Mwalimu msaidizi wa Coastal Union Ally Ahmed ‘Kidi’ ameweka
wazi kuwa timu yake ipo vizuri kilichobaki ni kuangalia namna watakavyojituma
uwanjani siku ya kesho dhidi ya Simba Sport Club.
Akizungumza na blogu hii Kidi, ameonyesha kujiamini
kukabiliana na Simba wenye point 19 wakishikilia nafasi ya tatu chini ya Azam
na Mbeya City.
Mechi hiyo itakayochezwa katika uwanja wa Mkwakwani Jumatano
Oktoba 23, itaamua hatma ya Wagosi wa Kaya wanaosuasua katika ligi baada ya
kupoteza michezo miwili mfululuzo kati ya Ashanti United na Kagera Sugar.
Wagosi ambao wamecheza mechi mbili nje ya Tanga na kupoteza
zote, wameahidi kurudisha heshima ya soka mkoani humo kwa kuanza kampeni ya
kushinda mechi zote tatu watakazocheza uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani, ambazo
ni kati ya Simba, Mtibwa Sugar na Mgambo JKT.
“Sisi tupo vizuri ingawa nafsi yangu haina raha baada ya
kupoteza michezo miwili mfululizo, vijana wangu wapo vizuri wanacheza kwa
kuonana lakini hata sijui sababu ni nini wanashindwa kufunga. Naamini wataamka
katika mechi hii, najua Simba ni timu nzuri na kubwa, lakini sidhani kama
vijana wangu watakubali kufungwa kirahisi,” alisema Kidi.
Katika hatua nyingine bado suala la Kocha Mkuu wa timu hiyo
Hamed Moroco halijakaa sawa baada ya maneno mengi kuzungumzwa bila kupatikana
muafaka.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa viongozi wa Wagosi, kocha
huyo tayari amemaliza mkataba wake na bado wapo kwenye majadiliano ima
kumuongezea mkataba ama kufanya mazungumzo na kocha mwingine. Wamewataka
mashabiki kuwa wapole wakati mchakato wa kocha ukifanyika, wakaweka wazi kuwa
baada ya kujiengua msemaji wa timu Edo Kumwembe, kwa sasa mwenye mamlaka ya kutoa
taarifa zozote ni mwenyekiti tu Hemed Hilal ‘Aurora’.
Aidha Coastal Union ipo nafasi ya 9 ikiwa imecheza michezo 9
kati ya 13, wamejizolea point 11 wakiwa wameshinda michezo miwili, suluhu tano
na kupoteza miwili.
Baada ya mechi dhidi ya Simba, Coastal Union watashuka
dimbani dhidi ya Mtibwa Sugar katika uwanja wa Mkwakwani Oktoba 26 siku ya
Jumamosi, Oktoba 30 dhidi ya Mgambo JKT uwanja wa Mkwakwani na kumalizia
mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya JKT Ruvu Novemba 2 siku ya Jumamosi katika
uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.
COASTAL UNION
22 OKTOBA, 2013
TANGA, TANZANIA
No comments:
Post a Comment