picha hizi ni game ya Coastal Union dhidi ya Mtibwa Sugar kombe la Mapinduzi mjini Unguja Januari mwaka huu. Matokeo yalikuwa ni 0-0.
Ndugu zangu,
Kesho kutakuwa na mechi ya
kukata na shoka kati ya Mtibwa Sugar ya Morogoro na Coastal Union kutoka Tanga
katika uwanja wa Manungu mjini Morogoro.
Mechi hiyo namba 147 ligi kuu
ya Vodacom Tanzania Bara mzunguko wa pili inawakutanisha wagosi wa kaya na
wakata miwa wa Manungu wakiwa na point sawa yaani 31 kila moja; ingawa wagosi
wapo nafasi mbili juu dhidi ya Mtibwa yaani nafasi ya nne na Mtibwa nafasi ya
sita kutokana na tofauti ya magoli.
Lakini matokeo mabaya kwa
wagosi itakuwa ni sawa na kuondolewa nafasi hiyo na kuwapisha wakata miwa kwani
point tatu zitawafanya wawe na point 34 sawa na Simba SC
walio nafasi ya tatu.
Wapenzi wa soka Mkoani Tanga
kesho watafusha moshi wa ubani na kuuelekeza Mkoa wa Morogoro Mungu aliounyima
bahati ya bahari kutokana na kuwekwa katikati ya nchi ya Tanzania; lengo la
ubani huo ni kuhakikisha timu yao inarudi Tanga ikiwa na point 34 ili kuendelea
kukaribia kutimiza malengo ya kumaliza msimu wakiwa nafasi za juu.
Mara ya mwisho Mtibwa Sugar
na Coastal Union kukutana ilikuwa ni kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi
mjini Unguja katika uwanja wa Amaan ambapo walitoka suluhu tasa 0-0.
Katika mzunguko wa kwanza wa
ligi kuu ya Vodacom mwaka jana Mtibwa Sugar walipokuwa uwanja wa Mkwakwani
Tanga waliambulia kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa wagosi wa kaya.
Maana yake wagosi wa kaya ili
kutunza heshima yao lazima wadhihirishe
hawakwenda Manungu kununua sukari wala kukata miwa bali wamekwenda kuchukua
haki yao .
Aidha, mechi hii
itafananishwa na fainali ya pili kwa wagosi kwani mechi iliyopita dhidi ya
Simba walipokonywa tonge mdomoni kwani ushindi ulimaanisha kukwea nafasi moja
juu lakini walipopoteza mchezo ule waliendelea kubaki nafasi ya nne kwa mashaka
mithili ya mkwezi aliekalia kuti kavu.
Kwa maana hiyo mechi ya kesho
wagosi wakifungwa, safari ya kurudi Tanga itakuwa ndefu kama wanakwenda nje ya
nchi kwani watashuka kutoka nafasi ya nne mpaka ya tano ama ya sita kwani
Kagera Sugar nao wakishinda mechi yao ya jumapili dhidi ya wekundu wa msimbazi
Simba katika uwanja wa Kaitaba watakuwa na point 34 ama wakisuluhu watakuwa na
point 32 maana yake Coastal Union wataruka nafasi mbili chini na point zao 31.
Blog yako kesho asubuhi
itakuwa njiani kuelekea Mkoani Morogoro ili kuungana na kikosi cha Coastal
Union kuendelea kuwahabarisha kila kitakachotokea pamoja na picha nyingi
iwezekanavyo.
Mungu ibariki Coastal Union,
Mungu ibariki Tanga.
COASTAL UNION
15 March, 2013
No comments:
Post a Comment