Friday, October 4, 2013

Coastal Union Vs Azam FC, Tanga haitoshi.

 Coastal Union ina kikundi maalum cha ngoma, ambacho kinaongozana na timu Tanzania nzima. Hapa walikuwa wanaifuata timu mjini Mbeya wiki iliyopita.

 Benchi la Coastal Union chini ya uongozi wa kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Moroco. Kila mchezaji afadhali ya mwenzake. Waliokuwa ndani na walio nje hakuna zaidi ya mwenzake, ndiyo raha ya CUSC. Kutoka kushoto Razak Khalfan, Danny Lyanga, Yayo Kato, Hamadi Juma 'Basmat', Yusuf Chuma 'Crouch', Said Lubawa na Kenneth Masumbuko. Wengine ni Mwalimu wa timu B Joseph Lazaro, Kit Manager Mohammed, kocha msaidizi ally Ahmed 'Kidi' na kocha mkuu Hemed Moroco. Kwa mbaaali anaonekana daktari wa timu Mzeee Mganga 'Bwinyex....'

Baadhi ya wachezaji wa Coastal Union kabla ya kucheza na Mbeya City katika uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, kutoka kushoto ni Golikipa Shaaban Kado, Uhuru Suleiman, Othman Tamim, Mbwana Kibacha, pius Kisambale, Marcus Ndeheli, Juma Said 'Nyosso', Haruna Moshi 'Boban', Crispian Odula na Abdi Banda, mwingine ambaye hakuonekana kwenye picha alikuwa ni Jerry Santo ambaye alikwenda kufanya shughuli za unahodha.

Baada ya kutoka suluhu ya 1-1 mjini Mbeya na timu iliyopanda daraja msimu huu ya Mbeya City, Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ kesho watashuka dimbani katika uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani kukutana na Azam FC ‘Wana lambalamba’ kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kusaka point tatu muhimu.

Wagosi wa Kaya wanaoshikilia nafasi ya nne wakiwa na point 10 sawa na Azam FC wanaoshikilia nafasi ya tatu wakipishana magoli ya kufunga na kufungwa, wamewahakikishia wapenzi wao kuwa wauza Ice Cream wa Bahresa wataondoka Tanga vichwa chini baada ya kichapo watakachokipata ndani ya dakika tisini za mchezo.

Itakumbukwa katika mechi ya Mbeya, wachezaji wa Azam FC pamoja na kocha wao walikuwa katika uwanja wa Sokoine kuangalia aina ya uchezaji wa Wagosi ili katika mechi yao wasipate tabu, lakini kocha msaidizi wa Wagosi amesema hilo halisumbui ‘mahakama’.

“Unajua unaweza kuiona mechi ya Manchester United, lakini ukashindwa kuwafunga. Sishangai kuwa kutuona kwao kunaweza kusitusaidie kitu chochote kwani timu yetu ina mifumo mingi ya uchezaji, mbali ya hayo pia tuna wachezaji wazuri ambao watatusaidia kuwatia adabu Azam,” alisiema Ally Ahmed ‘Kidi’.

Kidi aliongeza kuwa; “Tunajua msimu huu kila timu imejipanga, hasa zile ambazo zimepanda daraja msimu huu na kila timu inataka kumaliza nafasi tatu za juu lakini na sisi tupo vizuri, hatujapoteza mchezo hata mmoja ingawa tuna suluhu nyingi tutahakikisha hizi mechi sita zilizobaki tunarekebisha makosa yetu.”

Aidha, mwalimu Kidi alizungumzia suala la beki kinda aliyetokea timu ndogo ya Wagosi, Abdi Banda ambaye kwa sasa anacheza nafasi ya kiungo alisema; “Banda ni mchezaji mdogo na anayeelewa haraka. Nimegundua anacheza nafasi zote na tuliamua kumchezesha namba sita baada ya Odulla ‘Crispian Odulla’ kupewa kadi nyekundu hivyo tukaamua Santo ‘Jerry Santo’ acheze namba nane na Boban ‘Haruna Moshi’ acheze namba kumi.

“Halafu nafasi ya Banda ikachukuliwa na Othman Tamim ambaye anacheza beki zote za kulia na kushoto ameonyesha uwezo wa hali ya juu. Hii inadhihirisha kuwa timu yetu kwa sasa ina wachezaji wengi wanaocheza nafasi  nyingi.”

Alipotakiwa kuzungumzia mfumo wanaoutumia ambapo inaonekana wanajihami zaidi na mbele kuacha mchezaji mmoja haoni hilo litawapa nafasi ya Azam ya kuwachosha mabeki wa Coastal Union hasa ikizingatiwa wana washambuliaji wasiochoka, Kidi alisema “Kocha wa Azam anatujua vizuri, hatuna sababu ya kuweka hadharani mbinu zetu lakini ujue tu timu yetu ina washambuliaji wazuri wa pembeni wanaojua kupiga krosi, tumewafundisha vizuri na nina hakika wameelewa kikubwa wachezaji wajitume.”

Katika hatua nyingine mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Hilal ‘Aurora’ amewataka mashabiki wautumie vizuri mchezo wa nyumbani kwa kushangilia kwa nguvu. “Si umeona namna wachezaji wetu walivyocheza na Mbeya city tulikuwa na uwezo wa kuwafunga zaidi ya mabao matatu lakini wapenzi wao waliwashangilia kwa nguvu.

“Tuache kuzungumza maneno ya kuwakatisha tamaa wachezaji na walimu, tayari wameshafanya kazi yao na sisi tuhakikishe tunaujaza uwanja kama walivyofanya mashabiki  wa Mbeya City. Tuungane kuishangilia timu yetu nina hakika kila mtu atatukubali,alisema Aurora.”

Katibu wa hamasa na ushangiliaji Abdallah Zuberi ‘Unenge’, ambaye huandamana na timu kila inapokwenda alipozungumza na blogu hii alisema;  “Timu bado haijafungwa hata mechi moja, ingawa imetoka suluhu nyingi zitakazotugharimu huko mbeleni, lakini naaamini bado ipo katika chati inatajwa kwenye vyombo vya habari ni ishara njema kikubwa watu wa Tanga waibebetimu  yao  isianguke.”

Mpaka sasa Coastal Union imecheza mechi sita za ligi kuu ambapo wameshinda mechi mbili na kutoa suluhu mechi nne, hawajapoteza hata mchezo mmoja. Wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo ambapo nafasi ya kwanza inashikiliwa na Simba SC wenye point 14, ya pili ni Kagera Sugar (point 11), wa tatu ni Azam FC (point 10) na Coastal Union (point 10).

Baada ya kucheza na Azam FC siku ya jumamosi  Octoba 5 (kesho), Wagosi wa Kaya watakuwa wamebakisha mechi sita kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ambazo ni dhidi ya Ashanti Utd Octoba 13 siku ya Jumapili katika uwanja wa Chamazi  jijini Dar es Salaam.

Mechi nyingine ni dhidi ya Kagera Sugar (J2 Oct 19, Bukoba), Simba SC (J5 Oct 23, Tanga), Mtibwa Sugar (J1 Oct 26, Tanga), Mgambo JKT (J5 Oct 30, Tanga), mwisho watamalizia mzunguko wa kwanza katika Mkoa wa Pwani wakicheza dhidi ya JKT Ruvu Jumamosi Novemba 2.

Mungu akipenda blogu yako itahakikisha inakuwepo kila mechi ili kukupatia picha na habari kutoka eneo la tukio, na tayari blogu imeshatua mjini Tanga timu imehifadhiwa nje ya mji ili kuogopa hujuma za Azam FC. Wachezaji wote wapo katika hali nzuri mbali ya wachezaji wawili kupewa kadi nyekundu katika mechi dhi ya Mbeya City, yaani beki Marcus Ndeheli na kiungo mshambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’.

COASTAL UNION

4 OCTOBA, 2013

TANGA, TANZANIA

2 comments: