Na Mwandishi maalum
Timu ya Coastal Union kutoka
mjini Tanga leo imetoa suluhu tasa dhidi ya wajelajela Prison ya Mbeya katika
uwanja wa mkwakwani na kuendelea kubakia katika nafasi ya nne katika msimamo wa
ligi kuu chini ya wekundu wa msimbazi Simba inayoshikilia nafasi ya tatu.
Mchezo wa leo ulikuwa wa
kukamiana kwani maafande wa Prison walitaka kurekebisha makosa baada ya
kufungwa 3-1 katika mechi yao
ya kwanza ya mzunguko wa pili dhidi ya Yanga
katika uwanja wa taifa Dar es Salaam, dakika za awali mchezaji wa Coastal
Union Danny Lyanga aliipatia timu yake bao la kuongoza lakini refa akasema
alikuwa ameotea ‘offside’.
Coastal Union ambayo langoni
alikaa golikipa aliesajiliwa katika dirisha dogo kutoka mtibwa Sugar Shaaban
Kado, wengine ni Ismail Suma, Othman Tamim, Bakari Kibacha, Philip Mugenzi,
Jerry Santo, Lameck Dayton, Shango, Danny Lyanga, Suleiman Kassim Selembe na
Mahundi.
Katika dakika za majeruhi
kipindi cha pili kocha wa Coastal Union Hemed Morroco alifanya mabadiliko
akamtoa Mahundi akaingia Mbrazil Gabriel Barbosa ambae amecheza kwa mara ya
kwanza katika ligi kuu ya Tanzania Bara. Baadae akatoka Shango akaingia Castro
Mumbala.
Mbrazil Barbosa ambae kwa
kipindi kirefu alikuwa midomoni mwa mashabiki wa Coastal Union juu ya uwezo
wake kisoka, leo alionyesha soka la hali ya juu katika dakika 15 za mwisho
alizoingizwa. Alikosa magoli mengi lakini lile lililoamsha watu ni pale
alipopga tick tack lakini golikipa wa Prison alikuwa imara na kumkosesha bao
Barbosa.
Kwa matokeo hayo Coastal
Union itaendelea kubakia nafasi ya nne ikiwa na point 26, chini ya Simba ambayo
ina point 27 baada ya kutoka suluhu ya moja kwa moja leo dhidi ya JKT Ruvu
katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam .
Yanga wamebaki kileleni na
point 33 ambao nao walitoka suluhu ya moja kwa moja dhidi ya Mtibwa Sugar jana
kwenye uwanja wa Taifa jijini. Azam wao wapo nafasi ya pili wakiwa na point 30 baada ya kuwachabanga 3-1 Toto Africa katika
uwanja wa Chamazi kwenye mchezo wao wa pili.
Ligi sasa imekuwa na upinzani
mkali kwani timu nne za juu yaani Yanga, Azam, Simba na Coastal Union
zinaonyesha upinzani mkubwa na macho ya watanzania wengi yamehamia katika timu
hizo ingawa zipo timu kama Africa Lyon, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zinacheza
mpira wa nguvu na wa kukamia.
Coastal Union itacheza tena
mechi yake ya tatu tarehe 9 mwezi wa pili dhidi ya Toto Africa katika uwanja wa
CCM Kirumba mjini Mwanza na watabaki hukohuko kanda ya ziwa wakisubiri mechi yao nyingine tarehe 13
mwezi wa pili mwaka huu dhidi ya Kagera Sugar katika uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba.
Coastal Union
3/2/2013
No comments:
Post a Comment