Saturday, November 2, 2013

Coastal Union walazimishwa suluhu na Mgambo Mkwakwani leo.















INAWEZEKANA bahati haijakuwa yetu ama wachezaji hawajakuwa tayari kuipa furaha Coastal Union katika msimu huu.
Suluhu tasa ya leo dhidi ya Mgambo JKT, inazidi kudidimiza ndoto za Wagosi wa kaya kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi wakiwa katika nafasi nzuri, ili katika mzunguko wa pili wawe wamejipanga zaidi.
Dakika ya pili tu ya mchezo wa leo Masumbuko Keneth wa Wagosi alipokea pasi akiwa upande wa kulia, akawazidi ujanja mabeki wa Mgambo akaingia nao kwenye box  na kukunjuka shuti kali lakini likaenda fyongo.
Kama hiyo haitoshi Masumbuko huyohuyo katika dakika ya 22 kipindi cha kwanza akiwa winga ya kushoto alipokea pasi kutoka kwa Uhuru Suleiman ambaye alipiga mpira mrefu ukatua miguuni mwa Masumbuko, akawekwa mtu kati na mabeki wawili wa Mgambo lakini akawazidi mbio, kwa kujiamini akapiga shuti kwa mguu wa kushoto lakini likatoka nje mita chache na kugonga nyavu ndogo.
Mgambo walionekana wamechanganyoikiwa kutokana na kasi ya Wagosi wakaanza kupoteza mwelekeo. Mnamo dakika ya 24, Danny Lyanga alipokea pasi akiwa nje kidogo ya box, akapiga chenga na kuingia nao ndani kwa kasi kubwa mpaka katika box dogo lakini akapoteza mwelekeo na shuti lake halikuleta madhara.
Mambo yalizidi kuwa mabaya kwa upande wa Mgambo, mashabiki wa Coastal Union wakaanza kushangilia kwa nguvu wakiamini mchezo wa leo watashinda mabao mengi kutokana na mchezo kuwa wa kasi sana.
Danny huyohuyo ilipofika dakika ya 28 almanusura aipatie bao Coastal Union baada ya kuminyana na mabeki wa Mgambo ambao tayari walishakubali kuwa wamezidiwa nguvu. Akaingia mpaka kwenye box dogo lakini kadhalika shuti lake halikuzaa matunda. Akaanza kuzomewa na mashabiki wake.
Mpaka timu zinakwenda mapumziko hakuna aliyeona lango la mwenzake. Aidha Mgambo walitoka kichwa chini wakiamini mchezo wa leo hawana bahati nao.
Kipindi cha pili mwalimu Joseph Lazaro, alifanya mabadiliko akawatoa Suleiman Kassim ‘Selembe’ na Danny Lyanga wakaingia Haruna Moshi na Yayo Kato.
Ilipotimu dakika ya75 Mgambo walipata bao, lakini mwamuzi wa leo Geofrey Tumaini kutoka Dar Es Salaam akasema wameotea.
Baadaye hali ilizidi kuwa mbaya kwa upande wa Coastal Union ambapo Mgambo walishambulia kwa kasi wakitaka kupata bao la kuongoza lakini mabeki wa Coastal Union walikuwa makini.
Mpaka kipyenga cha mwisho wachezaji wa Coastal Union walipewa kadi za njano tatu ambapo Hamad Juma, Jerry Santo na Juma Nyosso walionyeshwa kadi moja moja kwa kucheza madhambi.
Kutokana na matokeo hayo ya suluhu ya bila kufungana Coastal Union imeambulia point 16 tukiendelea kushikilia nafasi ya nane, mchezo wa mwisho dhidi ya JKT Ruvu katika uwanja wa Chamazi siku ya jumatano wiki ijayo itamaliza utata juu ya nafasi watakayomaliza wagosi katika mzunguko wa pili.
Kikosi cha leo: Shaaban, Kado, Hamadi Juma, Othamna Tamim, Mbwana Kibacha, Juma Nyosso, Jerry Santo, Uhuru Suleiman, Crispian Odula, Masumbuko Keneth, Danniel Lyanga, Suleiman Selembe.
Sub: Said Lubawa, Haruna Moshi, Abdi Banda, Mohammed Sudi, Razakh Khalfan Marcus Ndehele, na Yayo Kato.
COASTAL UNION
2 SEPTEMBA, 2013
TANGA, TANZANIA

 

No comments:

Post a Comment