Thursday, March 28, 2013

Kama wewe ni mpenzi wa kweli wa Coastal Union soma hii, na hakikisha imekubadili fikra.


Ndugu zangu,

Klabu yetu imeanza kurudi midomoni mwa wapenzi wa Soka si mkoa wa Tanga tu bali Tanzania nzima. Muda si mrefu ikiwa malengo yetu yatatimia, kumaliza ligi tukiwa nafasi tatu za juu tutaanza kujulikana Afrika.

Mara nyingi kitu kizuri hutengenezwa kwa juhudi za wachache waliojitolea kwa hali na mali kuhakikisha kitu hicho husimama tena kwa miguu miwili.

Hakuna kitu kibaya kama kuona nguvu, muda na mali ulizotumia kusimamisha kitu mpaka kikapata miguu kinaharibiwa kwa dhana tu.

Naam, dhana ya watu kutaka kuihujumu timu ya Coastal Union imejaa kwenye vichwa vya mashabiki wengi; watu hawakamatiki na hakuna anaempa muda mwenzake kuzungumza. Hujuma ndiyo mada kuu, makundi yametengenezwa kuhakikisha hujuma hizo zinasitishwa.

Cha kusikitisha, kila kundi linanyoosha kidole kwenye kundi jingine kuwa kundi lile linataka kuihujumu timu yetu iwe inafungwa. Ama kundi lile linataka kuchukua uongozi ili liongoze kwa namna wanayotaka wao, ama kundi lile linataka kubaki kwenye uongozi wa timu ili wale pesa.

Sidhani kuna mtu anaweza kupewa muda azungumzie dhana yake mbele ya umati wa wapenzi wa Coastal Union, na akazungumza kama anavyozungumza anapokuwa pembeni.

Hatuwezi kuishi kwa dhana, lazima tujiulize uongozi uliopo madarakani umetumia mbinu gani mpaka leo hii timu imekuwa miongoni mwa timu nne zinazotajwa kwenye vyombo vya habari kila uchao.

Pesa si kitu, lakini si kila mtu anaweza kutia mkono mfukoni mwake akaisaidia timu. Na mapenzi ya timu si kitu, lakini si kila mtu anaweza kuwa na mapenzi ya dhati kwa timu kuliko mwengine.

Wapo wanazi wa Coastal Union, ambao timu ikifungwa wanalia, lakini masikini ya Mungu hawana uwezo wa kuchangia hata nauli ya kumfikisha Mbeya kuitazama timu ikicheza na Tanzania Prisons.

Kila mtu ana haki ya kufikisha mawazo yake, ila njia zinazotumika kufikisha mawazo hayo zinatia ukakasi sana. Matusi, dharau, kedi na kunyoosheana vidole si njia bora za kukosoana.

Tunaona namna timu kubwa ambazo si ajabu nikizitaja hapa Yanga na Simba, timu inapokuwa na migogoro basi hata uwezo wa wachezaji unashuka. Hatutaki kufika huko, tuna msimu wa pili tu tangu timu irudi ligi kuu kwa kishindo. Kunazungumzwa maneno mengi sana, lakini hayaonyeshi njia za kutatua matatzo tuliyo nayo.

Huu si msimamo wa timu, lakini kama timu ya waandishi wa Coastal Union hili tatizo la maneno maneno kwenye timu linatupa wakati mgumu sana kujibu maswali magumu kutoka kwa wapinzani wetu huko mtaani.

Ipo haja uitwe mkutano wa wanachama ili kila mwanachama alie hai, namaanisha alielipia ada ya uanachama. Azungumze kinachomgusa katika timu na atoe dukuduku lake katika mkutano.

Angalizo:

Kinachofanyika kwenye kurasa za facebook si kitu chema, maana wanaingia watu wengi wazuri na wabaya.

Cha kushangaza kuna watu hawatumii majina yao ya asili bali wanazungumza maneno mabaya kuhusu viongozi wetu. Itafika wakati mtu ambae hatumii jina halisi atatolewa katika ukurasa wa timu ili kuepusha kuingiza mamluki ambao inawezekana wametumwa kuja kuivuruga timu yetu ya wastaarabu.

Tanga ni mji unaotajika kwa watu wenye hekima na busara, tungependa hekima na busara hizo zitumike katia kujadili mustakabali wa timu yetu.

Wakatabahu

COASTAL UNION
28 March, 2013  
<

No comments:

Post a Comment