Thursday, March 28, 2013

Mechi ya kesho ushindi lazima. Nasikia harufu ya kombe la shirikisho...

 Wagosi wa kaya wlipokuwa uwanja wa Manungu wiki iliyopita Mkoani Morogoro kupambana na Mtibwa.

La Kapiteni Mbwana Kibacha akipeana mkono na Nahodha mwenzie wa Mtibwa Sugar kabla ya mchezo ulioshia kwa suluhu 1-1.


Timu ya Coastal Union kesho inashuka dimbani kumenyana na African Lyon kwenye uwanja wa Azam Complex Mbande jijini Dar es Salaam.

Wagosi wa kaya wanacheza mchezo wao wa 21 katika ligi ambao unakuwa ni mchezo wa tisa kwa mzunguko wa pili wa ligi hii ya Vodacom Tanzania Bara; ambapo kauli mbiu ya mechi ya kesho ni ushindi lazima kwani kwa kufanya hivyo itakwea mpaka nafasi ya tatu na kuwa na nafasi nzuri ya kubaki kwenye nafasi hiyo mpaka msimu unaisha ikawa watashinda mechi nne zilizobaki kukamilisha msimu wa 2012/2013.

African Lyon ambao wapo katika nafasi tatu za chini wapo katika hatihati ya kushuka daraja msimu huu hawatarajiwi kuleta madhara yoyote kwa wagosi ingawa mpira wa miguu hautabiriki wala haugangwi, hivyo matokeo yoyote yanaweza kutokea ikiwa wachezaji hawatotumia vema nafasi watakazopata kwani kwa mujibu wa kocha mkuu wa wagosi Hemed Morroco, wachezaji wapo fiti kwa mchezo.

Itakumbukwa huu ni mchezo wa tatu wenye ‘presha’ kwa vijana wa Tanga kwani mchezo wa kwanza ulikuwa ni dhidi ya wekundu wa Msimbazi Simba ambapo laiti wagosi wangeshinda mchezo ule basi wangeshika nafasi ya tatu, lakini kwa bahati mbaya wakapoteza mchezo ule kwa mabao 2-1.

Mchezo wa pili ulikuwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar uwanja wa Manungu Turiani, ambapo wagosi wangeshinda mchezo ule wangekuwa na point 34 sawa na Simba lakini vijana wakaishia kutoa suluhu ya 1-1 hivyo kupata point 32.

Aidha kutokana na Simba SC kushindwa mchezo wa jumatano Machi 27 uwanja wa Kaitaba dhidi ya Kagera Sugar kwa bao 1-0, nafasi ya tatu inayoshikiliwa kwa muda na wekundu hao wa msimbazi wanaoandamwa na migogoro kwenye timu yao kiasi wachezaji na wapenzi kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wao, imekuwa wazi kwa timu tatu za Kagera Sugar wenye point 34, Mtibwa Sugar wenye point 32 na Coastal Union wenye point 32.

Hivyo lazima wachezaji wa Coastal Union kupitia nahodha wao Mbwana Kibacha, kutambua macho ya wakazi wa Tanga yote yapo miguuni mwao kuhakikisha heshima ya soka inarudi mkoani mwetu kwa kushinda mechi ya kesho tena kwa magoli mengi ili kuepuka kuandamwa na mahasimu wetu Simba SC, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar wanaoonekana kuitaka kwa kasi zote nafasi hiyo.

COASTAL UNION
Dar es Salaam, Tanzania
29 March, 2013 

No comments:

Post a Comment