Sunday, July 28, 2013

Coastal Union wazee wa dozi wamchinja mnyama Mkwakwani.

Coastal Union wakinyoosha viungo kabla huku kocha msaidizi ally Kidi akiwaangalia.
Vikosi vyote viwili kabla ya mchezo kuanza.

Hapa vijana wakishangilia bao pekee la leo lililotumbukizwa na Crispian Odula Odwenye.

Wagosi wa kaya wameendelea kutuma salamu kwa timu zinazoshiriki ligi kuu Tanzania bara kwa kuwachapa 1-0 Simba SC kwenye mechi ya kirafiki kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom.
Mfungaji wa bao hilo ni mshambuliaji Mkenya, Crispian Odula aliyesajiliwa kutoka Bandari ya Mombasa.
Mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wengi uwanja wa Mkwakwani, ilikuwa gumzo kwenye viunga vya mji wa Tanga na Dar es Salaam ambapo Simba waliingia jijini hapo wakijitapa kulipiza kisasi cha msimu uliopita baada ya kubaniwa kupata point za bure na kutoka suluhu.
Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa kujihami huku kukiwa na mashambulizi ya kushtukiza ambapo mpaka dakika 45 za mwanzo hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili Coastal Union waliingia kwa kasi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kitu kilichompa wakati mgumu golikipa wa Simba, Mganda Abel Dhaira.
Kufikia dakika ya 54 Crispian Odula anayeheshimika sana ndani ya jiji hilo alipokea pasi safi kutoka kwa Keneth Masumbuko, akauacha udunde ndani ya eneo la hatari, akaja mchezaji wa Simba akampiga tobo akainua macho kumuangalia Mganda Dhaira akamekaa uelekeo gani, alipoona amekaa katikati ya lango akapiga kwenye nyavu ndogo na kuwatia wazimu mashabiki wa Coastal Union waliojaa ndani ya uwanjani utadhani hakuna Ramadhani.
Kitu kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu ni kuona kama mchezaji chipukizi aliyetoka Coastal Union, Ibrahim Twaha ‘Messi’ atacheza ama la, lakini kufika dakika ya 70 aliingizwa kuongeza mashambulizi baada ya Simba kuelemewa. lakini kocha Morocco alifanya ujanja kwa kumuingiza kijana mwenzie waliocheza pamoja timu B, Hamad Juma ‘Basmat’.
Kazi ya ‘Messi’ ikawa imeishia hapo kwani Hamad alipewa kazi moja tu ya kuhakikisha ‘Messi’ akifika winga ya kushoto ilipo ngome yake hapigi krosi. 
Mbwana Kibacha na Juma Nyosso wakaambiwa wahakikishe kijana huyo mwenye mbio nyingi havuki ukuta wa Coastal Union. Mwisho akaonekana hana msaada wowote kwa timu namna alivyodhibitiwa.
Kikosi cha Coastal Union: Shaaban Kado, Mbwana Kibacha, Othman Bakari, Juma Said ‘Nyosso’, Marcus Ndehele, Jerry Santo, Uhuru Suleiman, Crispian Odula, Keneth Masumbuko, Haruna Moshi ‘Boban’, na Daniel Lyanga.
Baadaye kocha mkuu wa coastal Union akishirikiana na Ally Kidi walifanya mabadiliko kwenye kipindi  cha pili kwa kuwatoa Uhuru Suleiman, Daniel Lyanga, Crispian Odula na Othman Bakar . Wakaingia Abdi Banda, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Mohammed Sudi na Hamad Juma ‘Basmat’.
COASTAL UNION
28 JULAI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA


Mechi ya kirafiki Coastal Union na Simba SC imekuwa gumzo Tanga.

 Shabiki mkubwa wa coastal Union (katikati) Eddy akiwa na maswahiba wake wakijadili mechi ya Coastal na URA wiki iliyopita.

 Hivi ndivyo vidume, Ally Kidi kocha msaidizi (aliyevaa kofia) na Hemed morocco kocha mkuu anayesalimiana na vijana. Hawa ndiwo watakaorudisha furaha ya soka jijini Tanga, taraa.

Mfungaji bora ligi kuu Zanizbar Abdallah Othman akishuka kwenye basi la timu.
 Viongozi wa Coastal Union wakijadiliana mawili matatu kuhusiana na mustakabali wa timu msimu ujao.

 Wachezaji wa Coastal Union wakiwa katika uzi mpya kabla ya mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya URA.

Kwa utaratibu mpya aliouanzisha mwalimu Morocco bunduki hizi huanzia benchi, ila zikiingia timu inakuwa mpyaaa. Kutoka kushoto Selembe, Banda na Kibacha.
                                       Hiyo Coastal Union ukiiona jinsi inavyoshangilia balaaa.



MECHI kati ya Coastal Union na Simba SC imeonekana kuvuta hisia za wapenda soka wengi si tu Tanga na Dar es Salaam bali Tanzania nzima kutokana na timu hizo kuwa hasimu kwa kipindi hiki baada ya kuchukuliana wachezaji.
Timu hizo ambazo zinajifua na kujipima nguvu ili kuhakikisha wanashiriki ligi kuu msimu unaoanza mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, wakiwa vema kutimiza azma ya kutwaa ufalme wa soka Tanzania bara, watashuka dimbani leo saa kumi alasiri uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa mechi kubwa ya kirafiki.
Itakumbukwa ziara ya kanda ya ziwa kwa Simba haikutoa matokeo mazuri kutokana na kupoteza baadhi ya michezo huku mingine wakitoa suluhu, imewasili jijini Tanga jana jioni wakitokea Kigamboni kwenye ufukwe wa Bamba Beach walipojichimbia ili kujifua.
Coastal Union walioweka kambi Raskazone Hotel jijini Tanga, wao walianza vema mechi za kujipima nguvu kujiandaa na msimu ujao kwa kuwachapa wababe wa Simba, Uganda Revenue Authority kwa bao 1-0 wiki iliyopita kwenye uwanja wa nyumbani Mkwakwani.
Vyombo vingi vya habari vinaandika kuwa Simba wanawafuata wachezaji wao kiungo matata Haruna Moshi ‘Boban’ na beki hatari Juma Said ‘Nyosso’ lakini mashabiki wa Coastal Union wanasema hayo ni maneno ya mkosaji kwani wachezaji hao walionyesha dalili za kutupiwa virago na timu hiyo ndipo Wagosi walipoona umuhimu wao na kuwachukua.
Mbali ya hayo chipukizi aliyetokea Coastal Union, Ibrahim Twaha Shekuhe ambaye alisajiliwa na Simba mwishoni mwa msimu uliopita atacheza dhidi ya timu yake ya zamani kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na Simba.
Blog hii ilifanya mazungumzo na Ibrahim kujua anajisikiaje kupeleka mashambulizi katika timu yake ya nyumbani alisema, “Kwa kweli ndugu yangu Coastal Union ndiwo wanaonijua zaidi kuliko timu yoyote, haya ni maisha tu na kutafuta lakini kwasababu nimesajili Simba nitaichezea kwa moyo wote na leo nitacheza kama mshambuliaji wa Simba.”
Katika hatua nyingine kocha mkuu wa Simba, Abdallah Kibaden ana kazi kubwa ya kupanga timu yake kutokana na mkanganyiko uliopo kwenye timu hiyo juu ya wachezaji chipukizi na wachezaji wa zamani ambapo kombinesheni ya wachezaji hao imeonekana kushindwa hasa baada ya kuonekana chipukizi wanapocheza peke yao wanaonyesha uwezo mkubwa tofauti wanapochanganywa na wakongwe.
Mbali ya hayo Kibaden ana kazi ya kuwajaribu beki mpya Vincent Matsobane kutoka Black Leopards ya Afrika kusini, mwingine ni kiungo mkabaji wa zamani Azam FC, Abdulhalim Humoud ambaye ameibukia Simba akisaka nafasi ya kusajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Humoud aliyemaliza mkataba wake na Azam FC Mei, mwaka huu na kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa na klabu ya Jomo Cosmos, alionekana katika kambi ya Simba iliyokuwa, Kigamboni, Dar es Salaam.
Naye kocha wa Coastal Union, Hemed Morocco bado anasisitiza utaratibu wake mpya wa kuangalia mshambuliaji atakayemsaidia kufumania nyavu katika msimu mpya ili aweze kutimiza ndoto za watu wa Tanga kushangilia ufalme wa soka kwa mara nyingine tangu miaka 25 iliyopita.
Morocco ameahidi kuwaanzisha wachezaji wote wapya kama alivyofanya kwenye mechi dhidi ya URA ambapo mfumo huo ulimsaidia kuwapumzisha wachezaji wake tegemeo Abdi Banda, Suleiman ‘Selembe’ na mbwana Kibacha ambao kwa kiasi kikubwa walibadili mchezo wa siku hiyo mpaka likapatikana bao pekee lililokata ngebe za waganda waliozitambia timu kongwe nyingine.
COASTAL UNION
28 JULAI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA





Thursday, July 25, 2013

Tathmini mechi ya jana Coastal Union Vs URA.

 Wakati wa kusalimiana mtu anazungumza lugha yoyote hasa tabasamu linazungumza lugha nyingi sana.

 Haruna Moshi 'Boban' siku ya jana alizungumza kwa kujiamini sana hata kuwakosha mashabiki baada ya mchezo kuna kundi la watoto walimfuata wanataka kumgusa. Kwanza alitaka kukataa lakini akatokea Hussein Chuse akamwambia Boban watoto wanataka kukugusa, ndipo akakubali wacha wamparamie.

 Hemed Morocco ni kwacha ndugu yangu maneno hayo yashikeni, anajua kumbadili mchezaji akacheza namba ambayo hajawahi kuicheza. Sasa yupo kwenye program ya kumchezesha Danny awe mshambuliaji wa kati.

                                             Huyo aliyeruka juu ni Captain Jerry Santo taraa...

                               Mchezaji anapokuwa professional huwachwa afanye anachoamini.

Zipo dalili hawa viumbe wakawa super sub. Ni mawazo tu, kutokana na mfumo mpya wa mwalimu Morocco. 

                          Ukisikia chenga ya mwili ndiyohii, halafu utasikia unaambiwa 'itie kiduni'

 Hapo Morocco anamwambia Abdi Banda kaa na mpira kaa na mpiraaa... Wataalamu wameshaelewa.

 Hizi ni furaha za bao dakika ya 72 ukiwaangalia hao URA wamepagawaaaaa, wanashika viuno atiii.

 Kocha wa URA (mwenye kofia) akifanya mahojiano na wanahabari kutoka Tanga mara baada ya timu yake kulala 1-0 Mkwakwani.

 Huyo aliyelala chini ni Juma Nyosso aliumia vibaya sana kwenye bega baada ya mchezaji wa URA kumtegea mgongo na kumshika mkono wakati Nyosso akiwa juu. Nafasi yake ikachukuliwa na Pius Kisambale.

Hapo golikipa wa URA anawaambia mabeki wake, jamani mzuieni huyo anaitwa Odula mchezaji wa bei ghali amevuka maji kutoka Mombasa msimuacheeeee....


Zile salamu alizozizungumzia mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Hilal ‘Aurora’ kwa timu zinazoshiriki ligi kuu zimetumwa rasmi jana kutoka uwanja wa Mkwakwani baada ya Wagosi wa Kaya kuwatuliza 1-0 wababe wa Simba na Yanga, Uganda Revenue Authority waliokuja Tanzania kujipima nguvu.
Pasi ya bao ilitoka mguuni mwa beki wa kushoto Coastal Union, Abdi Banda katika dakika 72 ya mchezo wakati wa kipindi cha pili walipokuwa wanashambulia kutoka lango maarufu la African Sports, Banda alipofika usawa wa benchi la Coastal Union alilazimisha kiki kali iliyotua katikati ya msitu wa wachezaji wa URA lakini mbali ya wachezaji wa URA kulikuwepo na Mbwa mwitu (Keneth Masumbuko) aliyevaa ngozi ya kondoo akaunasa mpira ule kwa mguu wa kushoto halafu bila kumtazama mtu alikunjuka shuti kwa guu la kulia lililompunyua mikononi golikipa mahiri wa URA, Bwite Brian aliyezidiwa ujanja na polisi huyo.
Ilikuwa ni sawa na kesi ya nyani kumpa ngedere maana URA ni kikosi maalum cha kukusanya na kudhibiti mapato nchini Uganda kama ambavyo TRA inafanya kazi Tanzania. Hivyo Masumbuko yeye ametokea kwenye timu ya Polisi Morogoro yenye kazi ya kulinda usalama wa raia hivyo ule upolisipolisi bado anao akahakikisha URA wanaondoka nchini bila kuathiri usalama wa raia kwa kufungwa nchini mwao.
Mchezo ulianza saa kumi na nusu alasiri baada ya mwamuzi wa siku hiyo Kidiwa kupuliza kipyenga na wachezaji wa URA wakaanza kwa mashambulizi ya kushtukiza yaliyowatia baridi mashabiki wa Coastal Union hasa ikizingatiwa dakika chache siku hiyo kulinyesha mvua kubwa.
Mpaka kufikia dakika ya 20 bado mchezo ulikuwa ni wa kuvuziana kwani timu zote mbili zilikuwa zikisoma mbinu ya mwenzie ili kuhakikisha hawatoki kwa aibu kwenye uwanja huo wa Mkwakwani unaochukua mashabiki 10,000.
Coastal Union walikuwa wakishambulia kutoka upande wa kushoto ambapo combination ya Uhuru Suleiman aliyekuwa akicheza namba 7 na Masumbuko Keneth ilimsaidia Danny Lyanga ambaye siku hiyo alikuwa akishambulia kutoka kati tofauti na ilivyozoeleka kocha akimchezesha winga ya kushoto.
Hata hivyo juhudi hizo za kubadili mbinu za ushambuliaji hazikuzaa matunda zaidi ya kuwazidisha ari mashabiki waliofurika kuangalia viwango vya wachezaji wapya waliokuwa wakipamba magazeti kwa kipindi kirefu.
Nusu ya kwanza mchezaji matata nje ya uwanja Haruna Moshi ‘Boban’ ndiye aliyekosha mashabiki wengi kutokana na umahiri wake wa kumiliki mpira huku akipiga chenga za maudhi na kutoa pasi za dhihaka utadhani anacheza na watoto wadogo lakini pasi hizo zilifika miguuni mwa walengwa hali iliyowakosha wana mangushi.
Dakika 45 ziliisha bila kufungana, lakini kulitokea zengwe la sare za mchezo ambapo URA walilalamika kuwa kuna mfanano wa aina fulani katika soxy na jezi za juu. Hivyo kutokana na uenyeji kuchanganyika na ustaarabu ulikokuwepo Tanga Coastal Union waliamua kubadili uzi wao mpya wenye rangi nyeupe tupu na rangi nyekundu mabegani wakaamua kuvaa uzi mwekundu bila kujua rangi nyekundu ingekuwa na bahati kwao siku hiyo.
Dakika 45 za kipindi cha pili zilianza bila timu yoyote kufanya mabadiliko mpaka ilipofika  52 ambapo kocha Hemed Morocco alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu alitoka Hamad Juma, Danny Lyanga na Othman Tamim akaingia Mbwana Kibacha, Suleiman Kassim ‘Selembe’ na Abdi Banda.
Kocha akabadili mchezo ambapo Masumbuko sasa akawa anapiga krosi kutoka kushoto au mara nyingine anamuachia Banda aliyekuwa akisaidiana na Uhuru apige huku yeye anaingi katikati mwenyewe. Taktik hiyo ilizaa matunda dakika ya 72 ya mchezo ambapo krosi ya Banda ndiyo iliyotua mguuni mwa Masumbuko na kupeleka kilio jijini Kampala.
Baada ya hapo Coastal Union wakawa wanalisakama lango la URA bila shaka kupata bao la pili ili kujihakikishia ushindi.
Kufikia dakika ya 85 almanusra URA wasawazishe baada ya Shaaban Kado kujaribiwa shuti la mbali na kumponyoka kwa bahati nzuri liligonga mwamba wa juu na kutoka nje ikawa kona. Ilipopigwa kona mpira ukambabatiza tena na kutaka kuingia lakini akautoa tena ikawa kona pacha.
Vitendo hivi vya dakika mbili viliwanyamazisha mashabiki 8000 wa Coastal Union waliohudhuria na kuwapa nguvu mashabiki wachache wa URA waliokuwa kwenye benchi lao kutokana na kuamini kuwa lolote linaweza kutokea. Kwa bahati nzuri kona ya pili haikuzaa matunda.
Baada ya hapo Wagosi wakaanza kucheza kiujanja ili kupoteza muda baada ya kugundua URA wanaweza kuwachangua udhu kabla ya magharibi kuingia na futari ikawatumbukia nyongo. Hatimaye mwamuzi akamaliza mpira yakatimia yale ya wazee kuwa mfupa uliomshinda fisi mbwa kautafuna.
Kikosi cha Coastal Union kilikuwa: Shaaban Kado, Hamad Juma, Othman Tamim, Marcus Ndehele, Juma Nyosso, Jerry Santo, Uhuru Suleiman, Crispian Odula, Daniel Lyanga, Haruna Moshi ‘Boban’, na Keneth Masumbuko. Akiba ni: Said Lubawa, Mbwana Kibacha, Abdi Banda, Philip Mugenzi, Mohamed Sudi, Pius Kisambale, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Green Atupele na Abdallah Othman.
Baada ya mechi kuisha mwandishi hakupata bahati ya kuzungumza na mwalimu Morocco maana alikuwa anamvizia kocha wa URA, ambapo alipompata na kuzungumza mambo mengi kuhusu timu yake na ziara ya Tanzania shukran katika mazungumzo yake hakugusia kuchoka kwa timu yake ambapo makocha wa kibongo wengi hutumia kama kisingizio.
“Tanzania kuna timu nzuri, hata mimi nimekuja kujaribu wachezaji wangu wapya wapo saba kwa hivyo sikuwa na uchungu sana kupoteza mechi hii lakini timu tatu nilizocheza nazo hapa nchini naziona zote zipo sawa.”
Akaulizwa amecheza na Simba ameshinda 2-1, akacheza na Yanga akatoka suluhu ya 2-2 leo amecheza na Coastal Union wamepoteza kwa bao 1-0 vipi maelezo yake. Akajibu: “The answer is simple, timu iliyonifunga ndiyo best.”
COASTAL UNION
25 JULAI, 2013
TANGA, TANZANIA   



Wednesday, July 24, 2013

Maandalizi ya mechi ya leo yalivyokuwa ndani na nje ya uwanja.









Leo kulitokea kituko uwanjani, Coastal Union walivaa jezi tofauti kila kipindi.

                               Huyu ndiye Odula Crispian kutoka Bandari ya Mombasa Kenya.










 Mbwana Kibacha akitafuta mbinu za kuwatoka Agaba Oscar (kulia) na Kasibante James (kushoto).

Ukisikia kuchonga ndo huku. Hapa mchezaji wa URA Ganya Willy akistaajabu Abdi Banda anavyousanifu mpira.


 Mara nyingine mbinu za kujiangusha zinasaidia kupunguza kasi wachezaji waroho kama kina Masumbuko wasitimize malengo yao.




Umeziona hizo picha tatu za juu, zamani Coastal Union ilikuwa na kamati ya zongo, lakini sasa hakuna kamati hizo tena bali kuna kamati za ushindi na hamasa. Lakini Ramadhan imewakata makali viumbe hawa.

Suala la Coastal Union kuvaa jezi nyeupe kipindi cha kwanza na nyekundu kipindi cha pili ni kutokana na makosa katika pre match meeting ambapo hawakuafikiana kuhusu rangi za sox, ikaonekana sox pamoja na fulana zinafanana kwa mbaali. coastal Union kwakuwa ni wenyeji walilazimika kubadili jezi zao na kuvaa rangi nyekundu kataaika iipindi cha pili kama utakuwa makini utaona kuna jezi nyeupe na nyekundu, usiogope.