wagosi wa Kaya wana mifumo mingi ambayo huwasaidia kubadilika kila wanapokutana na timu yenye mfumo tofauti. Mathalan kwa kipindi kirefu walikuwa wakitumia mshambuliaji mmoja mbele, lakini mechi ya juzi walitumia washambuliaji wawili. Hivyo katika mechi ya Ashanti wanaweza kubadilika na kutoka kivingine.

"Sisi hatutumii mfumo mmoja, wapinzani wetu wanatujua kwa namna tunavyobadilika na ndiyo maana utaona wanatumia zaidi msaada wa waamuzi kwa kuwanunua maana wanajua hawatuwezi," lisema Kidi.

Hata hivyo Coastal Union ipo katika hatihati ya kuwa timu isiyo na nidhamu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya kadi nyekundu baada ya mpaka mechi ya saba kufikisha idadi ya kadi nne kati ya kadi 12 zilizotoka katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara mpaka sasa.

Baada ya mechi ya Ashanti Jumamosi wiki hii, Wagosi watasafiri mpaka Bukoba katika uwanja wa Kaitaba kukutana na wakata miwa wa Kagera, kagera Sugar.

Mpaka saa Coastal Union yenye makazi yake Jijini Tanga, imeshacheza mechi Saba imeshinda mbili na kutoa suluhu tano, na kuwa miongoni mwa timu nne ambazo hazijapoteza hata mechi moja tangu ligi ianze. Timu hizo ni (Simba, Azam FC, Mbeya City na wao Coatal Union).

Aidha Wagosi wamefikisha pointi 11 ikiendelea kushikilia nafasi ya tano katika msimamo wa ligi baada ya Simba, Yanga, JKT Ruvu na Azam.

COASTAL UNION
OCTOBA 11, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment