Friday, October 11, 2013

Sahihisho: Mechi kati ya Ashanti na Coastal Union ni Jumamosi Octoba 12.

Sahihisho,

Awali blogu hii iliandika kuwa mechi itakayowakutanisha Ashanti United 'Watoto wa Ilala' na Coastal Union 'Wana Mangush', katika uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, itachezwa Jumapili Octoba 13 mwaka huu, lakini kwa mujibu wa viongozi na nahodha wa Coastal Union mechi itachezwa Jumamosi Octoba 12.

Awali ratiba ya kamati ya Ligi iliyo chini ya shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliandika kuwa mechi hiyo itachezwa Jumapili, lakini baadaye wakakiri kukosewa kwa tarehe hiyo, ambapo usahihi ni kuwa mechi itapigwa siku moja nyuma.

Mwandishi wa Coastal Union, alijaribu kuwasiliana na msemaji wa TFF, Boniface Wambura, lakini simu yake haikupatikana. Ndipo akajaribu tena kuwasiliana na mwenyekiti wa timu, Hemed Hilal 'Aurora' ambapo simu yake ilikuwa 'busy' nadhani ni kutokana na kutumika sana.

Aidha mwandishi akaenda mbali zaidi na kuwasiliana na meneja wa timu ndogo ya Wagosi, Abdulrahman Mwinjuma 'Ubinde' juu ya usahihi wa ratiba na kubainisha mechi itachezwa Jumamosi na si Jumapili kama ilivyoripotiwa awali.

Mwandishi akawasiliana na nahodha wa Wagosi, Mkenya Jerry Santo, ambaye naye alimhakikishia kuwa ni kweli TFF waliwasiliana nao na kukiri ratiba ya awali ilikuwa si sahihi, hivyo mechi itachezwa Jumamosi katika uwanja wa Chamazi saa kumi alasiri.

Katika hatua nyingine blogu hii ilitoa msimamo tofauti juu ya nafasi inayoshikilia Coastal Union, ambapo awali iliandika kuwa Coastal Union ipo nafasi ya nne. Lakini usahihi ni kuwa Coastal Union ipo nafasi ya saba ikiwana  pointi 11, imecheza mechi saba, kushinda mbili na kutoka suluhu mechi tano.

Aidha timu inayoongoza ligi mpaka sasa ni Wekundu wa Msimbazi Simba, wenye point 15 ikifuatiwa na Azam FC point 14, Mbeya City point 14, Ruvu Shooting point 13, Yanga yenye point 12 na JKT Ruvu yenye point 12. Coastal Union point 11.

Timu nyingine ni Kagera Sugar yenye point 11, Mtibwa Sugar 10, Rhino Rangers 7, huku Tanzania Prison ikiwa na point 7, JKT Oljoro 5, Mgambo JKT point 5 na Ashanti United ikishika mkia kwa point 2 ikiwa imecheza michezo saba, ikafungwa michezo mitano, kutoa suluhu miwili na haikushinda hata mmoja.

Vilevile bado Coastal Union ipo kwenye orodha ya timu nne ambazo hazijapoteza hata mchezo mmoja ambazo ni Simba, Azam, Mbeya City na Coastal Union wenyewe.

Blogu hii inaomba radhi kutokana na usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na mkanganyiko wa ratiba. Mara nyingi TFF hubadili ratiba kutokana na sababu mbalimbali kila zinapojitokeza.

Baada ya mechi ya Jumamosi mwandishi atakwenda ofisi za TFF ili kupata ratiba kamili hasa baada ya kutokuwa na uhakika zaidi juu ya mechi nyingine zilizobaki.

COASTAL UNION
OCTOBA 11, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA.

No comments:

Post a Comment