Tuesday, April 23, 2013

Mechi ya Coastal Union na Azam yarudishwa nyuma...



Shirikisho la soka Tanzania (TFF) limerudisha nyuma siku moja mechi kati ya Coastal Union na Azam iliyokuwa ichezwe jumamosi na sasa itachezwa ijumaa kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema awali mechi hiyo namba 168 ilikuwa ichezwe Aprili 27, lakini imerudishwa nyuma kwa siku moja ili kuipa nafasi Azam FC kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya kombe la shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayochezwa kati ya Mei 3, 4 au 5 nchini Morocco.

Katika mchezo huo wa ugenini Azam inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya mabao kufuzu kwa hatua ya 16 bora katika michuano hiyo yenye heshima kubwa barani Afrika.

Katika hatua nyingine mechi ya pili ya Coastal Union itakayochezwa Mei 1, katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Yanga, ndiwo mchezo utakaoamua hatma ya ubingwa wa Yanga kwa msimu huu baada ya kushinda mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu na kujizolea point 56 hivyo kubakisha point moja tu kufikisha point 57 ambazo hakuna timu yoyote itakayoweza kufikisha point hizo.

Hivyo ili kulinda heshima ya timu kutogeuka daraja la kuwapa watu ubingwa lazima vijana wa Tanga kucheza mpira wa uhakika ili kuwanyamazisha Yanga kama walivyofanya Mgambo JKT kutoka Tanga wiki iliyopita uwanja wa Mwakwani.

Baada ya mchezo na Azam halafu Yanga, timu ya Coastal Union yenye point 33 katika nafasi ya sita itabakisha mchezo mmoja dhidi ya Polisi Morogoro utakaochezwa katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro mwezi wa tano.

COASTAL UNION
23 April, 2013

<

No comments:

Post a Comment