Saturday, February 2, 2013

Coastal Union kukwea pipa safari yao ya Mwanza tarehe 9/02/2013 kucheza na Toto Africa uwanja wa Kirumba.

Uwanja wa mkwakwani unaingiza mashabiki 10,000 kwa wakati mmoja. Kwa muda mrefu wakati Coastal Union ilipokuwa nje ya michuano ya ligi kuu bara haukuwa ukijaza watu namna hii. Coastal inazidi kuwapa raha watu wa Tanga, nasi hatuna budi kuwapa raha kwa kuwaonjesha raha za ndege kwa safar za mbali kama Bukoba na Mwanza.


COASTAL Union ya Tanga itapanda ndege kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24 wakati itakapoondoka Februari 8 kuelekea Mwanza kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara. 

Habari za ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa timu hiyo itafanya safari hiyo ikitokea Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Ndege la Fast Jet kwa ajili ya kucheza mechi ya 
ligi dhidi ya Toto African itakayopigwa Februari 9 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. 

Timu hiyo itarejea Dar es Salaam, Februari 14 baada ya kucheza na Kagera Sugar, Februari 13 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. 

Coastal Union ikirudi itaelekea Tanga ili kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi JKT Oljoro itakayofanyika Februari 20 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. 

Mara ya mwisho kwa Coastal Union kupanda ndege ilikuwa mwaka 1989 wakati ilipokwenda Msumbiji kwenye mashindano ya Kombe la Washindi barani Afrika. 

Coastal Union ilikwenda huko kukabiliana na Costo Do Sol kwenye mechi ya marudiano ya mashindano hayo na ilifungwa 2-1 kwenye mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Machava mjini Maputo. 

Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Coastal Union ililala 2-0. 

Hata hivyo, kabla ya kwenda Msumbiji, pia walipanda ndege kwenda NairobiKenya kwenye mashindano ya Klabu Bingwa katika mwaka huo wa 1989. 

Siku hizi ni nadra kwa timu za Ligi Kuu hasa zile za mikoani 
kupanda ndege kutokana na gharama kubwa na kudorora kwa soka la mikoani. 

Katika miaka ya nyuma, ilikuwa si kitu cha ajabu kwa timu ya mkoani kupanda ndege mathalan timu kama Pamba ya Mwanza, Majimaji ya Songea, Bandari ya Mtwara na Mwadui ya Shinyanga zilikuwa na utaratibu wa kukwea ndege zinapokwenda kucheza mechi za ligi sehemu mbalimbali za Tanzania.

Chanzo: Mwanaspoti gazeti jumamosi tarehe 02-02-2013 .

No comments:

Post a Comment