Saturday, January 18, 2014

Mechi ya leo Seeb Club Vs Coastal Union



COASTA Union Wagosi wa Kaya, Wagosi wa Ndima, leo watashuka dimbani dhidi ya timu ngumu inayoshika nafasi ya nne katika ligi kuu ya Oman, Seeb Club.
Seeb SC, ambao wamecheza mechi 12 wameshinda mechi sita kutoa suluhu tano na kupoteza mchezo mmoja hivyo kuambulia point 23, wakiwa wamepishana point mbili na timu inayoongoza ligi, Al Nahda Club ambayo ina point 25 ikiwa imecheza michezo 12, kushinda minane, kupoteza mitatu na kutoa suluhu moja.
Aidha katika mechi ya leo Wagosi watahakikisha wanacheza kwa umakini ili kuondoka na jina zuri nchini Oman, ambapo mpaka sasa klabu nyingi zinatuma maombi ya kutaka kucheza na Wagosi baada ya kupata taarifa ya ushindi wa mfululizo katika mechi mbili za awali dhidi ya Al Mussannah inayoshika nafasi ya saba katika ligi kuu na Oman Club iliyo daraja la kwanza.
Mechi ya leo itachezwa saa kumi alasiri katika uwanja wa Seeb Club, jijini Muscat ingawa mratibu wa mechi za Coastal Union nchini hapa Twalib Hilal, ametoa maelezo kuwa kutakuwepo na mechi ya tano kabla ya kuondoka Januari 23, kujiandaa na mechi ya ufunguzi mzunguko wa pili dhidi ya JKT Oljoro katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Itakumbukwa Coastal Union tangu iwasili nchini Oman, januari 9 mwaka huu kwa ziara ya wiki mbili, imeshacheza mechi tatu dhidi ya Al Mussannah Club, Oman Club na Fanja SC. Ambapo wameshinda mechi mbili kwa mabao 2-0 kila mechi na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Fanja SC kwa bao 1-0.
Kwa mujibu wa kocha mkuu wa Coastal Union, Yusuf Chipo timu yake imepata mambo mengi ambayo yamemsaidia katika mafunzo yake.
“Mbali ya utulivu kwa wachezaji lakini nimejifunza mambo mengi kutoka klabu za hapa, kuanzia ubora wa viwanja, serikali inavyopenda soka na vifaa vya kufundishia. Naamini vijana wangu wamejifunza mambo mengi vilevile na mzunguko wa pili utakuwa mzuri tusubiri,” alisema.
Kikosi cha leo kitakachoanza dhidi ya Seeb Club ni, Shaaban Kado, Hamadi Juma, Othman Tamim, Juma Said ‘Nyoso’, Mbwana Kibacha, Jerry Santo, Ally Nassor ‘Ufudu’, Haruna Moshi ‘Boban’, Atupele Green, Danny Lyanga na Yayo Kato Lutimba.
Wengine 12 waliobakia wanaweza kuingia kutokana na upungufu utakaojionyesha wakati mchezo ukiendelea.
COASTAL UNION
18, JANUARI 2014
MUSCAT, OMAN
+986 97695911

No comments:

Post a Comment