Thursday, November 28, 2013

Coastal Union hiyooooo Fainali Uhai Cup. Kwa mara ya pili mfululizo









COASTAL Union, wameudhihirishia umma kuwa mwaka jana walipoingia fainali ya Uhai Cup, hawakubahatisha baada ya kuwatoa Azam FC, katika mechi ya leo hatua ya nusu fainali ya kombe hilo uwanja wa Chamazi, Azam Complex jioni hii.

Kufungwa kwa Azam FC bao 1-0, imekuwa pigo kubwa kwa timu hiyo hasa ikizingatiwa katika mechi ya ufunguzi walitandikwa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Karume Ilala jijini.

"Sisi kwa sasa tumeshafuta rekodi yao ya kutufunga mara mbili, walitufunga katika mechi ya fainali michuano hii hii mwaka jana baada ya dakika tisini wakatufunga kwa matuta. Baadaye mwaka huu katika michuano ya Rollingstone jijini Arusha wakatutoa kwa matuta kwenye hatua ya nusu fainali.

"Sasa sisi tumelipiza vipigo vya katika michuano hii hii, wao walitufunga katika michuano miwili tofauti tena kwa matuta, lakini sisi tumewafunga mara mbili mfululizo kwa tofauti ya wiki moja tu tena kwa dakika tisini," alijitapa beki wa kushoto wa Coastal Union Ayoub Masudi.

Bao la Wagosi lilipatikana dakika ya 32 kipindi cha kwanza baada ya Ally Nassor 'Ufudu' kukimbia na mpira kitokea katikati na kumpenyezea Mohammed Rajab ambaye aliwekwa kati na mabeki wawili wa Azam FC, lakini akawashinda nguvu na mbio, mwisho akabaki yeye na kipa, akapiga shuti hafifu ambalo lilipita juu ya goikipa huyo ambaye aliinua macho bila msaada huku mpira ukitinga wavuni.

Baada ya hapo Coastal Union, walicheza mpira wa kasi na kuonana hali iliyozidi kuwachanganya Azam ambao walikuwa wakizomewa na uwanja mzima.

Mpaka mapumziko matokeo yalibaki hivyohivyo 1-0, kipindi cha pili Azam walirudi na ari wakacheza nusu uwanja kwa takriban dakika ishirini, Coastal Union walionekana kupoteza mwelekeo na hawajui cha kufanya.

Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya kocha wa Azam kuingiza wachezaji wannne ndani ya dakika tano, hali iliyowafanya Wagosi kuzidi kuelemewa na kuamua kurudi nyuma kulnda lango badala ya kuongeza bao la pili.

Awali wakati kipindi cha pili kinaanza Kocha Joseph Lazaro alimtoa Mohammed Issa 'Banka' na kumuingiza Hussein Amir 'Zola. baadaye ilipotimia dakika ya 40 alitoka Mahadhi Juma, ambaye leo alicheza chini ya kiwango na kuingia Dihile Said, kabla ya mchezo kuisha aliingia Ramadhan Juma 'Batisata' na kutoka Mohammed Rajabu.

Coastal Union dakika kumi za mwisho walicheza soka la kuvutia na kujiamini kiasi walishangiliwa na uwanja mzima.

Mechi ya fainali itakayochezwa Jumapili wiki hii saa tisa alasiri uwanja wa Chamazi, inasubiri mshindi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar ambayo itapigwa kesho uwanja wa Chamazi.

COASTAL UNION
28 NOVEMBA, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Tuesday, November 26, 2013

Coastal Union yafanya kama ilivyofanya Arusha...


 Hawa jamaa wa Azam TV wametuchelewesha sana kuanza mechi.....

 Alitupiwa, akaipokea vizuri Mohammed Rajabu......

 Alipokunjuka akakutana na kigingi....

Ufuuuduuu vipi?

                                                       Furaha ya ushindi lazima ucheze ndombolo.

 Kipanga kila alipopokea mpira, pembeni yake alikuwa na wachezaji watatu wa JKT Oljoro. Huyu kijana yupo vizuri sana, aangaliwe kwa jicho la kulelewa kisoka.

Hapa Kocha Mkuu wa timu ya Viajana, Joseph Lazaro akizungumza na vijana wake, vipi jamaaani?
                                    Kosakosa langoni mwa Coastal Union hazikukosekana.

                                Leo Kipanga alikabwa na wachezaji watatu dakika zote.

 Nahodha wa Coastal Union, Nzara Ndaro akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mechi ya leo.

                   Nahodha Nzara Ndaro akiwasalimia mashabaki kuwashukuru baada ya mechi.

                               Safari ya kuelekea Arusha ilianzia Chamazi baada ya mechi.

MNAMO dakika ya 6 ya kipindi cha kwanza baada ya kulisakama lango la JKT Oljoro kwa takriban dakika tatu mfululizo, wachezaji Ayoub Semtawa na Mtenje Albano walipigiana pasi nje kidogo ya eneo la kujidai golikipa wa Oljoro.

Baadaye Juma Mahadhi akawazidi ujanja mabeki wa Oljoro akapokea pasi murua kutoka kwa Mtenje ambaye alijifanya kama anapiga mabeki walipogeuka akampa Mahadhi ambaye aliukokota mara mbili akainua uso kumuangalia golikipa amekaa upende gani, akakunjuka shuti kimo cha paka upande wa kushoto ukapuchua mwamba na kuzama ndani.

Baada ya bao hilo Oljoro walijitahidi kujibu mashambulizi lakini mabeki wa Coastal Union, walikuwa imara kumlinda golikipa wao.

Hata hivyo vijana wa Wagosi wa Kaya walikosa nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza kutokana na kukosa mawasiliano baina yao na uvivu wa kuvika langoni mwa Oljoro kila zilipomiminwa krosi..

Kabla ya kipindi cha kwanza kuisha Kocha Joseph Lazaro alimtoa Abdallah Waziri akamuingiza Zungu, ambapo mpaka timu zinakeenda mapumziko bado bao lilibaki 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Oljoro kuja juu na kucheza mpira wa kasi kitu kilichoisumbua ngome ya Wagosi wakapoeza mwelekeo.

Baada ya Lazaro kuona hali mbaya akafanya mabadiliko akamtoa Ayoub Semtawa na kumuingiza Mwaita, baadaye akamtoa Ally Ufudu na kumuingiza Raizini Haji, halafu ilipofika dakika ya 31 kipindi cha pili alimtoa Juma Mahadhi na kumuingiza Batista.

mabadiliko hayo yalirudisha uhai kidogo katika kikosi cha Wagosi ambao kama si golikipa wao kuwa imara bao hilo lingerudishwa katika dakika za awali za kipindi cha pili.

Hata hivyo mpaka kipyenga cha mwisho kinapulizwa, matokeo bado yalisomeka 1-0, ambapo hali hiyo iliashiria kitu kimoja tu. JKT Oljoro wana safari ya kurudi Arusha kama si leo usiku basi kesho alfajiri baada ya kuaga michuano ya Uhai.

Itakumbukwa katikati ya mwezi huu mjini Arusha JKT Oljoro na Coastal Union walikutana katika hatua hihii ya robo fainali ya michuano ya Rollingstone Oljoro wakatolewa kwa bao 1-0. Hivyo imedhihirisha hawa ni wateja wetu.

Mechi ijayo itachezwa katika uwanja wa Azam Complex Chamazi siku ya AlhamisiNovemba 28, katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Azam FC saa tisa alasiri.
COASTAL UNION
NOVEMBA 26, 2013
DAR ES SALAAM TANZANIA

Monday, November 25, 2013

Maandalizi ya robo fainali Uhai Cup.







Kesho asubuhi saa mbili katika uwanja wa Azam Complex 'Chamazi', Vijana wa Coastal Union watashuka dimbani kupamabana na JKT Oljoro kwenye robo fainali ya Uhai Cup.

Picha hizi zinaonyesha wachezaji wa timu ndogo wakiwa katika fukwe za bahari Coco Beach, lengo likiwa ni kuburudisha nafsi na kutuliza akili kabla ya mechi.
COASTAL UNION
25 NOVEMBA, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Friday, November 22, 2013

Coastal Union yazidi kufanya vizuri kombe la Uhai

 Kikosi cha leo kilichomenyana na maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Karume jioni hii na kutka na ushindi wa mabao 2-1.

 Mohammed Rajabu wa Coastal Union, huyu ndiye aliyetumbukiza mabao yote mawili na kurudisha matumaini kwa Wagosi baada ya kuchapwa na Yanga katika mechi iliyipota.

 Ramadhan Shamte wa Coastal Union akitafuta mbinu za kuunyakua mpira kutoka kwa mchezaji wa JKT Ruvu.

 Kocha Yusuf Chippo akiwaambia cha kufanya pindi waingiapo dimbani, Ally Kipanga jezi namba saba na Ayoub Semtawa jezi namba 10. Baada ya kuingia wao ndipo mpira ukabadilika na mabao yote mawili kuingia.

Mbona hamuingii/ Nimesema nyote mjae kati maana pale mipira ikiingizwa inakosa watu.....

Bao la dakika ya 69 lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa timu B, Mohammed Rajabu ndilo lililoibua matumaini ya kuendelea na michuano hiyo baada ya kuamini mechi ya leo itaisha kwa kufungwa ama kutosa suluhu kitu ambacho kingewafungisha virago wagosi.
Ilikuwa ni piga nikupige katika lango la JKT Ruvu, ndipo Juma Mahadhi alipoudaka mpira nje ya 18 na kumpenyezea Mohammed Rajabu ambae aliwakuta mabeki wa Ruvu wamejisahau akapenya na mpira mpaka akakutana na golikipa wa Ruvu, Patrick Matui akamlamba chenga na kupiga shhuti hafifu lililotinga wavuni.
Awali katika dakika ya 49, dakika tatu tu baada ya kipindi cha pili kuanza, Thomas Ndimbo alitumia vema makosa ya mabeki wa Wagosi akaifungia bao la kuongoza timu yake hali iliyowavunja nguvu Wagosi ambao walianza vibaya kipindi cha kwanza.
baada ya bao hilo kuingia wavuni kocha wa Wagosi alikaa kama kamati na benchi lake la ufundi akawainua wachezaji wote wa akiba akiwaambia wapashe lengo likiwa ni kupiga ramli nani aingie akaokoe jahazi.
ndipo akafanya maamuzi ya kumuingiza Ally Kipanga na Ramadhan Shame. akawatoa Mohammed Issa na Hassan Amir. Baadaye akamtoa Raizn Hajji akamuingiza Mtenje Albano.
ndipo ilipofika dakika ya 88 ya mchezo Ramadhan Shame alimpenyezea mpira Mohammed Rajabu ambaye alikuwa katikati ya uwanja na kuanza kukimbizana na mabeki wa Ruvu huku golikipa akiwa langoni hajui la kufanya, alipoingia ndani ya box, Mohammed aliachia shuti kali kimo cha paka na kumpita golikipa wa Ruvu katika kwapa huku ukitinga wavuni na kuibua shangwe kwa mashabiki wa Wagosi waliojaa uwanja mzima.
baadaye mpira ulikuwa upande wa Ruvu huku kosakosa zikiwa nyingi kabla mwamuzi kupuliza kipyenga cha mwisho kuashiria mchezo huo umesiha kwa Wagosi kuibuka na mabao mawili kwa moja huku wakizoa point tatu na kufanya kuwa na jumla ya point 6.
Itakumbukwa mevhoi ya awali Coastal Union walishinda dhidi ya Azam FC 2-1, wakafungwa na Yanga bao 1-0 na leo wameshinda mabao 2-1 dhidi ya Ruvu JKT. Mechi ya mwishi itachezwa katika uwanja wa Chamazi Jumapili Novemba 24 saa mbili asubuhi dhidi ya Mbeya City.
hata hivyo mwalimu wa Coastal Union amelalamikia ratiba mbovu ya michuano hiyo kwani awali ratiba ilikuwa ikionyesha mechi ya JKT Ruvu na Coastal Union itachezwa Jumamosi Novemba 23, lakini asubihi ya leo walipokuwa wakijiandaa kuelekea mazoezini ndipo walipopata taarifa ya mabadiliko hayo.
COASTAL UNION
DAR ES SALAAM, TANZANIA
NOVEMBA 22, 2013

Tuesday, November 19, 2013

Coastal Union yakubali uteja mbele ya Yanga mechi za Uhai U20.












LEO vijana wa Coastal Union wamekubali uteja kwa kuchapwa bao 1-0 na vijana wa Yanga kwenye michuano ya Uhai inayoshirikisha timu za vijana zinazoshiriki Ligi kuu ya Vodacom, katika uwanja wa Karume Ilala jijini Dar es salaam.
Mechi hiyo iliyochezwa asubuhi saa mbili na kukamilika saa tatu na nusu, ilikuwa na ushindani mkubwa katika kipindi cha kwanza ambapo vuta nikuvute kati ya timu hizo ilikuwa kali, na hakukuwa na timu iliyotabiriwa kutoka kifua mbele kutokana na wote kucheza mchezo wa kujihami.
Kipindi cha pili kilianza kwa Coastal Union kulikamia lango la Yanga lakini mabeki wa timu hiyo walikuwa makini kuhakikisha golikipa wao hapati kashkash zozote.
Coastal Union walianza kuonekana kukata tama ya ushindi baada ya kushindwa kutumia vema nafasi nyingi walizopata katika dakika ya 50 na 60 ya mchezo.
Ilipofika dakika ya 65 Yanga waliliandama lango la Coastal Union hali iliyowafanya mabeki wa pembeni kupoteza mwelekeo hasa beki wa kulia Aoub, alionekana kuzidiwa nguvu.
Nahodha wa timu hiyo Nzara Ndaro, naye alionekana kucheza chini ya kiwango hali iliyomfanya kupoteza mwelekeo na kufanya nafasi aliyokuwepo, beki wa katikati kuonekana kamaa haina mwenyewe.
Ilipofika dakika ya 68 Hamis Issa wa Yanga aliipatia bao la kwanza na la pekee katika mechi ya leo baada ya piga nikupige katika lango la Wagosi na kumuacha golikipa akiwa peke yake mabeki wameanguka pembeni. Hamis akautumbukiza mpira wavuni baada ya kupokea krosi kutoka upande wa kushoto.
Hali iliendelea hivyo mpaka dakiak tisini za mchezo kukamilika, ubao ukawa unasomeka Yanga 1-0 Coastal Union.
Kutokana na matokeo hayo Yanga wamejizolea point sita na mabao mawili baada ya mechi ya kwanza kuwafunga Mbeya City bao 1-0. Coastal Union wataendelea kubaki na point tatu na mabao mawili baada ya mechi ya juzi kuwafunga mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC mabao 2-1 katika uwanja huohuo wa Karume.
Mechi ijayo ya Coastal Union katika kundi lao itachezwa katika uwanja wa Chamazi Saa kumi alasiri siku ya Jumamosi Novemba 23.
Hii ni mara ya pili Coastal Union, wanashiriki michuano hiyo ya Uhai ambapo mwaka jana walifika mpaka hatua ya fainali wakatolewa kwa matuta na Azam FC.
COASTAL UNION
NOVEMBA 19, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA