Bundi bado hajaondoka kwenye paa la Coastal Union baada ya
jana kupoteza mchezo mwingine dhidi ya Kagera Sugar ya mjini Kagera, lilikuwa
ni bao la mkwaju wa penati lililotiwa kimiani na Salum Kanoni dakika ya 58
kipindi cha pili baada ya beki wa Coastal Union kuunawa mpira eneo la hatari.
Kagera Sugar hawakuonekana kuwa na uhai katika kipindi cha
kwanza lakini wachezaji wa Wagosi walishindwa kutumia vema udhaifu huo hivyo
kutoka kipindi cha kwanza bila kufungana.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo mabeki wa Kagera
Sugar walikuwa na wakati mgumu wa kuzui kasi hiyo, ingawa hakuna kilichofanyika
mpaka ilipofikia dakika ya 58 kulipotokea tafrani kwenye lango la wagosi na
kuzalisha penati iliyoonekana kuwa na utata.
Baada ya hapo wachezaji wa Coastal Union walizidishiwa nguvu
na Mganda Yayo Kato, Masumbuko Keneth na Uhuru Suleiman ambapo walibadilishana
na Suleiman Kassim ‘Selembe’, Mohammed Sudi na Abdullah Othman.
Kasi ya Coastal Union ilisumbua ngome ya Kagera Sugar lakini
mchezo wa kujiangusha na kupoteza muda kuliwamaliza nguvu Wagosi.
Hali hiyo ilikwenda mbali zaidi hata wachezaji na mashabiki
kuwakataza watoto wanaookota mipira ‘Ball Boys’ kuacha kuokota mipira na badala
yake wachezaji wa Wagosi waokote wenyewe.
Mpaka mwamuzi kutoka Mara ambaye alichezesha kwa kufuata
sheria zote 17 za mchezo huo anapuliza kipyenga cha mwisho matokeo yalisomeka
1-0, ambapo Kagera sugar walitoka kifua mbele.
Baada ya mchezo huo Coastal Union wamekuwa katika hali mbaya
ambapo kuna hatihati ya kushuka nafasi mbili chini kutoka ya nane mpaka ya 10.
Baada ya mchezo huo, mchezo unaofuata ni dhidi ya Simba
utakaochezwa Mkwakwani jijini Tanga, Mtibwa Sugar utakaochezwa Mkwakwani, halafu
tutacheza na Mgambo JKt uwanja wa Mkwakwani na kumalizia mzunguko wa kwanza wa
ligi dhidi ya Ruvu JKt uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.
COASTAL UNION
20 OKTOBA, 2013
BUKOBA, KAGERA
No comments:
Post a Comment