Ndugu zangu,
Klabu yetu imeanza kurudi
midomoni mwa wapenzi wa Soka si mkoa wa Tanga tu bali Tanzania nzima.
Muda si mrefu ikiwa malengo yetu yatatimia, kumaliza ligi tukiwa nafasi tatu za
juu tutaanza kujulikana Afrika.
Mara nyingi kitu kizuri
hutengenezwa kwa juhudi za wachache waliojitolea kwa hali na mali
kuhakikisha kitu hicho husimama tena kwa miguu miwili.
Hakuna kitu kibaya kama kuona
nguvu, muda na mali
ulizotumia kusimamisha kitu mpaka kikapata miguu kinaharibiwa kwa dhana tu.
Naam, dhana ya watu kutaka
kuihujumu timu ya Coastal Union imejaa kwenye vichwa vya mashabiki wengi; watu
hawakamatiki na hakuna anaempa muda mwenzake kuzungumza. Hujuma ndiyo mada kuu,
makundi yametengenezwa kuhakikisha hujuma hizo zinasitishwa.
Cha kusikitisha, kila kundi
linanyoosha kidole kwenye kundi jingine kuwa kundi lile linataka kuihujumu timu
yetu iwe inafungwa. Ama kundi lile linataka kuchukua uongozi ili liongoze kwa
namna wanayotaka wao, ama kundi lile linataka kubaki kwenye uongozi wa timu ili
wale pesa.
Sidhani kuna mtu anaweza
kupewa muda azungumzie dhana yake mbele ya umati wa wapenzi wa Coastal Union,
na akazungumza kama anavyozungumza anapokuwa
pembeni.
Hatuwezi kuishi kwa dhana,
lazima tujiulize uongozi uliopo madarakani umetumia mbinu gani mpaka leo hii
timu imekuwa miongoni mwa timu nne zinazotajwa kwenye vyombo vya habari kila
uchao.
Pesa si kitu, lakini si kila
mtu anaweza kutia mkono mfukoni mwake akaisaidia timu. Na mapenzi ya timu si
kitu, lakini si kila mtu anaweza kuwa na mapenzi ya dhati kwa timu kuliko
mwengine.
Wapo wanazi wa Coastal Union , ambao timu ikifungwa wanalia, lakini masikini ya
Mungu hawana uwezo wa kuchangia hata nauli ya kumfikisha Mbeya kuitazama timu
ikicheza na Tanzania Prisons.
Kila mtu ana haki ya
kufikisha mawazo yake, ila njia zinazotumika kufikisha mawazo hayo zinatia
ukakasi sana . Matusi,
dharau, kedi na kunyoosheana vidole si njia bora za kukosoana.
Tunaona namna timu kubwa
ambazo si ajabu nikizitaja hapa Yanga na Simba, timu inapokuwa na migogoro basi
hata uwezo wa wachezaji unashuka. Hatutaki kufika huko, tuna msimu wa pili tu
tangu timu irudi ligi kuu kwa kishindo. Kunazungumzwa maneno mengi sana , lakini hayaonyeshi
njia za kutatua matatzo tuliyo nayo.
Huu si msimamo wa timu, lakini
kama timu ya waandishi wa Coastal Union hili tatizo la maneno maneno kwenye timu
linatupa wakati mgumu sana
kujibu maswali magumu kutoka kwa wapinzani wetu huko mtaani.
Ipo haja uitwe mkutano wa
wanachama ili kila mwanachama alie hai, namaanisha alielipia ada ya uanachama. Azungumze
kinachomgusa katika timu na atoe dukuduku lake katika
mkutano.
Angalizo:
Kinachofanyika kwenye kurasa
za facebook si kitu chema, maana wanaingia watu wengi wazuri na wabaya.
Cha kushangaza kuna watu
hawatumii majina yao
ya asili bali wanazungumza maneno mabaya kuhusu viongozi wetu. Itafika wakati
mtu ambae hatumii jina halisi atatolewa katika ukurasa wa timu ili kuepusha
kuingiza mamluki ambao inawezekana wametumwa kuja kuivuruga timu yetu ya
wastaarabu.
Tanga ni mji unaotajika kwa
watu wenye hekima na busara, tungependa hekima na busara hizo zitumike katia
kujadili mustakabali wa timu yetu.
Wakatabahu
COASTAL UNION
28 March, 2013
<
No comments:
Post a Comment