Thursday, February 28, 2013

Mwaka wa Shetani CoastalUnion......

Timu ya CoastalUnion jana ilishindwa kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana na maafande wa Ruvu Shooting kutoka mkoa wa pwani.

Wagosi wa kaya walicheza mchezo wao wa sita katika mzunguko wa pili ligi kuu ya vodacom Tanzania bara ambapo mpaka sasa wana suluhu tatu, wameshinda michezo miwili na kupoteza mchezo mmoja.

kushindwa mechi ya jana kulimaanisha kitu kimoja tu kwa wapenzi wa mpira mijini Tanga, kunyimwa furaha ya kuwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi yenye timu 14. Hicho ni kitu wanachokingojea kwa hamu mashabiki wa wagosi wa kaya ambao wamesambaa duniani kote.

Wachezaji wa Coastal Union walioanza jana ni Shaaban Kado, Hamad Juma, Abdi Banda, Mbwana Kibacha, Philip Mutasela, Jerry Santo, Joseph Mahundi, Razakh Khalfan, Danny Lyanga, Rashid Hussein Simba na Suleiman Kassim 'Selembe'.


Baadae kocha Hemed Morroco alifanya mabadiliko na kumuingiza Mohammed Sudi na kumtoa Razakh Khalfan dakika ya 37 kipindi cha kwanza. lakini kufikia dakika ya 42 kabla ya kipindi cha kwanza kuisha nahodha wa Castal Union Jerry Santo aliumia kifundo cha mguu hivyo kulazimika kutoka na nafasi yake ikachukuliwa na Khamis Shengo.

hata hivyo kwakuwa jana Jerry Santo alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi mchezaji wa ruvu Shooting katika kipindi cha kwanza hivyo kukamilisha kadi tatu za njano, atalazimika kukaa nje mechi moja. Hivyo tutamkosa katika mechi dhidi ya Simba 10 March, 2013 uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

timu zilikwenda suluhu na ukame wa magoli yaani si Ruvu Shooting si coastal union walioona lango la mwenzie. Kipindi cha pili Coastal Union walionyesha udhaifu sana na kazi nzuri ya mlinda mlango wa wagosi wa kaya Shaaban Kado ilisaidia kuondoa aibu ya kufungwa nyumbani mpaka kufikia kupata heshima ya kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo 'man of the match'.

kufikia dakia ya 54 alitoka Rashid Simba akingia Atupele Green lakini hakuna kilichobadilika mpaka kipyenga cha mwisho na hatimae wapenzi wa wagosi wa kaya wakatoka uwanjani na huzuni ya kukosa nafasi ya tatu inayoshikiliwa na wekundu wa msimbazi simba.

aidha mechi hiyo ya mwezi wa tatu uwanja wa Taifa itakuwa na ushindani mkubwa kwani ndiyo itakayoamua hatma ya Coastal Union kumaliza nafasi za juu.kwa maana Simba wana point 31 na coastal Union baada ya suluhu ya jana wana point 31.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
28 Feb, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA





Tuesday, February 26, 2013

picha za maktaba safari ya kanda ya ziwa zinaendelea...

 Banda, Messi na Santo wakibadilishana mawazo kwenye kivuko.

 Mwenyekiti hapa alikuwa ananunua dawa, ila kila nilipomuuliza alikataa kuniambia ni dawa gani....

 Sato hao, au wazungu wanaita tilapia, wote ni Sh 20,000/= rahisi ama ghali?

 Ndani ya kivuko kuna restaurant nzuuuri unaweza kupata vinywaji na chakula pia ukitaka.

watu walijisahau kama wapo ndani ya kivuko story kwa kuenda mbele...

 Halafu kama hamjui Usagara huku kanda ya ziwa ndipo ilipoanzia kwa Chief Mangungo wa msovero, aliemwandikia barua Mjerumani na kumwambia sitoi ardhi yangu labda uniue. Chezea History wewe.nilipata A.

Ukiona hii sanamu ya Sato ujue umeshafika jijini Mwanza.



Halafu haaaaoooo tukapaa mwanawane, na picha zetu zikaishia hapaaaaaaaaaaaaaa....

COASTAL UNION
DAR ES SALAAM, TANZANIA
costalunion@gmail.com
27 Feb, 2013kanda ya ziwa zinaene

Wakati leo tunajiandaa na mchezo dhidi ya Ruvu Shooting tuangalie maktaba yetu....

Hii ilikuwa ni safari ya timu kutoka Bukoba kuelekea Mwanza, tuliamka asubuhi sana watu walikuwa taaban. Unaweza kuwatambua hawa?

Hii ndiyo hali halisi ya maisha ya watanzania vijijini,hapa ni mkoa wa Geita tulishuka kuomba maji ili kutengeneza gari. Lakini tukakosa maji. Hapo wanatwanga muhogo ili wapike ugali wa mchana na mboga za majani.

Mwenyekiti kila wakati alikuwa anapenda kukaa peke yake ili aweze kutafakari majibu atakaayowapa wapenzi wa Coastal Union ni kwanini amerudi Tanga na point moja badala ya sita alizowaahidi.

Uzuri wa Tanzania ulinifanya kila wakati niimbe kimoyomoyo 'Tazama ramani, utaona nchi nzuuriii, yenye mto na mabonde mengi ya nafakaa....

Nimegundua mikoani ama vijijini nyota ya kijani haijapita. Kila unaepishana nae ana mzigo na mtoto mgongoni.

Selembe na Tamim walipopanda kivuko cha MV misuno walijiona kama wapo kwenye boti...
 
Hapa Bawazir anaonekana akitia fitna ili Bus letu lipate nafasi katika kivuko, maana tulikuwa nyuma ya muda. Tulipasa kufika Mwanza kabla ya saa sita ili tule na kupumzika kidogo maana tulitakiwa kufika uwanja wa ndege saa tisa alasiri. Lakini tulifika kivukoni saa sita mchana na kutoka kivuko cha Kigongo mpaka Mwanza mjini ni kilomita 45, si mbali sana ila gari ilikuwa mbovu inatembea kama jongoo.

Hapa ni nyuma kidogo, tulikuwa Mkoa wa Geita Katoro palipotokea vurugu za dini kuhusiana na nani achinje. Namuona waziri wa mambo ya ndani Dk Emmanuel Nchimbi alipotuona alitupungia mkono,maana nae ni mwanamichezo kabla ya kuteuliwa waziri wa mambo ya ndani alikuwa waziri wa michezo.

Nilipokuwa katoro niliagiza supu ya ng'ombe na chapati, si nikajisahau nikauliza nyama hii amechinja nani? Watu wote hotelini walinigeukia nikaonaa mmhhh mapanga yananihusu.

Kupumzika pia imo.

Jamani eenhhh kumbe mwalimu Hemed morroco kabla ya kuwa kocha alikuwa fundi magari, njia nzimagari alikuwa akitengeneza yeye, kwanza ilikuwa ikisumbua Battery, akaitengeneza na ilipokuwa inachemsha pia aliitazama rejeta na kuchokonoa vitu akamshauri dereva akifika Mwanza abadili rejeta.


Jembe nacheza kiduku,mtaitakaaa..

Maaaambo hayooo..

Hata sijui Mwalimu Ally Kidi alikuwa anamwambia nini Mbrazil wa watu Barbossa.

COASTAL UNION
DAR ES SALAAM, TANZANIA
costalunion@gmail.com
27 Feb,2013

picha zinaendele.......

Coastal Union hatihati mchezo wa kesho kuchezwa bila mashabiki.


Timu ya Coastal Union kesho itashuka dimbani dhidi ya maafande Ruvu Shooting kusaka point tatu muhimu zitakazoipandisha mpaka nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Wagosi wa kaya wanacheza mchezo wao wa sita katika uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani wakiwa na historia ya kupoteza mchezzo mmoja tu dhidi ya Kagera Sugar kwa kufungwa goli moja bila majibu katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Hata hivyo mgambo hao wa wanaotoka mkoa wa Pwani wameshaanza mizengwe kwa kukimbilia TFF wakidai mchezo uliopita katika uwanja wa Mkwakwani walifanyiwa vurugu na mashabiki wa wagosi wa kaya hivyo waliwasilisha malalamiko hayo kwa njia ya DVD wakionyesha tukio la vurugu kwa njia ya video, hivyo kuitaka TFF kuchezesha mchezo huo wa kesho bila mashabiki.
Hata hivyo shirikisho hilo la mpira wa miguu Tanzania haikutilia maanani malalamiko hayo hivyo mchezo wa kesho utakuwepo kama kawaida na tunawataka wapenzi wa Coastal Union kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia timu yao ya nyumbani ikifanya maajabu na kuendeleza ubabe wa soka kutoka mkoa wa Tanga uliokuwepo kabla ya kupatikana uhuru wa Tanganyika.
Kwa kuthibitisha kuwa Coastal Union inawajali mashabiki wake wa nje ya mkoa wa Tanga mchezo huo wa kesho utarushwa moja kwa moja ‘live’ kwenye radio ya Kiss FM; pia kupitia ukurasa wetu wa facebook vijana wetu watakuwa wanaleta matangazo ya moja kwa moja kutoka uwanjani.
Coastal Union mpaka sasa imeshacheza michezo 18, na imebakisha michezo 8 ili kukamilisha michezo yote 26 ya ligi kuu. Na maombi ya viongozi na wanachama ni kuhakikisha wagosi wa kaya wanachukua taji hili ambalo wana uchu nalo kwa miaka 25 sasa tangu kulichukua kwa mara ya mwisho mwaka 1988.
Viongozi wa Coastal Union wakishuhudia timu yao ikipigwa 1-0 na Kagera Sugar uwanja wa Kaitaba Bukoba mkoani Kagera.

Aidha wagosi wa kaya wana point 30 kibindoni waking'ang'ania nafasi ya nne wakati Yanga anaeshika nafasi ya kwanza ana point 39, Azam FC walio nafasi ya pili wana point 36 na Simba wana point 31 wakiwa nafasi ya tatu.

ifuatayo ni michezo iliyobakia:

     27/02/2013 Mkwakwani (Tanga) Coastal Union Vs Ruvu Shooting.
2.    10/03/2013 Uwanja wa Taifa (Dar es Salaam) Simba Vs Coastal Union.
3.    16/03/2013 Manungu (Morogoro) Mtibwa Sugar Vs Coastal Union.
4.    30/03/2013 Azam Complex (Dar es Salaam) African Lyon Vs CoastalUnion.
5.     10/04/2013 Mkwakwani (Tanga) Coastal Union Vs JKT Ruvu.
6.     27/04/2013 Mkwakwani (Tanga) Coastal Union Vs Azam FC.
7.     01/05/2013 Mkwakwani (Tanga) Coastal Union Vs Young African.
8.     18/05/2013 Jamhuri (Morogoro) Polisi morogoro Vs Coastal Union.
 COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
26 feb, 2013
Dar es Salaam, Tanzania

Soma maoni ya mdau wa timu kuhusu mambo kadha yanayohusu timu.


Hongera "Coastal Union" na pia sitaacha kutoa maoni yenye lengo la kuijenga timu yetu kuwa yenye hadhi kitaifa na kimataifa.Mara nyingi tumeona"njaa ikiingia mlangoni,amani hutokea dirishani".Na sitapenda kuiona Coastal union ikizama kutokana na ukosefu wa fedha za uendeshaji.Moja ktk vitu muhim katika bishara kwanza ni bidhaa(product),ubora(quality),jina(brand),logo(nembo) na muhim customers(wateja/washabiki).
Vipi Coastal Union,imejiangalia katika hayo na mengineo kama yatakavyojitokeza wakati nikitoa /nikiwakilisha mada yangu.

Ningependa,wahusika wa mtandao huu kuiweka changamoto yangu kama ilivyo na ikiwezekana ipewe ukurasa maalum.

Nazungumzia Coastal Union(1948-2013),takribani miaka 65,changamoto za mwanzoni zilikuwa ni ushindani wa kijadi na changamoto za sasa ni ajira na biashara ili kuenzi urithi wetu.

Ili nisichoshe,naanza moja kwa moja na suala zima la bidhaa na hapa na maanisha soka,je! tumejiandaa vipi kwa ajili ya kuzalisha vipaji vipya(academy),kumiliki kiwanja yaani tuzalishe vipaji kwaajili ya kuchezea timu yetu nakuuza ili kupata fedha kujiendesha.Tusiwe wenye kupokea makapi toka Simba na Yanga(We dont need to buy classic ,we produce classic).

Umiliki wa Kiwanja ni muhimu,kwani miaka ijayo Mkwakwani Stadium kitakuwa na mechi nyingi na matamasha mengi kutokana na umuhimu wake.Timu kama African sports na nyengine nezo zinatumia uwanja huu kama wa nyumbani,matamasha na mikutano halkadhalka.Hapa yapasa uongozi uangalie faida ya kumiliki kiwanja kwani kijiografi inatuonesha utalipa kwa maana viingilio,ukodishwaji kwa matumizi ya biashara,matamasha,semina na mikutano.

Tukiangalia ubora(quality),hatujafikia kujiuza kutokana na soka safi na ushindani.Hapa itabidi,tujiangalie toka uongozi hadi kamati ya ufundi na timu yenyewe.Tuwe na viongozi wenye mawazo chanya na si hasi wasiwe viongozi mazoea wala kulindana.Tupate kocha anayejua timu inataka nini na wachezaji wanaojua majukumu yao.Kuwe na mkakati wa kuwa Simba na Yanga kama ndiyo soka la Tanzania ibaki kuwa historia.Tuna haki ya kuiwakilisha Tanzania kama tutatoa matokeo bora kutokana na soka safi na ushindani.

Ukweli Coastal Union,ni timu kongwe na jina lake linajiuza kitaifa na kimataifa haihitaji marekebisho ili kuendana na matakwa ya washika dau,tunaweza kama kutakuwa na mkakati madhubuti kuuza hisa.Dar Stock Exchange ipo pale,hebu uongozi ushirikiana na wataalamu wa kichumi miongoni wa wana Tanga au wapenda soka kuliangalia hili.

Kuhusu Logo(Nembo),hapa kidogo mtanisamehe kwani mimi binafsi juu ya kutoa ushauri sipo tayari kumvaa MBWA.Msingi wa kusema hivyo ni kuwa,Mbwa kama nembo ya timu ambayo inatumika kwenye vipeperushi ,jezi na fulana hata kofia inakuwa ngumu kujivika kivazi hicho kutokana na Imani ya kidini.Khofu yangu kuu,kuna watu wenye mtizamo kama wangu wanashindwa kutoa mchango katika timu kuhofia mgongano katika imani. 

Ningeomba kutoa changamoto kwa wadau na wapenzi wa Coastal Union kutafuta Nembo mpya na uongozi utoe fursa kwa wadau kuwakilisha zoezi hilo la utafutaji wa nembo mpya.

Unapozungumzia bishara haitakuwa na maana kama haikidhi wala haimfikii mlengwa.Mlengwa ni mtumiaji wa mwisho na ukizungumzia soka na maanisha wanachama na washabiki.Vipi Coastal Union inatumia fursa ilokuwa nayo kama timu pekee toka kanda ya Kaskazini yenye washabiki wengi ikizifata Simba na Yanga kwa kuwa na wananchama na washabiki wengi kitaifa.Uongozi lazima ulitambue hilo hakikisheni na mtumia ushawishi wa hali ya juu na kiutaalamu kuweza kujipatia wanachama wakutosha watakaoweza kulipa ada na kununua tiketi ikiwezekana za msimu mzima.

Mwisho ningependa Coastal Union kujithamini kama inaweza kujiuza na kukopesheka,inapasa kuwa na mtandao updated wenye kukidhi sifa na haja ili kuweza kutoa nafasi za matangazo ya kibiashara pia ni vyema kama Coastal Union ijisajili kama kampuni na ikiwezekana kumiliki television kuuza kazi zake kwani ni fursa njema kibiashara kwani nchi imetoka kwenye analogy na sasa ni digital hivyo ving'amuzi vitawawezesha kuuza mechi zenu ili kuonekana live na kuwafikia wadau.

Dunia ya sasa ni sayansi na teknolojia ikiwa Coastal Union hamjayaona hayo basi mtarajie teke litakalowajia.
Mimi Mdau wa Coastal Union
Ally Ahmad - asah04@hotmail.com

Ally Ahmad mnazi wa Coastal Union.
NB: Haya ni maoni ya mpenzi wa Coastal Union kutoka falme za kiarabu. Hata wewe ukiwa na maoni kuhusu timu basi huna budi kuwasiliana nasi kupitia email yetu costalunion@gmail.com.

Friday, February 22, 2013

Coastal Union na Yanga tofauti yao ni point 6 tu.

 



Pos. Logo Club P W D L GF GA GD Pts
1 Young Africans FC Young Africans SC 16 11 3 2 32 12 20 36
2 Azam FC Azam FC 17 11 3 3 31 14 17 36
3 Simba SC Simba SC 17 8 7 2 26 14 12 31
4 Coastal Union SC 18 8 6 4 21 16 5 30
5 Kagera Sugar FC Kagera Sugar FC 17 7 6 4 18 15 3 27
6 Ruvu Shooting Stars Ruvu Shooting Stars JKT 16 7 4 5 20 17 3 25
7 Mtibwa Sugar FC Mtibwa Sugar FC 17 6 6 5 20 18 2 24
8 JKT Mgambo 17 6 3 8 13 16 -3 21
9 JKT Oljoro FC 18 5 6 7 19 22 -3 21
10 Tanzania Prisons 16 4 6 6 10 13 -3 18
11 JKT Ruvu Stars JKT Ruvu Stars 16 4 4 8 14 26 -12 16
12 Toto African Toto African 19 2 8 9 15 28 -13 14
13 African Lyon FC African Lyon FC 18 3 3 12 12 30 -18 12
14 Polisi Moro 16 2 5 9 8 18 -10 11

Tuesday, February 19, 2013

COASTAL UNION KUCHEZA MICHEZO MIWILI NYUMBANI KABLA YA KUKUTANA NA SIMBA SC


Mabigwa Liguu Kuu Tanzania Bara 1989.Coastal Union Baada ya Kumaliza ziara yake ya Kanda ya Ziwa na Kuambulia Point 1 tu katika michezo yake Miwili dhidi ya Toto africans Ya Mwanza na kutoa sare ya Bila Kufungana na Kukubali kipigo cha 1-0 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba.

Michezo Miwili inayofuata Itacheza nyumbani michezo miwili kabla Ya kukutana na Simba Sc ya Dar-es-sallam Mchezo utakaochezwa 10/03/2013 katika Uwanja wa Taifa.Michezo Hiyo ni

20.02.2013-Jumatano
COASTAL UNION vs JKT OLJORO

27.02.2013-Jumatano
COASTAL UNION vs RUVU SHOOTING

Sunday, February 17, 2013

Haya wadau wa Coastal Union tazameni Kagera Sugar wanavyotupumulia.... tukipoteza mchezo dhidi ya JKT Oljoro tarehe 20 tumeumia.

 Pos.Club P W D L GF GA GD   Pts
1Young     16 11 3 2 32  12    20     36
2Azam FC16  10 3 3 27  14   13      33
3Simba SC16  7    7 2 25 14    11     28
4Coastal   17 7    6  4 19 16     3      27
5KageraFC17 7    6  4  18 15    3      27
6Ruvu JKT16 7   4   5  20 17   3       25
7Mtibwa 17   6    6  5   20 18  2       24
8JKT Olj 17  5    6   6  19  20- 1      21
9Mgambo17  6     3  8   13  16- 3      21
10Prisons15   4    6  5   10  12- 2     18
11Ruvu Stars15 4  4  7   14  22- 8    16
12Toto   18    2    8  8   15  26-11   14
13Polisi16    2      5  9    8   18- 10  11
14Lyon17    2      3  12   10 30- 20   9

Thursday, February 14, 2013

Vijana wa Coastal Union wamewasili salama usiku huu.

Kikosi cha Coastal Union kutoka Tanga kimewasili jioni hii kutoka Mkoani Mwanza kwa ndege ya shirika la Fast Jet.

Wagosi wa kaya walitoka mjini Bukoba saa kumi za usiku kuelekea Mwanza ambapo walifika saa nane mchana na kupanda ndege saa kumi na moja na nusu jioni.

Ndege ilisafiri kwa saa moja na dakika kumi na tano, na kutua uwanja wa Julius Nyerere saa kumi na mbili na dakika 45 salama.

Vijana watalala magomeni, na kuanza safari kesho asubuhi kuelekea mjini Tanga kwa kuweka kambi tayari kukumbana na JKT Oljoro siku ya jumatano tarehe 20 februari.

Coastal Union ilicheza mechi mbili za kanda ya ziwa ambapo walitoka suluhu mechi yao dhidi ya Toto Africa mjini Mwanza na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Kagera sugar mjini Bukoba.

Coastal wataendelea kubakia nafasi ya nne wakiwa na point 27 mkononi, lakini wakiendelea kutoa suluhu ama kupoteza michezo iliyobakia kuna uwezekano wa kushuka nafasi za chini kitu kitakachopoteza hadhi yao waliyoanza kujijengea mbele ya wapenda soka.

COASTAL UNION
costalunion@gmail.com
14 Feb, 2013
Dar es Salaam, Tanzania.

Wednesday, February 13, 2013

Hemed Morroco kujiuzulu......

Kocha mkuu wa Coastal Union Hemed Morroco akiwa mazoezini uwanja wa Kaitaba leo asubuhi.

Baada ya Coastal Union kupoteza mchezo wa leo dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba kocha mkuu wa timu hiyo Hemed Morroco amesema akifungwa mechi mbili zinazofuata za JKT Oljoro na Ruvu Shooting atajiuzulu kuifundisha timu hiyo na kuamua kurudi kwao Zanzibar.

Akizungumza kwa jazba na wachezaji wake mara baada ya kurudi kambini kichwa chini kwa goli moja kwa sifuri, Morroco aliwaambia wachezaji wake kuwa, "Nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu mimi na kocha msaidizi Ally Kidi, lakini inavyoonekana humu ndani kuna wachezaji hawana nia njema na timu hii.

"Hivyo natangaza rasmi na kila mtu asikie kuwa tukipoteza mchezo wa Ruvu Shooting na JKT Oljoro huo utakuwa mwisho wangu kuifundisha timu hii, lakini niwaambie kitu mtanikumbuka," alimalizia Morroco kwa hasira.

Morroco aliongeza," Labda mwalimu Kidi kama ataamua kubaki lakini nae akiondoka nitamlipia tiketi ya ndege turudi kwetu Zanzibar, maana hatuwezi kurudishwa nyuma na watu ambao hawataki kufuata tunachowafundisha. viongozi wanatoa pesa, wanawapa kila kitu mnachokitaka lakini nashindwa kuelewa tatizo lenu.

"Mimi niwaambie kitu, mshahara ninaolipwa na timu sijautumia hata senti moja, nitaurudisha wote halafu nivunje mkataba nirudi kwetu," alisema Morroco.

Nae msaidizi wake Ally Kidi alisema hata yeye ataondoka ikiwa Morroco atafungasha virago, "Mimi sina kitakachoniweka hapa ikiwa Morroco ataondoka. Sisi tutakwenda zetu watakuja watu wengine lakini hawawezi kuwa kama sisi.

"Nyie mnawatia huzuni sana viongozi wenu, watu wanapoteza pesa zao nyinyi mnafanya upuuzi, sisi tutaondoka lakini kama alivyosema mwalimu Morroco mtatukumbuka," alisisitiza Kidi.

Coastal Union imeshacheza mechi nne tangu mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara uanze, lakini mpaka sasa wameshinda mechi moja tu dhidi ya JKT Mgambo, lakini walitoa suluhu mechi ya pili dhidi ya Tanzania Prison na kutoa suluhu nyingine dhidi ya Toto Africa mjini Mwanza wiki iliyopita na leo wamefungwa goli moja bila majibu na Kagera Sugar.

Kwa matokeo hayo kuna hatihati Coastal Union wakashuka chini nafasi moja kutoka nafasi ya nne mpaka ya tano.

COASTAL UNION
3 Feb, 2013
Kagera, Tanzania

Uwanjani leo...


 Kikosi cha Kagera Sugar.


 Santo akiwa na nahodha wa Kagera sugar Amandus Nesta wakati wa kuchagua goli la kuanzia.


 Kikosi cha Coastal Union kilichoanza leo.

 Mwalimu Kidi na Morroco wakisalimiana na swahiba wao mwalimu wa Kagera Sugar King Abdallah Kibaden.

kiingilio kikubwa lazima tuparamie miti.

angalia watu walivyovurugwa

 Kila mtu aliudhika na maamuzi mabaya.


 Barbosa anataka kupigana... Mwalimu anamzuia.

 Mwalimu amechanganyikiwa.

 Meneja hajui afanye nini..

 Tamim hajui kilichotokea.

 Barbosa taaban..

 Kit Manager kilio.

MKT preshaa...