Tuesday, July 9, 2013

Coastal Union 1-0 JKT Oljoro, Rollingstone CUP Under 20 Arusha.

 Walinda mlango wa Coastal Union U20 kushoto Mansour Alawi, kulia Adamu Musaa wakijadiliana namna ya kuwawekea ngumu maafande wa JKT Oljoro leo. Baada ya filimbi ya mwisho matokeo yalikuwa Coastal Union 1-0 JKT Oljoro.

Huyu ndiye Ally Nassor 'Ufudu' aliyepachika bao la pekee kwenye mechi ya leo dhidi ya Oljoro. pembeni yake ni meneja na timu B, Abdulrahman Mwinjuma 'Ubinde'.


Mshambuliaji chipukizi wa Coastal Union chini ya miaka 20, Ally Nassor ‘Ufudu’ ameanza kuwa gumzo jijini Arusha baada ya kupachika mabao katika mechi mbuili mfululizo zilizochezwa jana na leo huku akiwa msumbufu kwa mabeki wa timu pinzani.
Coastal Union wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande wa JKT Oljoro kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid kwenye michuano ya vijana chini ya miaka 20 Rollingstone inayofanyika kwa mara ya 14 mfululizo tangu ilivyoanzishwa mwaka 1999 na kituo cha kukuza vipaji jijini humo cha Rollingsone Academy.
Wagosi walijipatia bao la kwanza na la pekee kwenye mechi ya leo baada ya kutoka vichwa chini kwenye dakika 45 za mwanzo kutokana na timu zote kucheza kwa kuviziana kwakuwa zinafahamiana aina ya uchezaji kwa kipindi kirefu.
Kama kawaida yake kocha wa Wagosi wa kaya Bakari Shime huwa anautumia vema muda wa mapumziko kwa kuwaelekeza wachezaji wake nini cha kufanya, hivyo mnamo dakika ya 49 Ally Ufudu alipokea pasi murua kutoka kwa Mohammed Issa ‘Banka’ na kumsukumia shuti kali golikipa wa Oljoro ambaye alishindwa kujinyoosha na kuuangalia mpira ukitinga wavuni bila msaada wowote.
Baada ya hapo Oljoro walikasirika na kuelekeza mashambulizi ya kasi langoni mwa Coastal Union lakini golikipa mwenye mbwembwe nyingi na ujuzi wa hali ya juu Mansour Alawi Mansour aliwakatisha tama washambuliaji wa maafande hao kwa kuzuia mashuti yao hafufu kwa mkono mmoja huku akisaidiwa na mabeki wenye roho ngumu wa Coastal Union, Mwaita Saleh, Hussein Zolla na nahodha wa kikosi cha ubingwa Nzara Ndaro.
Hata hivyo Ally Ufudu manusura awanyanyue katika benchi viongozi wa Coastal Union baada ya kuwapangua mabeki wa Oljoro halafu akabaki yeye na golikipa mnamo dakika ya 70 ya mchezo lakini kwa bahati mbaya akapata kigugumizi cha miguu na kupaisha mpira ikawa ni goal kick.
Aidha, Kikosi kilichoanza leo ni 1. Mansour Alawi, 2.Mwaita Saleh, 3.Hussein Amri ‘Zolla’, 4.Nzara Ndaro (captain), 5.Yusuf Chuma ‘Croach’, 6.Aziz Fatawi, 7.Mohammes Issa ‘Banka’, 8.Behewa Sembwana, 9.Mohammed Hassan, 10. Alli Nassor ‘Ufudu’, 11.Ayoub Semtawa.
Siku ya jana vijana  walicheza na Young Life wakashinda 3-0 ambapo Ally Ufudu alipachika mabao mawili peke yake huku Behewa Sembwana akifunga bao moja hivyo mpaka sasa wana point 6 na taarifa zinasema keshokutwa watashuka dimbani kukamilisha hatua ya makundi dhidi ya Testimonial Academy pia kutoka Arusha.
COASTAL UNION
9 Julai, 2013


No comments:

Post a Comment