Thursday, January 30, 2014

Mechi 11 za Coastal Union zilizobaki.



Ukiacha mechi ya Prison ambayo awali ilipangwa kuchezwa Februari 2, lakini mpaka sasa haijajulikana itachezwa tarehe hiyo ama la katika uwanja wa Sokoine mjini Mbeya; mechi nyingine za Coastal Union mzunguko wa pili Ligi Kuu ni kama ifuatavyo.
Februari 2, Rhino Rangers uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Februari 15, Ruvu Shootings uwanja wa Mabatini mkoa wa Pwani.
Februari 22, Mbeya City, uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Machi 8, Ashanti UTD, uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Machi 12, Simba SC, uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Machi 15, Azam FC, uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.
Machi 23, Mtibwa Sugar, uwanja wa Manungu, Turiani Morogoro.
Machi 30, Mgambo JKT, uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Aprili 12, JKT Ruvu, uwanja wa Mkwakwani Tanga
Aprili 27, Kagera Sugar, uwanja wa Mkwakwani Tanga.
COASTAL UNION
JANUARI 30, 2014
TANGA, TANZANIA

Wednesday, January 29, 2014

Coastal Union 0-0 Yanga



 Kocha wa Yanga (kulia) Van De Plunm akiwa na Meneja wa Yanga Hafidh Saleh kabla ya mchezo leo.


 Kocha wa Coasal Union Yusuf Chipo akihojiwa na wanahabari kabla ya mchezo.


 Abdi Banda akitafuta mbinu za kumtoka mchezaji wa Yanga, Oscar Joshua katika mchezo wa leo uwanja wa Mkwakwani.


Haruna Moshi 'Boban' akimuonyesha kocha Chipo kuwa mambo anayaweza.



                               Kenneth Masumbuko akitolewa uwanjani baada ya kuumia kipindi cha pili.

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Yusuf Chipo ameanza kuridhishwa na kiwango cha wachezaji wake mbali ya kutoa suluhu ya pili katika mechi za ligi kuu Tanzania Bara.
Mechi ya leo kati ya Coastal Union na mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga, iliyopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani imeisha kwa sukuhu tasa ya bila kufungana lakini walimu wote wawili wameonyesha kuvutiwa na soka lililochezwa leo.
Yanga walianza kwa kasi huku wakilisakama lango la Wagosi wa Kaya mfululizo na kupata kona Zaidi ya nne ndani ya dakika tano za awali kipindi cha kwanza. Hali ilizidi kuwa mbaya kwa upande wa Coastal Union ambapo Yanga walionekana kuwa makini na kushambulia kwa kasi.
Dakika ya 36, Crispian Odula wa Coastal Union alikosa bao la wazi akiwa yeye na golika wa Yanga Deogratius Munishi (Dida).
Mpaka kipindi cha kwanza kinaisha hakuna mtu alieona lango la mwenzake hali iliyowapa mwanya makocha kuwapa nasaha ili wasirudie makosa waliyofanya awali.
Hata hivyo maamuzi ya leo kwa refa wa kati yalionyesha kuwakera mashabiki wa pande zote mbili halo iliyoleta taharuki na mchezo kusimamishwa Zaidi ya mara mbili ili kuweka mambo sawa.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kushambulia kwa kasi ili kupata bao moja ili kuwaharibu kisaikolojia wachezaji wa Coastal Union, hata hivyo mlinda mlango wa Wagosi, Shaaban Kado alikuwa makini langoni kuhakikisha hatari zote zinaishia nje ya eneo lake la kujidai.
Dakika tisa za awali katika kipindi cha pili Nadir Haroub ‘Canavaro’ alitaka kujifunga katika harakati kuokoa shuti la Abdi Banda. Baada ya hapo mashabiki wa Yanga wakaanza kumrushia chupa Canavaro.
Katika kipindi cha pili Yanga walianza kupoteza pumzi na kuchezewa mpira mwingi na Coastal Union, walioamka kutoka usingizini.
Hata hivyo ilipofika dakika ya 68 mwamuzi alitoa nafasi kwa Yanga kupiga mpira wa adhabu ndogo baada ya mchezaji wao kuchezewa vibaya nje kidogo ya 18. Lakini faulo ile ilionekana kuwakera wachezaji wa Coastal Union, ndipo mwamuzi akampa kadi ya njano Haruna Moshi ‘Boban’.
Baadae dakika ya 77 winga wa Coastal Union, Kenneth Masumbuko aliumia misuli ya mguu akaingia Mohammed Sudi, ilipofika dakika ya 86 alitoka Yayo Kato akaingia Mohammed Miraji (86).
Mpaka dakika 90 zinakamilika matokeo yaliendelea kusomeka hivyo hivyo 0-0. Hali hiyo ilionekana kuwakera mashabiki wa timu zote kwani Yanga bado wana kampeni ya kushikilia kileleni, huku Coastal Union wakitaka kujisafisha baada ya kutoa suluhu ya 1-1 na JKT Oljoro katika uwanja huu huu wa Mkwakwani Jumamosi iliyopita.
COASTAL UNION
29 JANUARI, 2013
TANGA, TANZANIA

Monday, January 27, 2014

TIKETI ZA COASTAL NA YANGA ZIPO SOKONI

 Mashabiki wa Coastal Union wakiingia uwanjani kwenye mechi ya jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani, Coastal Union Vs JKT Oljoro. Matokeo yalikuwa ni 1-1.

 Vijana wa Coastal UNion wakipasha kabla ya mechi dhidi ya JKT Oljoro Jumamosi iliyopita.

 Kigoma cha Wagosi wa Kaya kikishughulika katika mechi ya Jumamosi iliyopita dhidi ya JKT Oljoro.

Angalia uwanja ulivyokuwa mtupu mechi ya Juammosi, haya ni matokeo ya tiketi za Elektroniki.





Mauzo ya tiketi za elektroniki kwa mechi tatu kati ya nne za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitakazochezwa keshokutwa (Januari 29 mwaka huu) tayari yameanza, hivyo wanatakiwa kununua mapema.
Mechi hizo ni kati ya Coastal Union na Yanga itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar itakayochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na ile ya Azam dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Kwa washabiki wa Dar es Salaam watakaokwenda Tanga kushuhudia mechi kati ya Coastal Union na Yanga wanashauriwa kuanza safari wakiwa na tiketi zao mikononi, hasa kwa wale watakaonunua kupitia maduka ya Fahari Huduma.
Tiketi pia zinaweza kununuliwa kupitia mtandao wa M-Pesa kwa kupiga namba *150*03*02#. Kwa wanaotumia CRDB simbanking wanaingia kawaida kwa *150*03.
Vilevile tunawakumbusha washabiki kuwa kwa viwanja ambavyo tayari vina mfumo wa tiketi za elektroniki hakuna tiketi zitakazouzwa uwanjani, hivyo wanaokwenda kwenye mechi wanatakiwa kuwa na tiketi zao mikononi.
COASTAL UNION
27 JANUARI, 2014
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Saturday, January 25, 2014

Coastal Union 1-1 JKT Oljoro

                      Kikosi cha leo kilichomenyana na JKT Oljoro uwanja wa Mkwakwani leo.

                   Viongozi wa Coastal Union wakifuatilia mechi ya leo uwanja wa Mkwakwani.

 Meneja wa Coastal Union akitaniana na Kocha wa JKT Oljoro Hemed Morocco kabla ya mchezo leo.

                     Atupele Green akimtoka mchezaji wa JKT Oljoro uwanja wa Mkwakwani leo.

 Kenneth Masumbuko, akitafuta mbinu za kumtoka Nurdin Mohammed wa JKT Oljoro katika uwanja wa Mkwakwani leo.

                                                             Yayo Kato Lutimba

 Yusuf Chipo, Kocha wa Coastal Union akiangalia mchezaji wake Danny Lyanga akifanya vitu vyake katika mechi ya leo uwanja wa Mkwakwani.

 Yayo Kato akijishauri cha kufanya kabla ya kuanza kukimbizana na Ally Hamza wa JKT Oljoro.

 Mfungaji wa bao la Coastal Union Yayo Kato, akigombania mpira na mchezaji wa JKT Oljoro Ally Hamza.

 Kocha Mkuu wa Coastal union, Yusuf Chipo akiwatuliza wachezaji wake baada ya kufungwa bao la kusawazisha leo.

                                             Coastal Union ina mashabiki wa mataifa mengi.

 Danny Lyanga akituliza mpira kwenye gamba katika mechi ya leo alicheza vizuri ingawa kuanguka anguka kulikuwa kwingi.

                                                                Danny Lyanga.



Wachezaji wa JKT Oljoro wakishangilia baada ya kusawazisha na kulazimisha matokeo kusomeka 1-1 leo.
 

MBALI ya kukaa Oman kwa wiki mbili lakini kikosi cha Coastal Union kimeshindwa kuwapa raha wapenzi wake katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga baada ya kulazimishwa suluhu na wanajeshi wa JKT Oljoro kutoka Arusha.
Suluhu ya 1-1 imeonekana kuwavunja nguvu viongozi na mashabiki wa Coastal Union, ambao waliingia uwanjani kwa idadi ndogo kutokana na tatizo la ukataji tiketi kuwakwaza baadhi ya mashabiki waliotaka kuiangalia timu yao iliyotoka Oman wiki hii.
Coastal Union walianza mchezo wa leo kwa kujiamini wakitoa pasi za uhakika huku wakifika katika lango la wapinzani wao mara kwa mara.
Ilipotimu dajkika ya 7, Yayo Kato aliandika bao la kwanza baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Kenneth Masumbuko baada ya Hamad Juma kufanya kazi nzuri ya kumdhibiti beki wa Oljoro na kupiga krosi.
Bao hilo lilidumu kwa dakika 45 za awali ambapo mpaka timu zinakwenda mapumziko ubao uliendelea kusomeka 1-0. Hali iliyoongeza furaha katika uwanja wa Mkwakwani huku kila mmoja akiamini kuna mabao mengi mengine yanakuja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku wachezaji wa Oljoro wakicheza kw akujihami na kupiga pasi fupi zilizoonyesha kuwachanganya wachezaji wa Coastal Union. Hali hiyo vilevile ilimnyima raha kocha wa Coastal Union, Yusuf Chipo ambae alionekana kusimama wakati wote.
Kufikia dakika ya 75 Coastal Union, tayari walishafanya mabadiliko ya wachezaji watatu ambapo alitoka Kenneth Masumuko na kuingia Abdi Banda, baadae alitoka Othamn Tamim akaingia Crispian Odula mwisho alitoka Yayo Kato na kuingia Mohammed Miraji.
Wagosi wa Kaya waliendelea kumiliki mpira, walifanya juhudi kubwa ambapo muda mwingi Danny Lyanga alikuwa msumbufu katika winga ya kushoto hali iliyomnyima raha golikipa wa Oljoro, Mohammed Yusuf.
Ilipotimu dakika ya 87 dakika chache kabla ya mwamuzi wa leo Israel Nkongo kumaliza kipute, Hamis Saleh wa JKT Oljoro alitumia vema makosa ya mabeki wa Coastal Union na kupachika bao lililoamcha benchi la timu yake kwa furaha.
Baada ya hapo Coastal Union hawakuonekana kukata tamaa waliendelea kuzitendea haki nyasi za uwanja wa Mkwakwani kwa kusakata kabumbu la hali ya juu. Dakika ya 89 Crispian Odula alipata pasi akiwa ndani ya 18 lakini akapiga shuti hafifu lililotua ndani ya mikono ya golikipa wa Oljoro.
Mpaka mchezo unakamilika, ubao ulisomeka 1-1 hali iliyowatoa kichwa chini wachezaji na mashabiki wa Wagosi wa Kaya waliokuwa na matumaini makubwa ya kushinda.
Kikosi cha leo Coastal Union kilikuwa hivi: Said Lubawa, Hamad Juma, Othman Tamim, Juma Nyoso, Mbwana Kibacha, Jerry Santo, Atupele Green, Razakh Khalfan, Yayo Kato, Danny Lyanga na Kenneth Masumbuko.
Wachezaji wa hakiba walikuwa ni: Mansoor Alawi, Abdi Banda, Yusuf Chuma, Mohammed Miraji, Suleiman Kassim, Crispian Odula na Ayoub Semtawa.
COASTAL UNION
25 JANUARI, 2014
TANGA, TANZANIA