Timu ya Coastal union ya Tanga itashuka dimbani siku ya
jumapili tarehe 10 mwezi huu katika uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam kukutana na Wekundu wa Msimbazi Simba kwenye mechi yao ya 20 mzunguko wa pili ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Simba inamenyana na wagosi wa kaya ikiwa imepata matokeo
mabaya kwa mechi takriban tano za ligi kuu na kombe la mabingwa Afrika hivyo
kufanya viongozi wake kuweweseka na baadhi wameshaanza kujiengua katika nafasi
zao.
Mwenyekiti wa Coastal Union Hemed Hilal ‘Aurora ’
ameieleza blog hii kuwa timu yake imejipanga vizuri kucheza kandanda la uhakika
na watahakikisha wanaonyesha soka safi
mbele ya mashabiki wa Kagera Sugar na Mtibwa Sugar ambao wanaiwania nafasi ya
nne.
‘Najua timu ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar zipo Dar es Salaam kwa sasa,
na watakuja uwanjani kuangalia mechi hii muhimu ambayo itaamua mtu
atakaeshikilia nafasi ya tatu. Lakini watambue ingawa wao wanawania nafasi ya
nne ambayo tumeishikilia kwa sasa, basi siku ya jumapili wajiandae kuitafuta
nafasi ya tatu ambayo tutakuwa tumeishikilia,” alisema Aurora ambae yupo njiani na timu kuelekea
mahali watakapoweka kambi mpaka siku ya jumapili.
Alipoulizwa kuhusu kuchafuka kwa hali ya hewa Mtaa wa
Msimbazi kutokana na kupoteza michezo mingi mfululuzo kutaweza kuwa ni mwanya
kwa wagosi wa kaya kuwafunga Simba Aurora alisema, “Siwezi kusema ni mwanya
kwetu lakini ninavyofahamu Simba ni timu nzuri lakini nasi tunajivunia uongozi
safi tulionao na wachezaji wanapata kila kitu hivyo kwa upande wetu tupo vizuri
ila kwa upande wa Simba siwezi kuzungumza chochote.”
Coastal Union ipo nafasi ya nne ikiwa na point 31 baada ya
kucheza mechi sita katika mzunguko wa pili ambapo wameshinda mechi mbili, dhidi
ya Mgambo Shooting na JKT Oljoro, wametoa suluhu tatu dhidi ya Tanzania Prison,
Toto African na Ruvu Shooting, halafu wakafungwa mechi moja dhidi ya Kagera
Sugar.
Baada ya kucheza na Simba siku ya jumapili Coastal Union
itabakisha mechi sita ambazo ni Mtibwa Sugar, African Lyon, JKT Ruvu, Azam FC,
Young Africans na Polisi Morogoro.
Timu ya Simba leo watakuwa na mkutano na waandishi wa habari
kuzungumzia suala la kujiuzulu mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti wa
kamati ya usajili Zacharia Hans Poppe, na makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Godfrey
Nyange ‘Kaburu’.
Blog yako itafika katika mkutano huo leo kwenye jengo la
klabu hiyo mtaa wa Msimbazi Kariakoo na itakuletea picha na habari kamili
kuhusiana na mustakabali wa ‘Simba iliyovurugwa’.
COASTAL UNION
8 March, 2013
No comments:
Post a Comment