Tuesday, April 23, 2013

Mchezaji wa Coastal Union Ibrahim Twaha 'Messi' aitwa timu ya Young Taifa Stars.

 Ibrahim Twaha (kulia) alipokuwa uwanja wa Manungu wakati Coastal Union ikipambana na Mtibwa Sugar.

Aliyempa jina la Messi hajakosea, mtoto huyu ana uwezo mkubwa wa kuondoka na kijiji na katibu tarafa wake.


Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametangaza timu ya pili ya Taifa (Young Taifa Stars) atakayoitumia kuangalia wachezaji ambao baadaye anaweza kuwajumuisha kwenye timu ya wakubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jumanne Aprili 23, Kim amesema timu hiyo ni sehemu ya mpango wa maendeleo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uliozinduliwa Aprili 4 mwaka huu ukilenga kuendeleza wachezaji.

“Huu ni mpango wa kuendeleza vipaji Tanania na timu hii inajumuisha wachezaji ambao wamepita umri wa kuchezea timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na wakubwa ambao hawajapata fursa ya kuingia Taifa Stars, lakini nitatumia Young Taifa Stars kuangalia uwezo wao.

“Timu hii ni kiungo kati ya vijana na wakubwa. Wengi wa wachezaji watakuwa vijana, lakini wakubwa wachache watapata fursa ya kuwemo ili kuangalia uwezo wao hata kama huko nyuma waliwahi kuchezea Taifa Stars. Lakini timu hii vilevile ni changamoto kwa wachezaji wa Taifa Stars kuwa wapo wanaosubiri wazembee ili wachukue nafasi zao,” amesema.

Young Taifa Stars yenye wachezaji 30 itakuwa na kambi ya siku tano jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 2 hadi 6 mwaka huu.

Wachezaji walioitwa ni Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Ali Mustapha (Yanga) ambao ni makipa. Mabeki ni Kessy Hassan (Mtibwa Sugar), Kennan Ngoma (Barnsley FC, Uingereza), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), David Mwantika (Azam), Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Waziri Salum (Azam), Samih Nuhu (Azam) na Emily Mgeta (Simba).

Viungo ni Haruna Chanongo (Simba), Edward Christopher (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), William Lucian (Simba), Jonas Mkude (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jimmy Shoji (JKT Ruvu), Abdallah Seseme (Simba), Ramadhan Singano (Simba), Farid Mussa (Azam) na Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar).

Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Jerome Lambele (Ashanti United), Zahoro Pazi (JKT Ruvu), Twaha Hussein (Coastal Union), Abdallah Karihe (Azam) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar).

Akizungumza na blog ya Coastal Union Ibrahim Twaha ‘Messi’ alisema anashukuru sana kuona juhudi zake zinatambuliwa na kocha Kim, kwani hakutegemea kabisa kuitwa katika kikosihicho cha wachezaji 30.

Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua niliyofikia, ni ndoto zangu za siku nyingi kucheza timu ya Taifa ya wakubwa, tayari nimeshachezea timu ya wadogo na sasa ni wakati wangu kuonyesha uwezo. Nitahakikisha nafanya vema na nitaingia rasmi timu ya wakubwa,” alisema Twaha.

Kutoka Coastal Union wawakilishi wa wachezaji chini ya umri wa miaka 20 walikuwa ni Ibrahim twaha na Ramadhan Shame ‘Batista’, lakini kwa bahati mbaya ‘Batista’ hajapata bahati ya kuingia kwenye kikosi hicho.

COASTAL UNION
APRILI 23, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA
</

No comments:

Post a Comment