Saturday, September 28, 2013

Mbeya City Vs Coastal Union nguvu sawa.

 Hakika Mbeya City wanapendwa sana na mashabiki wao, hilo liliwasaidia kuwachanganya wachezaji wa Coastal Union.

 Crispian odula akitafuta mbinu za kuwatoka mabeki wa Mbeya City huku akiwa hana msaada wowote.

 Danny Lyanga akikokota mpira huku Othman Tamim na Marcus Ndeheli wakiwa tayari kumsaidia.

 Yayo Kato akikimbilia mpira huku mchezaji wa Mbeya City akihakikisha hafanyi madhara yoyote.

Marcus Ndeheli wa Coastal Union na Richard Peter wakionyesha kadi nyekundu baada ya kutaka kupigana uwanjani.

Timu kisiki ambayo imejizolea umaarufu katika Ligi Kuu, Mbeya City imetoka suluhu na Coastal Union kutoka Tanga baada ya Mwagane Yeya, aliyeingia kipindi cha pili kukomboa bao la mapema lililofungwa na Haruna Moshi katika dakika ya 10.

Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa na upinzani wa hali ya juu, Wagosi wa Kaya walimaliza dakika tisini wakiwa pungufu baada ya wachezaji wawili kupewa kadi nyekundu katika kipindi cha pili cha mchezo.

Kadi ya kwanza ilitolewa kwa Marcus Ndeheli baada ya kupishana maneno na mchezaji wa Mbeya City, Richard Peter baada ya mwamuzi kutoa faulo ya utata hivyo kuleta mtafaruku uliosababisha mwamuzi wa leo Oden Mbaga, kutoa kadi nyekundu kwa wachezaji hao.

Kadi ya pili ilitolewa dakika tano kabla ya mchezo kuisha baada ya Haruna Moshi, kudaiwa kutoa maneno ya kashfa kwa mwamuzi wa pembeni hivyo mwamuzi wa kati alipoelezwa kuhusu hilo bila kufikiri akamwonyesha kadi nyekundu.

Aidha, bao la Coastal Union lilifungwa kwa ufundi mkubwa baada ya Mbwana Kibacha kupiga krosi nzuri iliyotua miguuni mwa Boban na kuitendea haki kwa kuitia wavuni akimuacha mlinda mlango wa Mbeya City Juma Mwambusi akiona uvivu kuuokota wavuni.

Nalo bao la Mbeya City lilifungwa kiufundi baada ya Mwagane Yeya kutumia vema makosa ya mabeki wa Wagosi ambapo ulipigwa mpira wa adhabu ndogo na Yeya akapiga kichwa kizuri kilichopita katikati ya mikono ya mlinda mlango wa Wagosi, Said Lubawa aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Shaaban Kado aliyeumia kabla ya kipindi cha kwanza kuisha.

Kutokana na matokeo hayo Wagosi wamevuna point 10 wakiwa wamecheza mechi sita wakitoa suluhu mechi nne na kushinda mechi mbili.

Aidha mechi nyingine ni dhidi ya Azam FC ambayo watakutana nayo siku ya jumamosi wiki ijayo katika uwanja wa Mkwakwani.

COASTAL UNION
MBEYA, TANZANIA

No comments:

Post a Comment