Sunday, July 7, 2013

Timu B kucheza na Young Life uwanja wa General Tyre jijini Arusha kesho.


Timu B ya Coastal Union itashuka dimbani kesho kutupa karata yao ya mwanzo dhidi ya Young Life ya mjini Arusha kwenye michuano maarufu ya vijana wanaotoka nchi za Afrika Mashariki na kati, Rolling Stone.
Michuano hiyo inayofanyika jijini Arusha imeanza rasmi jana ambapo Azam FC waliibuka na karamu ya mabao 3-0 dhidi ya Eagle FC kutoka Tanga hivyo kuwa mwanzo mbaya kwa mkoa wa Tanga.
Kwa mujibu wa meneja wa timu B, Abdulrahman Ubinde timu imewasili jana jioni ikiwa na wachezaji 20, kocha Bakari Shime pamoja na daktari wa timu Mzee Francis Mganga, tayari kuanza kampeni ya kuchukua ubingwa.
Mpaka sasa ratiba rasmi ya michuano hiyo haijatolewa kwani zipo taarifa kuwa baadhi ya timu zilizothibitisha ushiriki bado hazijawasili kambini hivyo kuwawia vigumu waandaaji wa michuano hiyo kupanga ratiba kwa kuchelea kuweka timu ambayo haitafika.
Taarifa rasmi zinaweka wazi kuwa Coastal Union watashuka dimbani kukabiliana na Young Life kesho saa nane mchana katika uwanja wa General Tyre jijini humo.
Mungu ibariki Coastal Union Mungu ubariki jiji la Tanga.
COASTAL UNION
7 Julai, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment