Bakari Jeki wa kwanza kulia alievaa kofia akiwa na mbunge wa Tanga, Omar Nundu enzi za uhai wake.
KWA niaba ya
uongozi wa Coastal Union, tunatangaza msiba wa mchezaji wa zamani wa timu hii
Bakari Jeki, aliefariki usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya rufaa Bombo.
Kwa mujibu
wa taarifa kutoka kwa kaka wa marehemu ndugu Ally Jeki, ndugu yetu aliugua kwa
muda mfupi ambapo alilazwa katika hospitali ya Bombo wiki iliyopita mpaka mauti
yalipomfika siku tatu baada ya kuanza kuugua.
Mwandisi wetu
alizungumza na mchezaji wa zamani wa Coastal Union, ambae alipata bahati
kumuona Bakari Jeki akiitumikia Coastal Union, Razak Yusuf ‘Careca’ ambae
alibainisha kuwa marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika timu.
“Coastal
Union imekosa mtu muhimu katika soka ambae alikuwa msaada mkubwa akitoa mawazo,
vilevile alikuwa hakosi katika mechi na mazoezi ya timu,” Careca.
Aidha beki
namba tano wa zamani Coastal Union, Mzee Salim Amir ambae alicheza na marehemu
katika michuano ya UFUMA, iliyoandaliwa na Chama Cha Soka nchini (FAT), ambao
ulikuwa ni ushauri wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere.
Nyerere alitoa
ushauri huo ili kuisaidia FAT iliyokuwa chini ya Said El Maamry, kuondokana na
madeni. Michuano hiyo ikapewa jina la Operesheni Futa Madeni (OFUMA).
Ilishirikisha
timu nne ambazo ni Simba (Dar es Salaam), Nyota (Mtwara), Coastal Union (Tanga)
na Nyota Afrika (Morogoro), Coastal Union waliibuka mabingwa marehemu Bakari
Jeki akiwa beki mbili na langoni alikuwa mdogo wake Said Jeki ambae pia alikuwa
golikipa wa Taifa Stars.
Baadhi ya
wachezaji waliokuwa katika kikosi kilichotwaa kombe la OFUMA, ambalo lilichezwa
mara moja tu na kutoendelea tena ni Zacharia Kinanda, Mohammed Makunda, Bakari
Rashid, Kuzu Mbwana, Salim Amir, Mohammed Salim, Zaharan Makame, Said Jeki na Mguruko.
“Alikuwa ni
beki mzuri, Coastal Union ilinufaika na uchezaji wake kwani alicheza kwa moyo
wote beki mbili ambayo ilipanda na kushuka bila kuchoka. Mbali na hayo aliishi
vizuri na wenzake hakuwa mtu wa matatizo muda mwingi alipenda utani.
“Alinikuta
mwaka1976 nikitokea Misri na timu ya Taifa, tukashiriki kombe la OFUMA tukiwa pamoja
katika safu ya ulinzi lakini baadae nilistaafu baada ya kuumia, yeye aliendelea
mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1980 ndipo akaachana na soka, lakini hakuacha kuwa
karibu na Coastal Union, muda mwingi alijitokeza kutoa ushauri na kila
alipohitajika hakusita kuitikia mwito, huyo ndie Bakari Jeki ninaemfahamu,”
alisema Salim Amiri.
Marehemu, alianza
kucheza Coastal Union mwaka 1976 akitokea timu ya Magunia Moshi, alipotua
Coastal Union alicheza kwa moyo wake wote mpaka alipostaafu soka, mpaka mauti
yanamfika alikuwa kocha wa timu za mchangani mjini tanga na mshauri mkubwa wa
benchi la ufundi Coastal Union.
Vilevile marehemu
alitoka katika familia yenye vipaji vya soka kwani walikuwa ndugu watatu wa
baba mmoja na mama mmoja ambapo Said Jeki alikuwa golikipa wa Coastal Union na
timu ya Taifa, mwingine ni Hassan Jeki ambae alikuwa akichezea Reli Morogoro, lakini
kwa sasa wote watatu ni marehemu.
Mwili wa
Marehemu utatolewa Hospitali ya Rufaa Bombo mjini Tanga kuelekea nyumbani kwa
kaka yake Ally Jeki maeneo ya Majengo, ifikapo saa tisa alasiri mwili wa
marehemu utasaliwa katika msikiti wa Majengo kabla ya kupelekwa kijijini kwa
Masuguru Wilayani Muheza Mkoani Tanga saa kumi alasiri.
Kaka wa
marehemu hakuweka wazi kuhusu familia ya marehemu hasa uppande wa mke ama
watoto lakini alibainisha kuwa marehemu alizaliwa mwaka 1953 wilayani Muheza,
Tanga.
HAFIDH KIDO-
MSEMAJI
COASTAL
UNION
26 FEB, 2014
Inalilahi waina ilahi rajiuon mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi amin..
ReplyDelete