Sunday, November 17, 2013

Coastal Union U20 yaanza vema michuano ya Uhai.

 Yusuf Chuma (mwenye shati la mistari) akiangalia wenzake wakimenyeka leo asubuhi. Yusuf Chuma ni miongoni mwa mabeki walioingarisha Coastal Union U20 tangu mwaka juzi akishirikiana na Nzara Ndaro, Abdi Banda na Hamad Juma. kwa sasa Chuma, Banda na hamad wamepandishwa timu ya wakubwa. Alikuja kuwaangalia wenzake baada ya Ligi Kuu kusimama.

 Nzara Ndaro akiangalia wa kumpa mpira katika kipindi cha kwanza wakati huo timu imelala 1-0.

 Ayoub, beki mbili wa Coastal Unio  akitoa pasi kwa Raizin Hafidh (namba nne) huku Nzara Ndaro (nahodha wa Coastal) akiangalia kwa makini.

 Kiungo mshambuliaji wa Coastal Union Ally Ufudu akikokota mpira kuelekea lango la Azam.

 Yusuf Chippo akiwajibika uwanjani, hapa anawakemea vijana wake wasicheze mipira ya juu.

 Tunakwenda moja moja, ndiyo staili ya kocha Yusuf Chippo.

 Balaaaa... mchezaji mmoja anakabwa na kijiji.

 Penalt hii iliyoingizwa kimiani na Raizin Hafidh 'Boban' dakika ya 50 baada ya mchezaji wa Azam kuunawa mpira katika eneo la hatari.

 Wachezaji wa Coastal Union wakishangilia bao la kwanza lililofungwa kwa mkwaju wa penalt dakika ya 50.

 Nao ni na...

 Raizin Hafidh 'Boban' akiwa ameshampiga chenga golikipa wa Azam, anaelekea kupiga shuti kwa guu lake la kushoto kuhitimisha kilio kwa Azam dakika ya 55.

 Wachezaji wa Coastal Union wakishangilia bao la pili lililofungwa na Raizin Hafidh 'Boban'.

 Raizin Hafidh 'Boban' akitafuta mbinu za kumtoka mchezaji wa Azam huku mchezaji wa Coastal akiwa tayari kutoa msaada.



Kocha wa Coastal Union, Yusuf Chippo akizungumza na kiungo wa timu hiyo Ally Ufudu wakati mechi ikiendelea, leo asubuhi uwanja wa Karume Ilala jijini.
 

TIMU ya Coastal Union chini ya miaka 20 imeanza vema michuano ya UHAI U20 baada ya kuwachapa mahasimu wao wa muda mrefu Azam FC kwa mabao 2-1 yaliyoingizwa kimiani na kijana
Ilikuwa ni dakika ya 50 kipindi cha pili baada ya mchezaji wa Azam kuunawa mpira katika eneo la hatari Raizin Hafidh ‘Boban’ akakabidhiwa mikoba ya kupiga mkwaju wa penalt ambao ulitikisa nyavu za Azam huku golkikipa wa timu hiyo akibaki chini ameshangaa.
Bao hilo liliamsha shangwe katika uwanja wa Karume uliopo Ilala jijini Dar es Salaam, hali iliyoonyesha watazamaji wengi walikuwa upande wa Coastal Union.
Baada ya bao hilo kuingia wachezaji wa Azam walipoteza mwelekeo na kuruhusu mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwao hali iliyompa mwanya ‘Boban’ ambaye alitokea upande wa kulia akamramba chenga beki wa Azam akaingia kwenye box dogo akakutana na golikipa wa Azam amezubaa, naye akamramba chenga na kumalizia kazi nzuri iliyotokana na juhudi zake binafsi kwa mguu wa kushoto.
Kuingia kwa bao la pili kulimaanisha kitu kimoja tu kwa Azam, kuhakikisha mvua hiyo ya mabao haiendelei. Hivyo wakaanza kucheza mchezo wa kujihami hali iliyowafanya kuendelea kushambuliwa mara kwa mara.
Hata hivyo wachezaji wa Coastal Union nao wakaanza kujisahau na kucheza kwa kujiamini huku wakionekana kuridhika na mabao hayo. Kutokana na mchezo huo ulioonyesha dharau na kujiamini vijana hao ambao mwaka jana walitawazwa kuwa kikosi bora cha michuano hiyo, walikosa mabao mengi ya wazi yaliyosababishwa na uzembe wa mabeki wao.
Katika kipindi cha kwanza Azam ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kuwatoa Coastal Union mwaka jana walipata bao la mapema katika dakika ya 3 mfungaji akiwa Erick Haule, aliyetumia vema makosa ya mabeki wa Coastal Union na kumalizia krosi iliyopigwa kutoka upande wa kulia ikamkuta miguuni na kumbabatiza golikipa wa Coastal Union kasha ukaingia wavuni.
Bao hilo lilidumu mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza huku vijana wa Coastal Union wakiomba kipindi hicho kiishe mapema kutokana na mashambulizi waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa wapinzani wao.
Katika hatua nyingine, ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC ndiwo ushindi wa kwanza kwa Coastal Union chini ya miaka 20 kwa vijana wenzao hao tangu walipoanza kukutana miaka minne iliyopita.
Aidha kwa mara tatu mfululizo Azam wamekuwa wakiwashinda Coastal Union kwa mikwaju ya penalt kwenye hatua ya mtoano, baada ya kutoka suluhu kwenye dakika za kawaida.
Kundi A lina timu nne za Coastal Union, Azam FC, Yanga na Mbeya City. Matokeo ya mechi inayochezwa sasa kati ya Yanga na Mbeya City ndiyo yataihakikishia Coastal Union kuongoza kundi kabla ya kutupa karata yake ya pili siku ya Jumanne dhidi ya Yanga katika uwanja wa Karume Ilala saa mbili asubuhi.
COASTAL UNION
NOV 17, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Tuesday, November 12, 2013

Yusuf Chippo ndiye Kocha mpya Coastal Union.

 Yusuf Chippo aliyekaa akibadilishana mawazo na kocha Joseph Lazaro, ambaye ndiye aliyekabidhiwa mikoba ya kocha aliyemaliza mkataba wake wa Wagosi, Hemed Morocco.

 Yusuf Chippo alipokuwa akisaidiana na Adel Amrouche kuifundisha Harambee Stars, timu ya soka ya Kenya.

                                                                    Yusuf Chippo.

BAADA ya aliyekuwa kocha mkuu wa Coastal Union, Hemed Morocco kumaliza muda wake na timu kuwa mikononi mwa wakongwe wa timu hiyo Joseph Lazaro na Razakh Yusuf 'Careca' sasa timu imepata mrithi atakayeinoa kuanzia Januari.

Yusuf Chippo, kutoka Kenya amesaini mkataba wa mwaka mmoja na Wagosi kukinoa kikosi hicho kilichosheheni wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu.

Akizunumza na mwandishi wa blogu hii mara baada ya kukiona kikosi cha Wagosi kwenye mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu bara, Chippo alisema "Nimeiona timu, si mbaya na ina wachezaji waliopevuka. Kuna mambo madogo sana ya kuwabadilisha na nina haakika watacheza soka nanyi mtaapara raha kama ulivyosema mnataka raha (kicheko....)."

Aidha kocha huyo ambaye aliwahi kufundisha timu kadhaa za Kenya ikiwemo Bandari ya Mombasa, Nzoia ya Bungoma, vilevie aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi (TD) wa Ulinzi pamoja na kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa la Kenya, Harambee Stars aliweka wazi kuwa hahitaji kuongezaa mchezaji bali haohao waliokuwepo wanaatosha kuifikisha mbali timu.

"Nilikaa kwenye jukwaa kuaangalia 'game' (Ilikuwa kati ya JKT Ruvu na Coastal Union), nimeona timu inazuia zaidi kuliko kushambulia, hiyo ni ugonjwa ya timu nyingi za TZ (Tanzania), na nitaondoa tatizo hilo wacha tuone," aliongeza Chippo.

COASTAL UNION
DAR ES SAALAAM, TANZANIA
12 NOV, 2013

Sunday, November 10, 2013

Uhai Cup U20 Coastal Union yawekwa kundi moja na Mbeya City, JKT Ruvu na Yanga.

Wachezaji wa Coastal Union aka vijana wa Ubinde, wakiomba dua kabla ya kuanza moja ya mechi zao.



MICHUANO ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu inaanza kutimua vumbi Novemba 17 mwaka huu katika viwanja vya Karume na Azam Complex, Dar es Salaam.

Droo ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Maji Uhai imefanyika leo (Novemba 8 mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo timu zimepangwa katika makundi matatu.

Kundi A linaundwa na timu za Azam, Coastal Union, JKT Ruvu Stars, Mbeya City na Yanga, wakati kundi B ni Ashanti United, Mgambo Shooting, Oljoro JKT na Ruvu Shooting. Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Rhino Rangers na Tanzania Prisons ndizo zinazounda kundi C.

Mechi za ufunguzi kundi A Novemba 17 mwaka huu ni kati ya Azam na Coastal Union (saa 2 asubuhi- Karume), Yanga na Mbeya City (saa 8 mchana- Karume). Kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United (saa 4 asubuhi- Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10 jioni- Karume).

Kagera Sugar na Mtibwa Sugar (saa 2 asubuhi- Azam) na Rhino Rangers na Tanzania Prisons (saa 10 jioni- Azam) ndizo zitakazocheza mechi za ufunguzi Novemba 17 mwaka huu katika kundi C.

Robo fainali ya michuano hiyo itachezwa Novemba 24 na 25 mwaka huu wakati nusu fainali itapigwa Novemba 26 na 27 mwaka huu. Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na ile ya fainali zitachezwa Novemba 30 mwaka.

Wednesday, November 6, 2013

Coastal Union yalala 1-0 kwa JKT Ruvu









MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara umekamilika leo baada ya Coastal Union kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya maafande wa JKT Ruvu, kwenye uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.
Kipindi cha kwanza kilianza kwa Wagosi kusuasua na kuwapa nafasi Ruvu kuutawala mchezo ambapo ndani ya dakika ya kwanz awalikosa bao na kupata kona.
Hali iliendelea hivyo kwa wachezaji wa Wagosi kupoteza mwelekeo ambapo katika dakika ya tisa Ruvu walikosa bao la wazi baada ya beki  Wagosi Juma Nyoso alichelewa kufika baada ya Ruvu kupiga krosi na mchezaji wao kuingia nao lakini golikipa wa Wagosi Shaaban Kado alikuwa makini langoni.
Ilipofika dakika ya 34 Ruvu waligongeana pasi ndani ya box la Wagosi, ambapo kutokana na walinzi kukosa umakini Bakari Kondo wa Ruvu aliipatia bao la kuongoza timu yake.
baada ya hali kuwa hivyo kocha Joseph Lazaro wa Wagosi alifanya mabadiliko na kuwatoa Hamad aliyeumia na kumuingiza Marcus Ndeheli. Halafu akamtoa Othman Tamim na kumuingiza Abdi Banda.
Aidha timu zilienda mapumziko Ruvu JKT wakiwa mbele kwa bao moja.
Kipindi cha pili, mchezo ulianza kwa Coastal Union  kutawala uwanja, na kuonyesha nguvu ya kutaka kukomboa bao lililopatikana kipindi cha kwanza.
Baadaye alitolewa Suleiman Kassim ‘Selembe’ na kuingia Daniel Lyanga. Lakini hakuna kilichobadilika mpaka daika tisini.
Mwamuzi wa leo Hasheem Abdallah kutoka Dar es Salaam, alimaliza mchezo akiwa anazomewa na mashabiki wachache wa Coastal Union waliojitokeza leo wakimshutumu kuchezesha hovyo.
Kwa hali hiyo Coastal Union itaendelea kushikilia nafasi ya saba ikiwa na point 16.
1.Kado
2.Hamad (Out)
3.Othman Tamim (Out)
4.Kibacha
5.Nyoso
6.Razakh
7.Uhuru
8.Odula
9. Boban
10.Masumbuko
11.Selembe. (Out)
Sub:
1.Lubawa
2.Banda (In)
3.Marcus (In)
4.Sudi,
5.Yaya
6.Danny lyanga (In)
7.Philip
COASTAL UNION
SEPTEMBA 6, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Saturday, November 2, 2013

Coastal Union walazimishwa suluhu na Mgambo Mkwakwani leo.















INAWEZEKANA bahati haijakuwa yetu ama wachezaji hawajakuwa tayari kuipa furaha Coastal Union katika msimu huu.
Suluhu tasa ya leo dhidi ya Mgambo JKT, inazidi kudidimiza ndoto za Wagosi wa kaya kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi wakiwa katika nafasi nzuri, ili katika mzunguko wa pili wawe wamejipanga zaidi.
Dakika ya pili tu ya mchezo wa leo Masumbuko Keneth wa Wagosi alipokea pasi akiwa upande wa kulia, akawazidi ujanja mabeki wa Mgambo akaingia nao kwenye box  na kukunjuka shuti kali lakini likaenda fyongo.
Kama hiyo haitoshi Masumbuko huyohuyo katika dakika ya 22 kipindi cha kwanza akiwa winga ya kushoto alipokea pasi kutoka kwa Uhuru Suleiman ambaye alipiga mpira mrefu ukatua miguuni mwa Masumbuko, akawekwa mtu kati na mabeki wawili wa Mgambo lakini akawazidi mbio, kwa kujiamini akapiga shuti kwa mguu wa kushoto lakini likatoka nje mita chache na kugonga nyavu ndogo.
Mgambo walionekana wamechanganyoikiwa kutokana na kasi ya Wagosi wakaanza kupoteza mwelekeo. Mnamo dakika ya 24, Danny Lyanga alipokea pasi akiwa nje kidogo ya box, akapiga chenga na kuingia nao ndani kwa kasi kubwa mpaka katika box dogo lakini akapoteza mwelekeo na shuti lake halikuleta madhara.
Mambo yalizidi kuwa mabaya kwa upande wa Mgambo, mashabiki wa Coastal Union wakaanza kushangilia kwa nguvu wakiamini mchezo wa leo watashinda mabao mengi kutokana na mchezo kuwa wa kasi sana.
Danny huyohuyo ilipofika dakika ya 28 almanusura aipatie bao Coastal Union baada ya kuminyana na mabeki wa Mgambo ambao tayari walishakubali kuwa wamezidiwa nguvu. Akaingia mpaka kwenye box dogo lakini kadhalika shuti lake halikuzaa matunda. Akaanza kuzomewa na mashabiki wake.
Mpaka timu zinakwenda mapumziko hakuna aliyeona lango la mwenzake. Aidha Mgambo walitoka kichwa chini wakiamini mchezo wa leo hawana bahati nao.
Kipindi cha pili mwalimu Joseph Lazaro, alifanya mabadiliko akawatoa Suleiman Kassim ‘Selembe’ na Danny Lyanga wakaingia Haruna Moshi na Yayo Kato.
Ilipotimu dakika ya75 Mgambo walipata bao, lakini mwamuzi wa leo Geofrey Tumaini kutoka Dar Es Salaam akasema wameotea.
Baadaye hali ilizidi kuwa mbaya kwa upande wa Coastal Union ambapo Mgambo walishambulia kwa kasi wakitaka kupata bao la kuongoza lakini mabeki wa Coastal Union walikuwa makini.
Mpaka kipyenga cha mwisho wachezaji wa Coastal Union walipewa kadi za njano tatu ambapo Hamad Juma, Jerry Santo na Juma Nyosso walionyeshwa kadi moja moja kwa kucheza madhambi.
Kutokana na matokeo hayo ya suluhu ya bila kufungana Coastal Union imeambulia point 16 tukiendelea kushikilia nafasi ya nane, mchezo wa mwisho dhidi ya JKT Ruvu katika uwanja wa Chamazi siku ya jumatano wiki ijayo itamaliza utata juu ya nafasi watakayomaliza wagosi katika mzunguko wa pili.
Kikosi cha leo: Shaaban, Kado, Hamadi Juma, Othamna Tamim, Mbwana Kibacha, Juma Nyosso, Jerry Santo, Uhuru Suleiman, Crispian Odula, Masumbuko Keneth, Danniel Lyanga, Suleiman Selembe.
Sub: Said Lubawa, Haruna Moshi, Abdi Banda, Mohammed Sudi, Razakh Khalfan Marcus Ndehele, na Yayo Kato.
COASTAL UNION
2 SEPTEMBA, 2013
TANGA, TANZANIA