Monday, June 17, 2013

unamjua mzee Azgar, alikuwa golikipa wa Coastal union. Coastal ikicheza mkwakwani anakwenda kujificha Jet.





Huyu mzee ninaewaletea hapo juu ni mshabiki wa Coastal Union wa miaka hiyo na hadi sasa amekua mzee bado anaipenda Coastal Union kwa moyo wote. Nyumba yake inatazamana na club barabara 11, yeye ndiye alikuwa akiwapa wanachama habari za timu ilipokuwa ikicheza mikoani, kipindi hicho hakukuwa na simu za mikononi na vituo vya radio vilikuwa vichache.

Nakumbuka katika shamrashamra za ubingwa hapo club 1988 huyu mzee alijitolea nyumba yake ikafanywa sherehe, akitegemewa sana kutoa habari kwa njia ya simu timu ikisafiri mikoani simu zilikua za kukoroga.

Anaitwa Azgar, ni Bohora kutokana na mapenzi na timu alikuwa na presha sana timu ikicheza Mkwakwani alikuwa anakwenda baharini Jet mpaka ikifika jioni anasubiri watu wanaorudi kutoka Mkwakwani akisikia 'Mohammed Salim lile goli la 3 kalifunga vizuri sana,' hapo na yeye anarudi haraka kuja kushangilia na wapenzi wenzake alikua na presha sana.

Kwa mujibu wa mchezaji wa zamani wa Coastal Union, Razack Yusuf 'Careca' mzee huyu kipindi cha ujana wake aliwahi kuichezea Coastal Union nafasi ya golikipa.

Imeeandikwa na Ally Kiraka, mwanahistoria wa Coastal Union.
COASTAL UNION
TANGA TANZANIA
17 June, 2013

Mlinzi wa kambi ya timu aliyetokea Singida.

Nikisema wazee wa club basi huyo naweza sema ndo mwenye funguo za club! Huyu mzee hadi leo yupo hapo jirani na club anafanya biashara zake nje ya MINI RESTAURANT.

Huyu mzee alikua ni CLUB TEAM MANAGER miaka ya nyuma, mwenzie wa karibu aliyeshirikiana naye ni marehemu KARABAI MWAKO. Leo nilimtembelea na amefurahi sana, mwenyewe akiiniita we MMAHARA upo?.

Jina lake anaitwa Mzee juma, hata kambi ya karibu na shule ya bombo alikuwepo ni mlinda kambi wa zamani sana alikuja Coastal Union akitokea Singida alikuja kama TX, NI MTU SPESHELI KWA MAMBO YA ULINZI WA KAMBI HATA SASA ANAENDELEA NA ULINZI WA CLUB NA PIA HANA HAJA YA KUJUA LUHA YENU RAZAKI ANAITA RASHAKI.

Imeeandikwa na Ally Kiraka, mwanahistoria wa Coastal Union.
COASTAL UNION
TANGA TANZANIA
17 June, 2013

Sunday, June 16, 2013

Kutana na Binslum, mdau wa soka aliyepania kuinyanyua Coastal Union ya Wagosi wa Kaya

Nassor Ahmed Binslum akiwa ofisini kwake Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
                    Hili ni gazeti la leo la Mtanzania, mwandishi Kambi Mbwana anaandika......

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
ILI timu iweze kufanya vizuri, kunahitaji vitu vingi, kama vile uongozi bora, sambamba uwezo wa kuingiza chochote kitu, maana mpira wa siku hizi ni fedha.

Zipo timu ambazo zinashindwa kutikisa, maana zinakabiriwa na njaa katika mifuko yao, kama vile Villa Squad, Ashanti FC, Toto African na nyinginezo zinazowania nafasi ya kucheza ligi kuu, ukiacha zile zinazomilikwia na
Kampuni au taasisi, kama vile Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, JKT Orjolo, Ruvu JKT, Mgambo Shooting na nyinginezo.

Hali hii kwa sasa haipo tena ndani ya Coastal Union, yenye maskani yake jijini Tanga, maana ina mdau, Nassor Ahmed ‘Bin Slum’, ambaye kwa kupitia moyo wake, mapenzi yake dhidi ya Wagosi wa Kaya hao, mambo yanaonekana mazuri.

Tangu mwaka 2008 alipoongeza mapenzi na msaada kwenye timu hiyo, haijashuka tena daraja, sanjari na kusajili au kutumia kila wanachohitaji, ikiwa ni pamoja na kumudu kuwalipa mishahara wachezaji wote wanaokipiga Coastal Union.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, Bin Slum ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi pamoja na Mdhamini wa Coastal Union, mdau huyo na mnazi mkubwa wa timu hiyo anasema alianza zamani kuisaidia timu hiyo kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo.

Anasema kuwa hapo awali alitaka kukipiga Coastal Union, lakini baada ya kupata ajali yaa kuumia goti uwanjani, ndoto yake ilitoweka rasmi na kubaki kama shabiki mkubwa wa mpira wa miguu, hususan kwenye timu hiyo ya nyumbani kwao.

“Coastal Union ni timu yangu ya nyumbani, nimezaliwa na kusomea Tanga, hivyo nadhani bado nahitaji kufanya kila niwezalo katika kuhakikisha kuwa inasonga mbele.

“Hapo zamani nilikuwa nafanya siri, lakini ukimya huo uliondoka na kuona nijitangaze tu kuwa msaada unatoka ndani ya Kampuni yangu ya Binslum Tyres Company Ltd, ingawa nakiri kuwa siisaidii Coastal nikiangalia faida kwa muda huu, maana ni wazi haiwezi kupatikana,” alisema BinSlum.

Mdau huyo anasema msimu wa 2011 na 2012 waliweza kufanya vizuri na kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi licha ya malengo yao kulilia wasishuke daraja, ila msimu wa 2012/2013 hali imebadilika baada ya kuambulia naafsi ya sita.

Anasema si matokeo mabaya kwa timu yao, maana timu kama Coastal Union ina changamoto nyingi, ikiwamo uwezo wa kifedha, malengo na ushirikiano kwa wachezaji wake.

BinSlum anasema kuwa tayari wameanza kufanya usajili wenye dhamira ya kuifanya Coastal inyakuwe ubingwa msimu ujao, wakimsajili Haruna Moshi Boban na Juma Nyosso wote kutoka Simba.

Wengine waliosajiliwa Coastal Union ni pamoja na Markus Ndehele na Said Lubao wote kutoka JKT Orjolo, wakati Abdallah Athuman Ally huyu anatokea Jamhuri ya mjini Pemba, ambaye pia ni mchezaji bora katika soka la Zanzibar na Kennet Masumbuko aliyesajiliwa kutoka Polisi Morogoro.

Msimamo wa Coastal Union ni kuwa hawana udugu kabisa na timu za Simba na Yanga, kama baadhi yao wanavyofikiri, isipokuwa uswahiba huo utakuwapo katika masuala ya Kitaifa.

Anasema wapo baadhi ya watu wanasema kuwa timu ya Coastal Union ina urafiki na Simba, jambo ambalo halina ukweli wowote, hivyo .
Said Lubao, wua wakati soka u wa Benchi la
 Chanzo: Handeni kwetu blog.

Friday, June 14, 2013

Picha hii ilitolewa wiki chache kwenye ukurasa wa facebook wa Coastal Union

Leo nimewaletea picha ya kambi ya coastal union iliyokua jirani na shule ya msingi bombo!angalieni vizuri hiyo picha mutaniona ally kiraka huyo alovaa kishati cha bahama!nilianza kuipenda coastal toka utoto wangu na nilikua karibu sana na timu, naijua vizuri Coastal, hehehe mimi ndiyo Coastal Union bwana! Hapo nilikua napiga makofi kuwapa hamasa wachezaji na sipendi majungu. Hayo ni maneno ya Ally Kiraka.

Baadaye akaingia Hussein Mwakuluzo katika ukurasa akaandika hivi "Hapo namuona mzee mbunge aliyesimama, na huyu aliyekuwa karibu na Ali ni Ali Haniu, na aliyekuwa kushoto kwa mzee mbunge ni Mohammed Mwameja, na yule anaefunga viatu ni Jangalu!'
Asante kwa kumbukumbu!

Kumbukumbu za Ally Kiraka zinaanza kuingia kwenye blog...


Wadau mnawakumbuka hawa? kutoka kushoto ni Said Salim 'Kolongo,' Ali Mwaliza na Mohammed Kampira 'Kaball'.


Hawa ni wachezaji wa coastal union! watakumbukwa sana hawa wachezaji kwa heshima waloileta 1988!kila mchezaji alikua na heshima yake na jina lake la utani!kuna anaeitwa kaball,kuna anaitwa hapitiki,ila huyo wa kati alikua na cfa ya mtibuaji mipira,alikua akicheza no.4,huyo ndie alimchana nyama KURWA shabaan wa african sports na akala RED CARD!haya nimeanza tena kuleta kumbukumbu!


Kiraka
Tanga Ngamiani.

Bunduki za Coastal Union msimu ujao, hizo ni bunduki nane bado mbili ambazo zitakuwa kutoka nchi za nje..

 Kiungo machachari wa Simba na timu ya Taifa wakati fulani Haruna Moshi 'Boban' akitia saini kuichezea Coastal Union msimu ujao mbele ya kocha mkuu wa Wagosi wa kaya Hemed Morocco.

 Yusuf Chuma kutoka timu B naye akisaini mkataba wa miaka mitatu kuichezea Coastal Union mbele ya makamu mwenyekiti Steven Mnguto.

 Hamad Juma akikokota mpira katika mechi ya mzunguko wa pili dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Ingawa matokeo yalikuwa 2-1 na Simba kutoka kifua mbele lakini kijana huyu wa timu B alifanya vizuri sana mpaka kocha Hemed Morocco akaamua kumsainisha mkataba wa miaka mitatu kuichezea Coastal Union.

 Makamu mwenyekiti wa wagosi wa kaya Steven Mnguto akishikana mkono na golikipa kutoka JKT Oljoro, Said Lubawa.

 Marcus Ndehele kutoka JKT Oljoro akitia saini kuichezea Coastal Union kwa msimu ujao.

 Juma Said 'Nyosso' kutoka Simba akiwa na makamu mwenyekiti wa Coastal Union Steven Mnguto mara baada ya kumwaga wino kuichezea timu yetu kwa msimu ujao.

 Abdullah Othman Ally kutoka Jamhuri ya Pemba akiwa na kocha mkuu wa Coastal Union Hemed Morocco, punde baada ya kusaini kuichezea Coastal kwa msimu ujao.

Keneth Masumbuko kutoka Polisi Morogoro akishikana mkono na Makamu Mwenyekiti wa Coastal Union Steven Mnguto mara baada ya kuahidi kufanya vema msimu ujao akiwa kikosini.



"Utakumbuka msimu uliopita timu yetu imevutia mashabiki wengi wa soka kutokana na aina ya uchezaji tuliouonyesha, tulikuwa na malengo makubwa lakini hayakutimia mwalimu (Hemed Morocco) ameliona hilo na ndiyo maana wachezaji tuliowasajili yeye ndiye aliyewapendekeza hivyo msimu ujao ni burudani tupu hizi timu zinazopenda kujisifia tunaziomba zijiandae kwa mvua ya mabao," alisema Aurora.

Aidha kwa mujibu wa Aurora katika wachezaji wanane ambao wanategemewa kuingarisha Coastal Union, watatu ni vijana wa timu ndogo ya Wagosi ambao waliwika wakati wa kombe la Uhai chini ya miaka 20 mwaka jana, wachezaji wawili wanatoka Simba wakati wawili wengine wanatoka JKT Oljoro, mmoja anatoka Zanzibar katika timu ya Jamhuri ya Pemba ambaye katika msimu ulioisha alikuwa mchezaji bora wa michuano na mmoja anatoka Polisi Morogoro.

"Tumefanikiwa kunasa wachezaji wawili kutoka Simba, Haruna Moshi 'Boban', Juma Said 'Nyosso', JKT Oljoro tumenasa wawili ambao ni beki Marcus Ndehele na golikipa Said Lubawa, kuna mchezaji wa Jamhuri ya Pemba ni kiungo anaitwa Abdullah Othman Ali, wakati Polisi Morogoro tumemnasa Kenneth Masumbuko huyu ni mshambuliaji, katika timu B tumewapandisha Hamad Juma na Yusuf Chuma kuna mtoto mmoja wa timu B bado hatujamalizana naye lakini pia tutampandisha," alisema.

Naye msemaji wa timu hiyo Eddo Kumwembe, amewataka mashabiki wa Coastal Union kuwa na umoja wakati wa kipindi hiki cha usajili kwani kutazungumzwa mengi ambayo yanalenga kuleta siasa za soka, kwani hakuna timu ambayo inapenda kuona inapoteza mchezaji mzuri lazima watatengeneza fitina ili aonekane mkorofi ama hafai.

"Katika huu usajili nitazungumzia kuhusu wachezaji wawili Juma Nyosso na Boban 'Haruna Moshi', Boban ni kiungo wa uhakika tumemchukua ili kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji, tayari tumeshazungumza naye tunaamini ni mtu mzima hatuangalii maisha yake ya nje ya uwanja bali tunahitaji msaada wake ndani ya dimba wakati wa dakika tisini za mchezo.

"Yatazungumzwa mengi lakini tunaamini Boban ametuelewa na ametuahidi kucheza soka la uhakika, na kuhusu Nyoso, heheheeeeee (anacheka) ninashangaa sana watu wanaotubeza kwa kumsajili Nyoso kuna timu inamtaka ipo Afrika Kusini, kama hiyo haitoshi Libolo ya Angola nayo inamuhitaji tunataka nini tena," aihoji Eddo.

Coastal Union ambayo ilirudi katika ramani ya soka katika msimu wa 2011/12 ambapo ilimaliza nafasi ya tano katika msimu ulimalizika wa 2012/13 imeshika nafasi ya sita lakini imeleta ushindani kwa timu ambazo zimekuwepo katika ligi kwa muda mrefu, hivyo wanaamini msimu ujao utakuwa mzuri kwa usajili uliofanyika chini ya kocha mkuu wa timu hiyo Hemed Morocco na msaidizi wake Ally Mohammed 'Kidi' pamoja na kocha wa walinda mlango Juma Pondamali 'Mensah'.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
Tanga Tanzania
14 June, 2013

blogu imerejea mitamboni, poleni wadau mliokuwa mkiikosa.

Kunradh mashabiki wetu,

Kwa kipindi kirefu blogu yetu imekuwa kimya, ni kutokana na matatizo ya kiufundi. Lakini tunashukuru kwa sasa hali imetengemaa na tutaendelea kuwaletea taarifa za kila siku kuhusiana na klabu yetu tunayoipenda.

Hasa ukizingatia hiki ni kipindi cha usajili na maandalizi ya msimu ujao wa 2013/14 hivyo tutaendelea kuwaletea mambo mazuri kuhusiana na shughuli za kila siku zinazohusiana na klabu.

Kadhalika tunategemea kuwa na mkutano mkuu wa wanachama, yatajadiliwa mengi kadhalika picha nyingi tutaziweka humu kwa kumbukumbu kwa wale waliohudhuria mkutano huo. Punde baada ya kupata taarifa kamili kutoka kwa viongozi juu ya ajenda na mambo mengine yanayohusiana na mkutano tutawaarifu.

Vilevile ukurasa wetu wa facebook umeanzisha utaratibu wa kuwakumbuka wachezaji wa zamani wa Coastal Union, pamoja na vibweka vya mashabiki wakiwa uwanjani. Tutakuwa pamoja na mwanahistoria wetu Ally, almaaruf Ally Mmahara au Kiraka. Yeye atakuwa na nafasi maalum katika blogu hii kutuletea historia pamoja na picha.

Wenu katika ujenzi wa chama kubwa, Coastal Union 'Wagosi wa kaya'.

COASTAL UNION
TANGA, TANZANIA
14 June, 2013