Tuesday, July 23, 2013

Coastal Union kucheza mechi ya kwanza ya kimataifa dhidi ya URA kesho.


Timu ya soka Coastal Union ‘Wagosi wa kaya’ kutoka Tanga kesho itashuka dimbani kucheza pambano la kirafiki la kimataifa dhidi ya Uganda Revenue Authority (URA) katika uwnaja wa Mkwakwani saa kumi alasiri.


URA kutoka Uganda waliokuja nchini kwa mechi za majaribio kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi nchini mwao tayari wameshacheza mechi mbili kati ya Simba na Yanga.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Wagosi wa Kaya, Hemed Hilal ‘Aurora’ timu yake itacheza na URA ili kutuma salamu kwa timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu Tanzania bara kutokana na usajili kabambe walioufanya mwaka huu.
“Hii mechi si rahisi kama watu wengine wanavyodhani lakini tumeamua kucheza na URA kama moja ya kampeni yetu ya kutuma salamu kwa timu zinazoshiriki ligi kuu, maana Simba na Yanga wameshindwa kuwafunga hawa waganda lakini sisi tutawafunga.
“Kauli mbiu ya timu yetu msimu ni ubingwa, mkumbuke hii ni mechi ya kwanza kubwa tangu tumalize ligi kuu msimu uliopita, wachezaji wengi ni wapya na bado hawajajuana vizuri lakini baada ya kuzungumza na kocha akasema hana neno na kikosi chake kipo tayari kwa mechi, hivyo mashabiki wetu waje kwa wingi kuangalia mechi hii ili hawa waganda wasijisifu kuwa wamekuja Tanzania na hawajafungwa mechi hata moja,” alisema aurora.
Naye kocha mkuu wa Wagosi, Hemed Morocco amesema kikosi chake ni kizuri ingawa bado mazoezi hayajawakolea kwani hawana muda mrefu tangu waingie kambini, lakini anaamini watawapa furaha mashabiki wa Tanga kwa mechi ya kesho.
Alipozungumzia suala la washambuliaji ambalo lilikuwa tatizo msimu uliopita Morocco alisema, ‘Bado sijapata mshambuliaji, nimeangalia katika timu nzima sijaridhika na safu ya ushambuliaji lakini hakuna kinachoshindikana ligi inaanza msimu ujao hawahawa nilio nao nitawaelekeza namna ya kufanya maana kazi ya kocha ni kumfundisha mchezaji kufanya asichokijua.”
Katika hatua nyingine Morocco alitoa ufafanuzi wake juu ya upangwaji wa ratiba ya msimu unaoanza mwezi ujao kwa kusema hana tatizo na ratiba.
“Sina matatizo sana na upangwaji ratiba huwa naamini ni lazima tucheze mechi mbili, moja nyumbani na nyingine ugenini sasa hata iweje ratiba lazima izunguke. Hata sisi Coastal Union hatuna tabu sana maana ratiba inaonyesha katika mzunguko wa kwanza tunacheza mechi saba ugenini na sita nyumbani ni kama nusu kwa nusu haina tabu tutacheza soka.”
Kwa upande wake nahodha msaidizi wa Wagosi Mbwana Kibacha, amesema “Wachezaji wana morali ya juu sana ingawa hatuna muda mrefu tangu tuingie kambini lakini katika mazoezi tunaelewana na hata juzi tulicheza mechi ya wenyewe kwa wenyewe nadhani kocha ameridhika na kiwango tulichoonyesha.
“Kuhusu kuchelewa kuanza mazoezi sina tatizo sana maana wachezaji wote walianza mazoezi wakiwa nyumbani, unajua mchezaji anayejitambua huwa hakai kizembezembe hivyo wote wamekuja tayari wakiwa wameiva.”
URA tangu imekuja nchini imecheza mechi mbili dhidi ya Simba jumamosi iliyopita ambapo Simba walilala kwa mabao 2-1, mechi nyingine walicheza dhidi ya Yanga ambapo walitoka suluhu ya 2-2 ikiwa Coastal Union watachapwa katika mechi ya kesho URA wataondoka Tanzania wakiwa kifua mbele akini ikiwa watatulizwa basi Wagosi hao watapata sifa kubwa.  
Aidha wachezaji wapya wa Coastal Union ni Haruna Moshi 'Boban', Juma Said 'Nyosso', Marcus Ndehele na golikipa Said Lubawa, kuna mchezaji kutoka Jamhuri ya Pemba Abdullah Othman Ali, mwingine ni Kenneth Masumbuko na Uhuru Suleiman aliyekwenda kwa mkopo kutoka Azam FC. Huku kutoka Kenya wakinasa mchezaji mmoja wa Bandari Mombasa,
NB: blog ya Coastal Union inafanya taratibu za kuhakikisha itakuwepo kwenye mechi ili kupata picha na matukio mbalimbali, lakini pia kwa wale wafanyabiashara blog hii inafungua milango kutangaza nasi kwa bei nafuu ili kuipa uwezo wa kusafiri na timu kila inapokwenda. Wasiliana nasi kwa namba +255 752 593894/ +255 713 593894.
COASTAL UNION
23, JULAI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment