Thursday, October 17, 2013

Coastal Union yatua Mwanza na kufanya mazoezi katika uwanja wa CCM Kirumba ili kujiweka fiti.

 Kocha Mkuu wa Coastal Union Hemed Moroco (mwenye kofia), akiwa na viongozi wa timu hiyo Abdul Ubinde wa kwanza kulia na Miraji Wandi wa pili kulia, wa kwanza kushoto ni Uhuru Suleiman, kiungo wa timu hiyo; katika uwanja wa kimataifa wa JK nyerere kabla ya kupanda ndege kuelekea Mwanza na baadaye Bukoba kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu kati yao na Kagera Sugar siku ya Jumamosi wiki hii.
.


 Meneja wa Coastal Union, Akida Macha akiwa na Kocha wa timu hiyo Hemed Moroco...













COASTAL UNION
17OKTOBA, 2013
MWANZA, TANZANIA

Sunday, October 13, 2013

TUMEFUNGWA 2-1.

Masumbuko Keneth akikokota mpira kuelekea langoni mwa Ashanti UTD huku mwamuzi wa jana Anthony kutoka Rukwa akimtazama kwa makini. Coastal Union ililala 2-1.

 Krossi ya Masumbuka ikipenya kwenye kifua cha mchezaji wa Ashanti...

 Mganda, Yayo Kato akiwa ndani ya box la Ashanti lakini uwepo wake haukuleta madhara yoyote.

 Uhuru Suleiman akimimina majaro ndani ya box la Ashanti lakini hakuna mchezaji wa Coastal Union kuweza kupokea majaro hiyo.


 Nahodha Jerry Santo wa Wagosi wa Kaya akikokota mpira huku mchezaji wa Ashanti akimnyemelea.

 Atupele Green akigombania mpira na mchezaji wa Ashanti United katika kipindi ha pili.


 Shaaban Kado wa Coastal Union akiokoa moja ya hatari zilizosababishwa na mchezaji wa zamani wa Wagosi, Joseph Mahundi ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa Ashanti United.

 Kocha wa Coastal Union, Hemed Moroco akibishana na mwamuzi wa jana Anthony Kayombo, baada ya bao la pili la Ashanti kuingia kwa utata. Baadaye Moroco alitolewa nje ya uwanja.

 Mashabiki wa Wagosi wakiwa kimya baada ya bao la pili kuingia kwa utata.



Wachezaji wa Ashanti United, wakiwa na furaha baada ya mchezo wa jana kuisha kwa ushindi wa 2-1. Huo ndiwo ushindi wa kwanza wa Ashanti tangu ligi ianze. Na pia ndiwo mchezo wa kwanz akwa Coastal Union kuupoteza. 

BAO la pili lililofungwa na Tumba Sued, wa Ashanti United lilitosha kuwanyong’onyeza wachezaji wa Coastal Union na kukiri kuwa mchezo umeshaisha kwa mabao 2-1.
Ilikuwa ni dakika ya 85 baada ya mwamuzi Anthony Kayombo, kutoka Rukwa kupuliza filimbi akimaanisha mlinda mlango wa Wagosi wa Kaya amechezewa madhambi, lakini wakati walinzi wa Wagosi wakisubiri Kado apige mpira mara akatokea Tumba wa Ashanti na kuutumbukiza mpira wavuni, mwamuzi akasema ni bao.
Kulitokea rabsha kwa dakika kadhaa ambapo wachezaji waliokuwa eneo la tukio walibishana na mwamuzi, kadhalika kocha wa Wagosi alianza kumshutumu mwamuzi hatimaye aliamuliwa kutoka uwanjani.
Aidha kipindi cha kwanza Ashanti walicheza soka la nguvu lakini kwa bahati mbaya ilipofika dakika ya pili mmoja wa wachezaji wao aliunawa mpira katika eneo la hatari. Mwamuzi akasema ni penati na nahodha Jerry Santo akaitendea haki likaandikwa bao la kwanza.
Lakini kabla ya kipindi cha kwanza kuisha mchezaji wa Ashanti aliangushwa katika eneo la hatari na mwamuzi akasema ipigwe penati dakika ya 21, beki wa Ashanti Tumba Sued akasawazisha hivyo mpaka timu zinakwenda mapumziko ubao ulisomeka 1-1.
Kipindi cha pili Ashanti walishambulia kwa kasi kiasi wakawachanganya Coastal Union, mshambuliaji wa pembeni Joseph Mahundi alionekana mwiba kwa mabeki wa Coastal Union, hali iliendelea hivyo mpaka dakika ya thamanini lilipotokea zahma la bao la utata.
Tathmini ya mpira wa jana ni wazi wachezaji wa Wagosi wa kaya walizidiwa uwezo na timu inayoshika mkia Ashanti United.
Katika hatua nyingine kabla ya mchezo kuanza kulitokea utata wa jezi baada ya Ashanti United kutokeza uwanjani wakiwa na jezi nyeupe huku Coastal Union nao wakiwa na jezi nyeupe,  kutokana na sheria za mchezo mwenyeji ndiye anayeamua jezi ya kuvaa hivyo mgeni alitakiwa kubadili.
Kwa bahati mbaya jezi nyekundu za Wagosi wa Kaya hazikuwa uwanjani, ukatolewa ushauri kuwa wavae jezi nyeupe halafu waongeze jezi za mazoezi ambazo ni nyekundu lakini zimekatwa mikono.
Kwa matokeo hayo Coastal Union itaendelea kubaki na point 11 na kuna uwezekano ikashuka zaidi kutoka nafasi ya saba kutokana na matokeo ya jana na leo katika viwanja vya michezo nchini. Ambapo Simba wameendelea kujikita kileleni kwa kuvuna point 18 katika mechi ya jana na Yanga kukwea mpaka nafasi ya pili wakiwa na point 15.
COASTAL UNION
OKTOBA 12, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Friday, October 11, 2013

Sahihisho: Mechi kati ya Ashanti na Coastal Union ni Jumamosi Octoba 12.

Sahihisho,

Awali blogu hii iliandika kuwa mechi itakayowakutanisha Ashanti United 'Watoto wa Ilala' na Coastal Union 'Wana Mangush', katika uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, itachezwa Jumapili Octoba 13 mwaka huu, lakini kwa mujibu wa viongozi na nahodha wa Coastal Union mechi itachezwa Jumamosi Octoba 12.

Awali ratiba ya kamati ya Ligi iliyo chini ya shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliandika kuwa mechi hiyo itachezwa Jumapili, lakini baadaye wakakiri kukosewa kwa tarehe hiyo, ambapo usahihi ni kuwa mechi itapigwa siku moja nyuma.

Mwandishi wa Coastal Union, alijaribu kuwasiliana na msemaji wa TFF, Boniface Wambura, lakini simu yake haikupatikana. Ndipo akajaribu tena kuwasiliana na mwenyekiti wa timu, Hemed Hilal 'Aurora' ambapo simu yake ilikuwa 'busy' nadhani ni kutokana na kutumika sana.

Aidha mwandishi akaenda mbali zaidi na kuwasiliana na meneja wa timu ndogo ya Wagosi, Abdulrahman Mwinjuma 'Ubinde' juu ya usahihi wa ratiba na kubainisha mechi itachezwa Jumamosi na si Jumapili kama ilivyoripotiwa awali.

Mwandishi akawasiliana na nahodha wa Wagosi, Mkenya Jerry Santo, ambaye naye alimhakikishia kuwa ni kweli TFF waliwasiliana nao na kukiri ratiba ya awali ilikuwa si sahihi, hivyo mechi itachezwa Jumamosi katika uwanja wa Chamazi saa kumi alasiri.

Katika hatua nyingine blogu hii ilitoa msimamo tofauti juu ya nafasi inayoshikilia Coastal Union, ambapo awali iliandika kuwa Coastal Union ipo nafasi ya nne. Lakini usahihi ni kuwa Coastal Union ipo nafasi ya saba ikiwana  pointi 11, imecheza mechi saba, kushinda mbili na kutoka suluhu mechi tano.

Aidha timu inayoongoza ligi mpaka sasa ni Wekundu wa Msimbazi Simba, wenye point 15 ikifuatiwa na Azam FC point 14, Mbeya City point 14, Ruvu Shooting point 13, Yanga yenye point 12 na JKT Ruvu yenye point 12. Coastal Union point 11.

Timu nyingine ni Kagera Sugar yenye point 11, Mtibwa Sugar 10, Rhino Rangers 7, huku Tanzania Prison ikiwa na point 7, JKT Oljoro 5, Mgambo JKT point 5 na Ashanti United ikishika mkia kwa point 2 ikiwa imecheza michezo saba, ikafungwa michezo mitano, kutoa suluhu miwili na haikushinda hata mmoja.

Vilevile bado Coastal Union ipo kwenye orodha ya timu nne ambazo hazijapoteza hata mchezo mmoja ambazo ni Simba, Azam, Mbeya City na Coastal Union wenyewe.

Blogu hii inaomba radhi kutokana na usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na mkanganyiko wa ratiba. Mara nyingi TFF hubadili ratiba kutokana na sababu mbalimbali kila zinapojitokeza.

Baada ya mechi ya Jumamosi mwandishi atakwenda ofisi za TFF ili kupata ratiba kamili hasa baada ya kutokuwa na uhakika zaidi juu ya mechi nyingine zilizobaki.

COASTAL UNION
OCTOBA 11, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA.

Thursday, October 10, 2013

Coastal Union kuvaana na Ashanti bila Boban, Hamadi.



JINAMIZI la kadi nyekundu linazidi kuiandama klabu kongwe ya Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' baada ya wiki iliyopita beki kinda Hamadi Juma 'Basmat', kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba, baada ya kupishana maneno na mchezaji wa Azam FC Kipre Tchetche.

Hali hiyo inamfanya Hamadi kuungana na kiungo mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban', ambaye alionyeshwa kadi nyekundu mjini Mbeya katika mechi baina ya Wagosi wa Kaya na Mbeya City.

Kukosekana wachezaji hao katika mechi itakayochezwa Octoba 12, siku ya Jumamosi kati ya Ashanti United na Coastal Union kwenye uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, kutamlazimisha mwalimu wa Wagosi, Hemed Moroco kubadili mfumo wa ushambuliaji kwa mara nyingine baada ya awali kumtumia Boban kucheza nafasi ya kiungo namba nane, lakini baadaye akawa anamtumia kama mshambuliaji wa kati, katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Tanga ambapo iliisha kwa sluhu ya bila kufungana mwalimu Moroco aliwatumia mganda Yayo Kato na Pius Kisambale lakini mfumo huo haukuonekana kuleta uhai.

Kwa mujbu wa mwalimu msaidizi wa timu hiyo, Ally Ahmed 'Kidi' Wagosi wa Kaya wana mifumo mingi ambayo huwasaidia kubadilika kila wanapokutana na timu yenye mfumo tofauti. Mathalan kwa kipindi kirefu walikuwa wakitumia mshambuliaji mmoja mbele, lakini mechi ya juzi walitumia washambuliaji wawili. Hivyo katika mechi ya Ashanti wanaweza kubadilika na kutoka kivingine.

"Sisi hatutumii mfumo mmoja, wapinzani wetu wanatujua kwa namna tunavyobadilika na ndiyo maana utaona wanatumia zaidi msaada wa waamuzi kwa kuwanunua maana wanajua hawatuwezi," lisema Kidi.

Hata hivyo Coastal Union ipo katika hatihati ya kuwa timu isiyo na nidhamu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya kadi nyekundu baada ya mpaka mechi ya saba kufikisha idadi ya kadi nne kati ya kadi 12 zilizotoka katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara mpaka sasa.

Baada ya mechi ya Ashanti Jumamosi wiki hii, Wagosi watasafiri mpaka Bukoba katika uwanja wa Kaitaba kukutana na wakata miwa wa Kagera, kagera Sugar.

Mpaka saa Coastal Union yenye makazi yake Jijini Tanga, imeshacheza mechi Saba imeshinda mbili na kutoa suluhu tano, na kuwa miongoni mwa timu nne ambazo hazijapoteza hata mechi moja tangu ligi ianze. Timu hizo ni (Simba, Azam FC, Mbeya City na wao Coatal Union).

Aidha Wagosi wamefikisha pointi 11 ikiendelea kushikilia nafasi ya tano katika msimamo wa ligi baada ya Simba, Yanga, JKT Ruvu na Azam.

COASTAL UNION
OCTOBA 11, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Monday, October 7, 2013

Nassor Binslum afiwa na baba yake.

TANZIA

Blogu hii kwa niaba ya uongozi wa Coastal Union, mjini Tanga inaungana na familia ya Nassor Ahmed Binslum kutokana na msiba wa baba yake uliotokea jana nchini India.

Binslum ambaye ni mwanachama wa Coastal Union na mtu aliyeshiriki kwa kiasi kikubwa kusaidiana na viongozi wa timu kuifikisha klabu hapa ilipo, alikuwa na baba yake nchini India ambaye naye enzi za uhai wake alikuwa mnazi mkubwa wa Wagosi wa kaya.

Mzee Ahmed aliugua kwa muda mrefu na alikaa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) kwa takriban mwezi mmoja, mpaka jana jioni roho yake iliporudi kwa MwenyeziMungu.

Taarifa za awali kutoka katika familia ya Binslum zinaeleza kuwa maziko yatafanyika hukohuko India, na kwa wale wanaotaka kutoa pole wanaweza kuwasiliana na Ally Kiraka ama ndugu yake Nassor yaani Mohammed Binslum.

SOTE NI WAJA WA MWENYEZIMUNGU NA KWAKE TUTAREJEA.

COASTAL UNION
OCTOBER, 2013

Saturday, October 5, 2013

Coastal Union yapokonywa tonge mdomoni na Azam FC mjini Tanga.

 Kikosi cha leo kilichoanza kutoka nyuma kushoto Pius Kisambale, Crispian Odulla, Juma Nyoso, Jerry Santo, Othman Tamim, kutoka mbele kushoto, Mbwana Kibacha, Uhuru Suleiman, Masumbuko Keneth, Yayo Kato, Hamadi Juma na golikipa Shaaban Kado.

 Leo golikipa wa Azam Mwadini Ally alikuwa na wakati mgumu sana, ingawa bahati haikuwa ya Wagosi.

 Hamadi Juma katika hekaheka za kuondoa hatari langoni mwa Wagosi.

 'Nipishe' Ni kama Pius Kisambale akimwambia beki wa Azam ili amimine krosi kwa vijana wake.

                             Yayo Kato akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Azam FC.

 Nahodha Jerry Santo akikunjuka nje kidoo ya lango la Azam, ingawa shuti lake halikuleta madhara.

 Kocha wa Coastal Union, Hemed Moroco akiwabwatukia wachezaji wake wacheze kama alivyowafunza.




 Hili ndilo bao la kipindi cha pili walilokosa Coastal Union, ambapo shuti la Selembe lilipita mikononi mwa Mwadini Ally na kugonga mwamba.



SULUHU ya bila kufungana kati ya Coastal Union na Azam FC katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga imezidi kuwaongezea idadi ya suluhu Wagosi wa kaya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Mchezo huo uliokuwa na presha kubwa kwa mashabiki na wachezaji ulimuweka katika wakati mgumu mwamuzi Andrew  Shamba kutoka Pwani, kutokana na kushutumiwa kuwapendelea Azam FC.

Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa nguvu zikihakikisha zinapata mabao ya mapema na kujihakikishia ushindi lakini hakuna hata timu moja iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kushambulia kwa kasi huku wakimiliki mpira hali iliyowachanganya wachezaji wa Coastal Union wakaanza kupoteana na kucheza bila kufuata mfumo. Hali hiyo ilizidi kuwachanganya Wagosi wa Kaya hasa baada ya mwamuzi kuanza kutoa maamuzi ya utata, kwani katika dakika ya sabini alitoa kona kwa Azam wakati ilikuwa ni goal kick.

Mashabiki wakaanza kuhamaki na kutaka kuvuruga mchezo baada ya mwamuzi kuzidisha kutoa maamuzi ya utata kama faulo zisizoeleweka na kona za utata. Hali hiyo ilimtisha mwamuzi na kusimamisha mchezo mara kwa mara ili kuwataka wasimamizi wa mchezo huo kuwatuliza mashabiki.

Tukio lililotokea kipindi cha kwanza ambapo mwamuzi wa pembeni alipigwa na kitu kisichojulikana kutoka jukwaa la 'Rasha' lilitaka kujirudia kipindi cha pili baada ya chupa na mawe kutupwa uwanjani baada ya mwamuzi kutoa faulo nje kidogo ya 18 upande wa Coastal Union.

Dakika ya 65 mwalimu Hemed Moroco alifanya mabadiliko na kumtoa Pius Kisambale akaingia Suleiman Kassim 'Selembe'. Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa Wagosi hasa kutokana na aina ya uchezaji wa Selembe kutumia mipira ya kasi.

Azam FC walianza kuelemewa kutokana na Mganda, Yayo Kato kutumia vema mwili wake mfupi na wenye nguvu kuwashambulia mabeki wa Azam, hali hiyo iliwafanya Azam kubadilika na kucheza mpira wa hovyo uliowapa nafasi Coastal Union kupiga mipira mirefu ambapo ilipofika dakika ya 75 kipindi cha pili katika jukwaa la African Sports, Wagosi walikosa bao la wazi baada ya Selembe kupiga krosi iliyopenya ngome ya Azam akiwemo mlinda mlango Mwadini Ally na kugonga mwamba.

Kutokana na piga nikupige ya lala salama kufika dakika ya 74 mwamuzi alimnyooshea mlinzi wa kulia wa Coastal Union, kinda Hamadi Juma 'Basmat', kadi nyekundu baada ya kubadilishiana maneno na mchezaji wa Azam, Kipre Tchetche.

Tukio hilo lilianzia kwa Kipre kumpiga Hamadi kiwiko cha shingo hali iliyomfanya kinda huyo kumfuata kwa jazaba huku akimuuliza kwanini amemfanyia hivyo. Mwamuzi baada ya kuona Hamadi amemuelekezea kichwa Kipre akadhani kinda huyo anapigana ndipo akatoa kadi ya moja kwa moja.

Baada ya kadi hiyo hali ya uwanja ilichafuka ambapo mashabiki walikuwa wakipiga kelele huku wachezaji wakitaka kupigana, ndipo mchezaji mwingine wa Coastal Union beki wa kushoto Othman Tamim akapewa kadi ya njano papo hapo.

Baadaye mchezo ulirudi katika hali yake lakini ngome ya Coastal Union ilikuwa imepwaya hali iliyomfanya Juma Said 'Nyoso' kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha ngome yao inakuwa imara.

Ilipofika dakika ya 84 mwlimu Moroco alifanya mabadiliko kwa kumtoa Uhuru Suleiman na kumuingiza Yusuf Chuma. Ambapo kinda huyo alionyesha uwezo mkubwa na kurudisha uhai wa safu ya ulinzi.

Mpaka mwamuzi wa leo anapuliza kipyenga cha mwisho matokeo yaliendelea kusomeka hivyo hivyohivyo 0-0, na kuendelea kuibakisha Coastal Union katika nafasi ya nne ikiwa na point 11 nyuma ya Azam iliyo nafasi ya tatu yenye point 11 lakini ikiwa na mabao mengi ya kufunga.

Baada ya mechi ya leo Coastal Union itashuka dimbani wiki ijayo katika uwanja wa Chamazi dhidi ya Ashanti United wanaoshika mkia katika ligi.

COASTAL UNION
5 OCTOBA, 2013
TANGA, TANZANIA    

Friday, October 4, 2013

Coastal Union Vs Azam FC, Tanga haitoshi.

 Coastal Union ina kikundi maalum cha ngoma, ambacho kinaongozana na timu Tanzania nzima. Hapa walikuwa wanaifuata timu mjini Mbeya wiki iliyopita.

 Benchi la Coastal Union chini ya uongozi wa kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Moroco. Kila mchezaji afadhali ya mwenzake. Waliokuwa ndani na walio nje hakuna zaidi ya mwenzake, ndiyo raha ya CUSC. Kutoka kushoto Razak Khalfan, Danny Lyanga, Yayo Kato, Hamadi Juma 'Basmat', Yusuf Chuma 'Crouch', Said Lubawa na Kenneth Masumbuko. Wengine ni Mwalimu wa timu B Joseph Lazaro, Kit Manager Mohammed, kocha msaidizi ally Ahmed 'Kidi' na kocha mkuu Hemed Moroco. Kwa mbaaali anaonekana daktari wa timu Mzeee Mganga 'Bwinyex....'

Baadhi ya wachezaji wa Coastal Union kabla ya kucheza na Mbeya City katika uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, kutoka kushoto ni Golikipa Shaaban Kado, Uhuru Suleiman, Othman Tamim, Mbwana Kibacha, pius Kisambale, Marcus Ndeheli, Juma Said 'Nyosso', Haruna Moshi 'Boban', Crispian Odula na Abdi Banda, mwingine ambaye hakuonekana kwenye picha alikuwa ni Jerry Santo ambaye alikwenda kufanya shughuli za unahodha.

Baada ya kutoka suluhu ya 1-1 mjini Mbeya na timu iliyopanda daraja msimu huu ya Mbeya City, Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ kesho watashuka dimbani katika uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani kukutana na Azam FC ‘Wana lambalamba’ kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kusaka point tatu muhimu.

Wagosi wa Kaya wanaoshikilia nafasi ya nne wakiwa na point 10 sawa na Azam FC wanaoshikilia nafasi ya tatu wakipishana magoli ya kufunga na kufungwa, wamewahakikishia wapenzi wao kuwa wauza Ice Cream wa Bahresa wataondoka Tanga vichwa chini baada ya kichapo watakachokipata ndani ya dakika tisini za mchezo.

Itakumbukwa katika mechi ya Mbeya, wachezaji wa Azam FC pamoja na kocha wao walikuwa katika uwanja wa Sokoine kuangalia aina ya uchezaji wa Wagosi ili katika mechi yao wasipate tabu, lakini kocha msaidizi wa Wagosi amesema hilo halisumbui ‘mahakama’.

“Unajua unaweza kuiona mechi ya Manchester United, lakini ukashindwa kuwafunga. Sishangai kuwa kutuona kwao kunaweza kusitusaidie kitu chochote kwani timu yetu ina mifumo mingi ya uchezaji, mbali ya hayo pia tuna wachezaji wazuri ambao watatusaidia kuwatia adabu Azam,” alisiema Ally Ahmed ‘Kidi’.

Kidi aliongeza kuwa; “Tunajua msimu huu kila timu imejipanga, hasa zile ambazo zimepanda daraja msimu huu na kila timu inataka kumaliza nafasi tatu za juu lakini na sisi tupo vizuri, hatujapoteza mchezo hata mmoja ingawa tuna suluhu nyingi tutahakikisha hizi mechi sita zilizobaki tunarekebisha makosa yetu.”

Aidha, mwalimu Kidi alizungumzia suala la beki kinda aliyetokea timu ndogo ya Wagosi, Abdi Banda ambaye kwa sasa anacheza nafasi ya kiungo alisema; “Banda ni mchezaji mdogo na anayeelewa haraka. Nimegundua anacheza nafasi zote na tuliamua kumchezesha namba sita baada ya Odulla ‘Crispian Odulla’ kupewa kadi nyekundu hivyo tukaamua Santo ‘Jerry Santo’ acheze namba nane na Boban ‘Haruna Moshi’ acheze namba kumi.

“Halafu nafasi ya Banda ikachukuliwa na Othman Tamim ambaye anacheza beki zote za kulia na kushoto ameonyesha uwezo wa hali ya juu. Hii inadhihirisha kuwa timu yetu kwa sasa ina wachezaji wengi wanaocheza nafasi  nyingi.”

Alipotakiwa kuzungumzia mfumo wanaoutumia ambapo inaonekana wanajihami zaidi na mbele kuacha mchezaji mmoja haoni hilo litawapa nafasi ya Azam ya kuwachosha mabeki wa Coastal Union hasa ikizingatiwa wana washambuliaji wasiochoka, Kidi alisema “Kocha wa Azam anatujua vizuri, hatuna sababu ya kuweka hadharani mbinu zetu lakini ujue tu timu yetu ina washambuliaji wazuri wa pembeni wanaojua kupiga krosi, tumewafundisha vizuri na nina hakika wameelewa kikubwa wachezaji wajitume.”

Katika hatua nyingine mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Hilal ‘Aurora’ amewataka mashabiki wautumie vizuri mchezo wa nyumbani kwa kushangilia kwa nguvu. “Si umeona namna wachezaji wetu walivyocheza na Mbeya city tulikuwa na uwezo wa kuwafunga zaidi ya mabao matatu lakini wapenzi wao waliwashangilia kwa nguvu.

“Tuache kuzungumza maneno ya kuwakatisha tamaa wachezaji na walimu, tayari wameshafanya kazi yao na sisi tuhakikishe tunaujaza uwanja kama walivyofanya mashabiki  wa Mbeya City. Tuungane kuishangilia timu yetu nina hakika kila mtu atatukubali,alisema Aurora.”

Katibu wa hamasa na ushangiliaji Abdallah Zuberi ‘Unenge’, ambaye huandamana na timu kila inapokwenda alipozungumza na blogu hii alisema;  “Timu bado haijafungwa hata mechi moja, ingawa imetoka suluhu nyingi zitakazotugharimu huko mbeleni, lakini naaamini bado ipo katika chati inatajwa kwenye vyombo vya habari ni ishara njema kikubwa watu wa Tanga waibebetimu  yao  isianguke.”

Mpaka sasa Coastal Union imecheza mechi sita za ligi kuu ambapo wameshinda mechi mbili na kutoa suluhu mechi nne, hawajapoteza hata mchezo mmoja. Wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo ambapo nafasi ya kwanza inashikiliwa na Simba SC wenye point 14, ya pili ni Kagera Sugar (point 11), wa tatu ni Azam FC (point 10) na Coastal Union (point 10).

Baada ya kucheza na Azam FC siku ya jumamosi  Octoba 5 (kesho), Wagosi wa Kaya watakuwa wamebakisha mechi sita kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ambazo ni dhidi ya Ashanti Utd Octoba 13 siku ya Jumapili katika uwanja wa Chamazi  jijini Dar es Salaam.

Mechi nyingine ni dhidi ya Kagera Sugar (J2 Oct 19, Bukoba), Simba SC (J5 Oct 23, Tanga), Mtibwa Sugar (J1 Oct 26, Tanga), Mgambo JKT (J5 Oct 30, Tanga), mwisho watamalizia mzunguko wa kwanza katika Mkoa wa Pwani wakicheza dhidi ya JKT Ruvu Jumamosi Novemba 2.

Mungu akipenda blogu yako itahakikisha inakuwepo kila mechi ili kukupatia picha na habari kutoka eneo la tukio, na tayari blogu imeshatua mjini Tanga timu imehifadhiwa nje ya mji ili kuogopa hujuma za Azam FC. Wachezaji wote wapo katika hali nzuri mbali ya wachezaji wawili kupewa kadi nyekundu katika mechi dhi ya Mbeya City, yaani beki Marcus Ndeheli na kiungo mshambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’.

COASTAL UNION

4 OCTOBA, 2013

TANGA, TANZANIA