Friday, April 26, 2013

Coastal Union kumenyana na Azam FC Mkwakwani leo.

Kocha mkuu wa Coastal Union akiwapa mawaidha wachezaji wake baada ya mazoezi. Hii ilikuwa ni Zanzibar, wakati wa kombe la mapinduzi.

Timu ya coastal Union kutoka Tanga leo itashuka dimbani kumenyana na Azam FC katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Wagosi wa kaya ambao wanacheza mchezo huu ikiwa ni miongoni mwa michezo mitatu muhimu iliyobakia kwao kumaliza ligi kuu, kwa bahati mbaya wagosi hawatafuti chochote zaidi ya kulinda heshima yao na kubakia kwenye ligi kuu ili msimu ujao waweze kujipanga vema.

Mei 1, 2013 watacheza mechi yao ya pili dhidi ya Yanga katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo mchezo huo utakuwa kama sikukuu kwa Yanga kwani wakishinda ama kutoa suluhu ya aina yoyote basi watafanikiwa kutangaza ubingwa kupitia mgongo wa Coastal Union ambapo itakuwa ni aibu kubwa kwa timu hiyo ya Tanga.

Mechi ya mwisho kwa wagosi itapigwa katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Mei 18 dhidi ya maafande wa Polisi Morogoro ambao wapo katika hatihati ya kushuka daraja katika ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.

Nafasi ya sita wanayoshikilia Coastal Union na point 33 si malengo ya timu hiyo iliyorudi kwa kasi katika ligi kuu ya Soka Tanzania bara, kwani walipanga msimu huu wamalize nafasi tatu za juu ili walau washiriki mechi za kimataifa zitakazowasaidia kujipima nguvu na timu nyingine barani Afrika.

Lakini malengo hayo yamekwenda harijojo baada ya kushindwa kuipigania nafasi ya tatu iliyokuwa imewachwa wazi na Simba zaidi ya mara tatu mpaka Kagera Sugar ilipoamua kuukata mzizi wa fitina na kujiweka katika nafasi ya tatu na kwa namna ligi inavyokwenda kuna hatihati Coastal Union ikashuka nafasi zaidi ikiwa watafanya uzembe kwa kutozichukua point 9 zilizobakia kwa mechi tatu zinazowakabili ambapo moja kati ya hizo wanacheza leo kwenye uwanja wa nyumbani.

kila lakheri Coastal Union, kila la kheri soka la Mkoa wa Tanga.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
26 Aptil, 2013
Dar es Salaam, Tanzania

No comments:

Post a Comment