Friday, March 15, 2013

Coastal Union inashuka dimbani dhidi ya Mtibwa Sugar ikiwa kifua mbele...


picha hizi ni game ya Coastal Union dhidi ya Mtibwa Sugar kombe la Mapinduzi mjini Unguja Januari mwaka huu. Matokeo yalikuwa ni 0-0.


Ndugu zangu,

Kesho kutakuwa na mechi ya kukata na shoka kati ya Mtibwa Sugar ya Morogoro na Coastal Union kutoka Tanga katika uwanja wa Manungu mjini Morogoro.

Mechi hiyo namba 147 ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara mzunguko wa pili inawakutanisha wagosi wa kaya na wakata miwa wa Manungu wakiwa na point sawa yaani 31 kila moja; ingawa wagosi wapo nafasi mbili juu dhidi ya Mtibwa yaani nafasi ya nne na Mtibwa nafasi ya sita kutokana na tofauti ya magoli.

Lakini matokeo mabaya kwa wagosi itakuwa ni sawa na kuondolewa nafasi hiyo na kuwapisha wakata miwa kwani point tatu zitawafanya wawe na point 34 sawa na Simba SC walio nafasi ya tatu.

Wapenzi wa soka Mkoani Tanga kesho watafusha moshi wa ubani na kuuelekeza Mkoa wa Morogoro Mungu aliounyima bahati ya bahari kutokana na kuwekwa katikati ya nchi ya Tanzania; lengo la ubani huo ni kuhakikisha timu yao inarudi Tanga ikiwa na point 34 ili kuendelea kukaribia kutimiza malengo ya kumaliza msimu wakiwa nafasi za juu.

Mara ya mwisho Mtibwa Sugar na Coastal Union kukutana ilikuwa ni kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi mjini Unguja katika uwanja wa Amaan ambapo walitoka suluhu tasa 0-0.

Katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom mwaka jana Mtibwa Sugar walipokuwa uwanja wa Mkwakwani Tanga waliambulia kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa wagosi wa kaya.

Maana yake wagosi wa kaya ili kutunza heshima yao lazima wadhihirishe hawakwenda Manungu kununua sukari wala kukata miwa bali wamekwenda kuchukua haki yao.

Aidha, mechi hii itafananishwa na fainali ya pili kwa wagosi kwani mechi iliyopita dhidi ya Simba walipokonywa tonge mdomoni kwani ushindi ulimaanisha kukwea nafasi moja juu lakini walipopoteza mchezo ule waliendelea kubaki nafasi ya nne kwa mashaka mithili ya mkwezi aliekalia kuti kavu.

Kwa maana hiyo mechi ya kesho wagosi wakifungwa, safari ya kurudi Tanga itakuwa ndefu kama wanakwenda nje ya nchi kwani watashuka kutoka nafasi ya nne mpaka ya tano ama ya sita kwani Kagera Sugar nao wakishinda mechi yao ya jumapili dhidi ya wekundu wa msimbazi Simba katika uwanja wa Kaitaba watakuwa na point 34 ama wakisuluhu watakuwa na point 32 maana yake Coastal Union wataruka nafasi mbili chini na point zao 31.

Blog yako kesho asubuhi itakuwa njiani kuelekea Mkoani Morogoro ili kuungana na kikosi cha Coastal Union kuendelea kuwahabarisha kila kitakachotokea pamoja na picha nyingi iwezekanavyo.

Mungu ibariki Coastal Union, Mungu ibariki Tanga.

COASTAL UNION
15 March, 2013
Dar es Salaam, Tanzania

No comments:

Post a Comment