Wednesday, August 21, 2013

Ally Kidi: Yayo Kato lazima ajifunze kutafuta mipira mwenyewe.

 Ally Mohammed 'Kidi' akiwa uwanja wa Manungu kukabiliana na Mtibwa Sugar msimu uliopita ambapo mechi iliisha kwa suluhu ya 1-1.

Kushoto kocha mkuu wa Coastal Union, Hemed Morocco akiwa na msaidizi wake matata Ally Kidi, mwenyewe anajiita Polisi (Kitaaluma ni polisi kweli).



Kocha msaidizi wa Coastal Union, Ally Mohamed Kidiamesema kikosi chake kipo vizuri kwa ligi kuu ya Vodacom msimu huu baada ya kufanya kazi kubwa ya usajili na kuunganisha timu kuanzia beki mpaka mshambuliaji.
Akizungumza na blog hii kwa njia ya simu kutoka mjini Moshi, Mwalimu Kidi amesema kazi kubwa tuliyoifanya ni kuunganisha mabeki wazoeane na viungo, wajuane na wazoee aina ya pasi wanazotoa na kupokea. Baada ya kuridhishwa na nafasi ya beki na kiungo tukahamia kwa washambuliaji, tulitaka viongo na washambuliaji wa pembeni na kati wajuane na namna ya kupeana mipira.
Kwa mfano huyu Yayo aliyetoka URA mashabiki wanalalamika hajafunga bao hata moja tofauti na alivyokuwa na timu yake ya awali lakini watu hawajajua kuwa alipokuwa huko alikuwa na viungo bora ambao walikuwa wakimlisha mipira yeye anamalizia. Tumefanya kazi kubwa ya kumbadilisha azoee aina ya soka la bongo ambapo mshambuliaji mara nyingine anajitafutia mwenyewe, tunashukuru anatuelewa,alisema.
Aidha alipoulizwa juu ya winga mwenye kasi Danniel Lyanga kutaka kubadilishiwa namba na kuwa mshambuliaji wa kati alisema: Ni kweli Morocco alitaka kufanya hivyo lakini baadaye tukabadili nia baada ya kumuona anateseka bure, pale katikati hupawezi kama huna maamuzi ya haraka Danny ameshazoea kucheza winga, na kwa bahati nzuri tumeona akicheza na Uhuru Suleiman wanaelewana sana maana wote wana kasi.
Aliongeza kuwa timu ipo vizuri wameamua kusogea Moshi ili kuwa karibu na Arusha iwe rahisi kwao kusafiri mechi ikikaribia, wamecheza mechi moja tu ya kirafiki dhidi ya Machava FC (ambayo kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari wameibuka na ushindi wa bao 3-0 wafungaji wakiwa Danny Lyanga, Atupele Green na Yayo Kato) ili kuwapa wachezaji muda wa kutosha wa kupumzika baada ya kucheza mechi tano mfululizo na kusafiri kuelekea Mombasa, ni vema wawe na nguvu mpya ya kuanza mikiki ya ligi kuu.
COASTAL UNION
AGOSTI 22, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment