Friday, March 8, 2013

Coastal Union kukutana na Simba iliyovurugwa...


Timu ya Coastal union ya Tanga itashuka dimbani siku ya jumapili tarehe 10 mwezi huu katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kukutana na Wekundu wa Msimbazi Simba kwenye mechi yao ya 20 mzunguko wa pili ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.

Simba inamenyana na wagosi wa kaya ikiwa imepata matokeo mabaya kwa mechi takriban tano za ligi kuu na kombe la mabingwa Afrika hivyo kufanya viongozi wake kuweweseka na baadhi wameshaanza kujiengua katika nafasi zao.

Mwenyekiti wa Coastal Union Hemed Hilal ‘Aurora’ ameieleza blog hii kuwa timu yake imejipanga vizuri kucheza kandanda la uhakika na watahakikisha wanaonyesha soka safi mbele ya mashabiki wa Kagera Sugar na Mtibwa Sugar ambao wanaiwania nafasi ya nne.

‘Najua timu ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar zipo Dar es Salaam kwa sasa, na watakuja uwanjani kuangalia mechi hii muhimu ambayo itaamua mtu atakaeshikilia nafasi ya tatu. Lakini watambue ingawa wao wanawania nafasi ya nne ambayo tumeishikilia kwa sasa, basi siku ya jumapili wajiandae kuitafuta nafasi ya tatu ambayo tutakuwa tumeishikilia,” alisema Aurora ambae yupo njiani na timu kuelekea mahali watakapoweka kambi mpaka siku ya jumapili.

Aurora aliongeza kuwa “Ingawa katika mechi dhidi ya Simba tutamkosa kiungo wetu mahiri na nahodha wa timu Jerry Santo kutokana na majeraha aliyoyapata katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting lakini tunawahakikishia soka safi wapenzi wa Coastal Union.”

Alipoulizwa kuhusu kuchafuka kwa hali ya hewa Mtaa wa Msimbazi kutokana na kupoteza michezo mingi mfululuzo kutaweza kuwa ni mwanya kwa wagosi wa kaya kuwafunga Simba Aurora alisema, “Siwezi kusema ni mwanya kwetu lakini ninavyofahamu Simba ni timu nzuri lakini nasi tunajivunia uongozi safi tulionao na wachezaji wanapata kila kitu hivyo kwa upande wetu tupo vizuri ila kwa upande wa Simba siwezi kuzungumza chochote.”

Coastal Union ipo nafasi ya nne ikiwa na point 31 baada ya kucheza mechi sita katika mzunguko wa pili ambapo wameshinda mechi mbili, dhidi ya Mgambo Shooting na JKT Oljoro, wametoa suluhu tatu dhidi ya Tanzania Prison, Toto African na Ruvu Shooting, halafu wakafungwa mechi moja dhidi ya Kagera Sugar.

Baada ya kucheza na Simba siku ya jumapili Coastal Union itabakisha mechi sita ambazo ni Mtibwa Sugar, African Lyon, JKT Ruvu, Azam FC, Young Africans na Polisi Morogoro.

Timu ya Simba leo watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia suala la kujiuzulu mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti wa kamati ya usajili Zacharia Hans Poppe, na makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Godfrey Nyange ‘Kaburu’.

Blog yako itafika katika mkutano huo leo kwenye jengo la klabu hiyo mtaa wa Msimbazi Kariakoo na itakuletea picha na habari kamili kuhusiana na mustakabali wa ‘Simba iliyovurugwa’.

COASTAL UNION
8 March, 2013
Dar es Salaam, Tanzania


No comments:

Post a Comment