Wednesday, February 5, 2014

Tanzania Prison 0-0 Coastal Union, Mbeya



Kwa mara ya tatu mfululizo Coastal Union ‘Wagosi wa kaya’, wametoka suluhu katika mechi za mzunguko wa pili Ligi kuu Tanzania bara, baada ya kukutana na Tanzania Prison mjini Mbeya.
Wagosi wametoka suluhu ya bila kufungana katika uwanja wa kumbukumbu ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine mjini humo.
Itakumbukwa mechi ya ufunguzi mzunguko wa pili katika uwanja wa Mkwakwani Januari 25, Coastal Union walilazimishwa suluhu ya 1-1 na JKT Oljoro, baada siku nne baadae Januari 29 walitoka suluhu ya 0-0 na Yanga katika uwanja wa Mkwakwani.
Aidha mechi ya leo ilionekana kukaa vibaya kwa upande wa Wagosi kwani maafande wa magereza walionekana kupania kuondoka na point tatu muhimu katika uwanja wa nyumbani ambao waliugharamia kukukarabati mwezi uliopita.
Ilipofika dakika ya 29 kipindi cha kwanza, mashabiki wachache wa Wagosi, waliohudhuria kwenye mechi hiyo walipatwa na taharuki baada ya golikipa wao namba moja, Shaaban Kado kugaagaa chini baada ya kupata maumivu makali mchezo ukiendelea.
Mwamuzi wa leo alisimamisha mchezo kwa muda ili kutoa nafasi ya kugangwa kwa Kado, huku kocha Yusuf Chipo akitumia muda huo kuwaelekeza wachezaji wake kipi cha kufanya kuondokana na aibu hiyo ya suluhu.
Mpaka dakika 45 za awali zinatimia, ubao wa matokeo uliendelea kusomeka 0-0, hali iliyozidi kumtia hasira kocha Chipo ambae alizungumza maneno makali katika vyumba vya kupumzikia.
Mbali ya ukali huo lakini kipindi cha pili kilianza kwa kusuasua bila kuonyesha uhai wowote, mbaya zaidi timu ilikuwa ikishambuliwa sana hali iliyomfanya Chipo, kufanya mabadiliko kwa kumtoa Hamadi juma na kumuingiza Yusuf Chuma.
Baadae alitoka Jerry Santo na kuingizwa kijana mdogo Kipanga, halafu akatoka Abdi Banda akaingi Mohammed Miraji. Lakini bado hakuna kilichofanyika mpaka dakika tisini zinakamilika mbali ya Tanzania Prison kucheza pungufu baada ya mchezaji wao kuonyeshwa kadi nyekundu maada ya kucheza madhambi.
Kwa matokeo hayo Coastal Union imefikisha point 19 wakiendelea kung’ang’ania nafasi ya saba katika msimamo wa ligi huku wakiwa wamebakisha mechi kumi ambazo ni sawa na point 30 ikiwa watashinda zote.   
Baada ya mechi hiyo ya Mbeya, Wagosi watasafiri mpaka Tabora kumenyana na Rhino Rangers katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi siku ya Jumapili, Februari 9 mwaka huu.
Kikosi cha leo kilichoanza ni: Shaaban Kado, Hamadi Juma, Othman Tamim, Juma Nyoso, Mbwana Kibacha, Jerry Santo, Crispian Odula, Abdi banda, Kenneth Masumbuko, Danny Lyanga na Yayo Kato.
Wachezaji wa akiba walikuwa ni: Said Lubawa, Ayoub Semtawa, Yusuf Chuma, Kipanga, Mohammed Sudi na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
Hizi ndizo mechi kumi zilizobaki kwa CUSC:
9 February (Tabora) Jumapili
Rhino Vs Coastal Union

15 February (Mlandizi) Jumamosi
Ruvu Shooting Vs Coastal Union

22 February (Tanga) Jumamosi
Coastal Union Vs Mbeya City

8 March (Tanga) Jumamosi
Coastal Union Vs Ashanti

12 March (Dar) Jumatano
Simba Vs Coastal Union

15 March (Dar) Jumamosi
Azam Vs Coastal Union

23 March (Morogoro) Jumapili
Mtibwa Vs Coastal Union

30 March (Tanga) Jumapili
Coastal Union Vs Mgambo

9 April (Tanga) Jumatano
Coastal Union Vs Jkt Ruvu

27 April (Tanga) Jumapili
Coastal Union Vs Kagera
COASTAL UNION
5 FEBRUARI, 2014



No comments:

Post a Comment