Wednesday, February 13, 2013

Hemed Morroco kujiuzulu......

Kocha mkuu wa Coastal Union Hemed Morroco akiwa mazoezini uwanja wa Kaitaba leo asubuhi.

Baada ya Coastal Union kupoteza mchezo wa leo dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba kocha mkuu wa timu hiyo Hemed Morroco amesema akifungwa mechi mbili zinazofuata za JKT Oljoro na Ruvu Shooting atajiuzulu kuifundisha timu hiyo na kuamua kurudi kwao Zanzibar.

Akizungumza kwa jazba na wachezaji wake mara baada ya kurudi kambini kichwa chini kwa goli moja kwa sifuri, Morroco aliwaambia wachezaji wake kuwa, "Nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu mimi na kocha msaidizi Ally Kidi, lakini inavyoonekana humu ndani kuna wachezaji hawana nia njema na timu hii.

"Hivyo natangaza rasmi na kila mtu asikie kuwa tukipoteza mchezo wa Ruvu Shooting na JKT Oljoro huo utakuwa mwisho wangu kuifundisha timu hii, lakini niwaambie kitu mtanikumbuka," alimalizia Morroco kwa hasira.

Morroco aliongeza," Labda mwalimu Kidi kama ataamua kubaki lakini nae akiondoka nitamlipia tiketi ya ndege turudi kwetu Zanzibar, maana hatuwezi kurudishwa nyuma na watu ambao hawataki kufuata tunachowafundisha. viongozi wanatoa pesa, wanawapa kila kitu mnachokitaka lakini nashindwa kuelewa tatizo lenu.

"Mimi niwaambie kitu, mshahara ninaolipwa na timu sijautumia hata senti moja, nitaurudisha wote halafu nivunje mkataba nirudi kwetu," alisema Morroco.

Nae msaidizi wake Ally Kidi alisema hata yeye ataondoka ikiwa Morroco atafungasha virago, "Mimi sina kitakachoniweka hapa ikiwa Morroco ataondoka. Sisi tutakwenda zetu watakuja watu wengine lakini hawawezi kuwa kama sisi.

"Nyie mnawatia huzuni sana viongozi wenu, watu wanapoteza pesa zao nyinyi mnafanya upuuzi, sisi tutaondoka lakini kama alivyosema mwalimu Morroco mtatukumbuka," alisisitiza Kidi.

Coastal Union imeshacheza mechi nne tangu mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara uanze, lakini mpaka sasa wameshinda mechi moja tu dhidi ya JKT Mgambo, lakini walitoa suluhu mechi ya pili dhidi ya Tanzania Prison na kutoa suluhu nyingine dhidi ya Toto Africa mjini Mwanza wiki iliyopita na leo wamefungwa goli moja bila majibu na Kagera Sugar.

Kwa matokeo hayo kuna hatihati Coastal Union wakashuka chini nafasi moja kutoka nafasi ya nne mpaka ya tano.

COASTAL UNION
3 Feb, 2013
Kagera, Tanzania

No comments:

Post a Comment