Thursday, July 25, 2013

Tathmini mechi ya jana Coastal Union Vs URA.

 Wakati wa kusalimiana mtu anazungumza lugha yoyote hasa tabasamu linazungumza lugha nyingi sana.

 Haruna Moshi 'Boban' siku ya jana alizungumza kwa kujiamini sana hata kuwakosha mashabiki baada ya mchezo kuna kundi la watoto walimfuata wanataka kumgusa. Kwanza alitaka kukataa lakini akatokea Hussein Chuse akamwambia Boban watoto wanataka kukugusa, ndipo akakubali wacha wamparamie.

 Hemed Morocco ni kwacha ndugu yangu maneno hayo yashikeni, anajua kumbadili mchezaji akacheza namba ambayo hajawahi kuicheza. Sasa yupo kwenye program ya kumchezesha Danny awe mshambuliaji wa kati.

                                             Huyo aliyeruka juu ni Captain Jerry Santo taraa...

                               Mchezaji anapokuwa professional huwachwa afanye anachoamini.

Zipo dalili hawa viumbe wakawa super sub. Ni mawazo tu, kutokana na mfumo mpya wa mwalimu Morocco. 

                          Ukisikia chenga ya mwili ndiyohii, halafu utasikia unaambiwa 'itie kiduni'

 Hapo Morocco anamwambia Abdi Banda kaa na mpira kaa na mpiraaa... Wataalamu wameshaelewa.

 Hizi ni furaha za bao dakika ya 72 ukiwaangalia hao URA wamepagawaaaaa, wanashika viuno atiii.

 Kocha wa URA (mwenye kofia) akifanya mahojiano na wanahabari kutoka Tanga mara baada ya timu yake kulala 1-0 Mkwakwani.

 Huyo aliyelala chini ni Juma Nyosso aliumia vibaya sana kwenye bega baada ya mchezaji wa URA kumtegea mgongo na kumshika mkono wakati Nyosso akiwa juu. Nafasi yake ikachukuliwa na Pius Kisambale.

Hapo golikipa wa URA anawaambia mabeki wake, jamani mzuieni huyo anaitwa Odula mchezaji wa bei ghali amevuka maji kutoka Mombasa msimuacheeeee....


Zile salamu alizozizungumzia mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Hilal ‘Aurora’ kwa timu zinazoshiriki ligi kuu zimetumwa rasmi jana kutoka uwanja wa Mkwakwani baada ya Wagosi wa Kaya kuwatuliza 1-0 wababe wa Simba na Yanga, Uganda Revenue Authority waliokuja Tanzania kujipima nguvu.
Pasi ya bao ilitoka mguuni mwa beki wa kushoto Coastal Union, Abdi Banda katika dakika 72 ya mchezo wakati wa kipindi cha pili walipokuwa wanashambulia kutoka lango maarufu la African Sports, Banda alipofika usawa wa benchi la Coastal Union alilazimisha kiki kali iliyotua katikati ya msitu wa wachezaji wa URA lakini mbali ya wachezaji wa URA kulikuwepo na Mbwa mwitu (Keneth Masumbuko) aliyevaa ngozi ya kondoo akaunasa mpira ule kwa mguu wa kushoto halafu bila kumtazama mtu alikunjuka shuti kwa guu la kulia lililompunyua mikononi golikipa mahiri wa URA, Bwite Brian aliyezidiwa ujanja na polisi huyo.
Ilikuwa ni sawa na kesi ya nyani kumpa ngedere maana URA ni kikosi maalum cha kukusanya na kudhibiti mapato nchini Uganda kama ambavyo TRA inafanya kazi Tanzania. Hivyo Masumbuko yeye ametokea kwenye timu ya Polisi Morogoro yenye kazi ya kulinda usalama wa raia hivyo ule upolisipolisi bado anao akahakikisha URA wanaondoka nchini bila kuathiri usalama wa raia kwa kufungwa nchini mwao.
Mchezo ulianza saa kumi na nusu alasiri baada ya mwamuzi wa siku hiyo Kidiwa kupuliza kipyenga na wachezaji wa URA wakaanza kwa mashambulizi ya kushtukiza yaliyowatia baridi mashabiki wa Coastal Union hasa ikizingatiwa dakika chache siku hiyo kulinyesha mvua kubwa.
Mpaka kufikia dakika ya 20 bado mchezo ulikuwa ni wa kuvuziana kwani timu zote mbili zilikuwa zikisoma mbinu ya mwenzie ili kuhakikisha hawatoki kwa aibu kwenye uwanja huo wa Mkwakwani unaochukua mashabiki 10,000.
Coastal Union walikuwa wakishambulia kutoka upande wa kushoto ambapo combination ya Uhuru Suleiman aliyekuwa akicheza namba 7 na Masumbuko Keneth ilimsaidia Danny Lyanga ambaye siku hiyo alikuwa akishambulia kutoka kati tofauti na ilivyozoeleka kocha akimchezesha winga ya kushoto.
Hata hivyo juhudi hizo za kubadili mbinu za ushambuliaji hazikuzaa matunda zaidi ya kuwazidisha ari mashabiki waliofurika kuangalia viwango vya wachezaji wapya waliokuwa wakipamba magazeti kwa kipindi kirefu.
Nusu ya kwanza mchezaji matata nje ya uwanja Haruna Moshi ‘Boban’ ndiye aliyekosha mashabiki wengi kutokana na umahiri wake wa kumiliki mpira huku akipiga chenga za maudhi na kutoa pasi za dhihaka utadhani anacheza na watoto wadogo lakini pasi hizo zilifika miguuni mwa walengwa hali iliyowakosha wana mangushi.
Dakika 45 ziliisha bila kufungana, lakini kulitokea zengwe la sare za mchezo ambapo URA walilalamika kuwa kuna mfanano wa aina fulani katika soxy na jezi za juu. Hivyo kutokana na uenyeji kuchanganyika na ustaarabu ulikokuwepo Tanga Coastal Union waliamua kubadili uzi wao mpya wenye rangi nyeupe tupu na rangi nyekundu mabegani wakaamua kuvaa uzi mwekundu bila kujua rangi nyekundu ingekuwa na bahati kwao siku hiyo.
Dakika 45 za kipindi cha pili zilianza bila timu yoyote kufanya mabadiliko mpaka ilipofika  52 ambapo kocha Hemed Morocco alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu alitoka Hamad Juma, Danny Lyanga na Othman Tamim akaingia Mbwana Kibacha, Suleiman Kassim ‘Selembe’ na Abdi Banda.
Kocha akabadili mchezo ambapo Masumbuko sasa akawa anapiga krosi kutoka kushoto au mara nyingine anamuachia Banda aliyekuwa akisaidiana na Uhuru apige huku yeye anaingi katikati mwenyewe. Taktik hiyo ilizaa matunda dakika ya 72 ya mchezo ambapo krosi ya Banda ndiyo iliyotua mguuni mwa Masumbuko na kupeleka kilio jijini Kampala.
Baada ya hapo Coastal Union wakawa wanalisakama lango la URA bila shaka kupata bao la pili ili kujihakikishia ushindi.
Kufikia dakika ya 85 almanusra URA wasawazishe baada ya Shaaban Kado kujaribiwa shuti la mbali na kumponyoka kwa bahati nzuri liligonga mwamba wa juu na kutoka nje ikawa kona. Ilipopigwa kona mpira ukambabatiza tena na kutaka kuingia lakini akautoa tena ikawa kona pacha.
Vitendo hivi vya dakika mbili viliwanyamazisha mashabiki 8000 wa Coastal Union waliohudhuria na kuwapa nguvu mashabiki wachache wa URA waliokuwa kwenye benchi lao kutokana na kuamini kuwa lolote linaweza kutokea. Kwa bahati nzuri kona ya pili haikuzaa matunda.
Baada ya hapo Wagosi wakaanza kucheza kiujanja ili kupoteza muda baada ya kugundua URA wanaweza kuwachangua udhu kabla ya magharibi kuingia na futari ikawatumbukia nyongo. Hatimaye mwamuzi akamaliza mpira yakatimia yale ya wazee kuwa mfupa uliomshinda fisi mbwa kautafuna.
Kikosi cha Coastal Union kilikuwa: Shaaban Kado, Hamad Juma, Othman Tamim, Marcus Ndehele, Juma Nyosso, Jerry Santo, Uhuru Suleiman, Crispian Odula, Daniel Lyanga, Haruna Moshi ‘Boban’, na Keneth Masumbuko. Akiba ni: Said Lubawa, Mbwana Kibacha, Abdi Banda, Philip Mugenzi, Mohamed Sudi, Pius Kisambale, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Green Atupele na Abdallah Othman.
Baada ya mechi kuisha mwandishi hakupata bahati ya kuzungumza na mwalimu Morocco maana alikuwa anamvizia kocha wa URA, ambapo alipompata na kuzungumza mambo mengi kuhusu timu yake na ziara ya Tanzania shukran katika mazungumzo yake hakugusia kuchoka kwa timu yake ambapo makocha wa kibongo wengi hutumia kama kisingizio.
“Tanzania kuna timu nzuri, hata mimi nimekuja kujaribu wachezaji wangu wapya wapo saba kwa hivyo sikuwa na uchungu sana kupoteza mechi hii lakini timu tatu nilizocheza nazo hapa nchini naziona zote zipo sawa.”
Akaulizwa amecheza na Simba ameshinda 2-1, akacheza na Yanga akatoka suluhu ya 2-2 leo amecheza na Coastal Union wamepoteza kwa bao 1-0 vipi maelezo yake. Akajibu: “The answer is simple, timu iliyonifunga ndiyo best.”
COASTAL UNION
25 JULAI, 2013
TANGA, TANZANIA   



No comments:

Post a Comment