Wednesday, March 13, 2013

Hii ndiyo tathmini yangu mechi zilizobaki msimu huu.



 Kocha Hemed Morroco akizungumza na vijana wake baada ya mechi ya Simba uwanja wa Taifa jijini.




Baada ya coastal union kupoteza mchezo uliopita tarehe 10 March dhidi ya Simba kwa mabao 2-1, siku ya jumamosi March 16 watakutana na Mtibwa Sugar uwanja wa Manungu kuendelea kugombania nafasi ya nne ambayo wapo nayo sasa mithili ya mkwezi aliekalia kuti kavu.

Wagosi wa kaya wanakutana na Mtibwa Sugar wanaolingana nao point 31 sawa na Kagera Sugar ingawa Coastal Union inaongoza kutokana na tofauti ya magoli hivyo kuendelea kukalia nafasi ya nne, Kagera sugar nafasi ya tano na Mtibwa Sugar nafasi ya sita.

Aidha, wagosi wa kaya waliorudi kwa kasi kwenye ligi kuu kiasi kuwanyima usingizi vigogo wa ligi hiyo mpaka sasa wamebakisha mechi sita ili kukamilisha mzunguko wa pili wa ligi kuu ya vodacom Tanzania bara.

Mechi hizo ni Mtibwa Sugar, Azam FC, Young African, JKT Ruvu, African Lyon na Polisi Morogoro. Maana yake baada ya kumaliza mechi zote hizo watakuwa na point 49 ikiwa watashinda mechi zote. Na wakitoa suluhu mechi zote watajikusanyia point 37 mpaka wanamaliza msimu.

Simba ambao wanashikilia nafasi ya tatu inayomezewa mate na wagosi wa kaya wamebakisha mechi saba ili kukamilisha msimu. Ambazo ni Toto African, Young African, Polisi Morogoro, Azam FC, Mgambo Shooting, Kagera Sugar na JKT Oljoro. Na ikiwa watashinda mechi zote watakuwa na point 55. Na wakitoa suluhu mechi zote watakuwa na point 38.

Kwa upande wa Azam FC wanaoshikilia nafasi ya pili wakiwa na point 37 wamebakisha mechi sita ambazo ni JKT Oljoro, Mgambo Shooting, Coastal Union, Simba SC, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons.

Maana yake wakishinda mechi zote hizo watajikusanyia point 55 na iwapo watatoa suluhu mechi zote watakuwa na point 44.

Yanga ambao wanaangaliwa kwa jicho la ushindi wakiwa wamejikita nafasi ya kwanza kwa muda mrefu sasa wana point 45 na wamebakisha mechi sita kukamilisha msimu. Ambazo ni Ruvu Shooting, Polisi Morogoro, JKT Oljoro, Mgambo shooting, Coastal Union na Simba SC.

Wakifanikiwa kushinda mechi zote hizo watajitangazia ushindi wakiwa na point 63, na bahati mbaya wakitoa suluhu mechi zote watakuwa na point 51.

Nadhani kwa tathmini hiyo tayari umeshajua Coastal Union wanahitaji kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufanikiwa malengo waliyojiwekea msimu huu kwa kumaliza nafasi nne za juu. Maana kwa ushindi bado ila hata kushiriki mechi za kimataifa kama kombe la shirikisho na mengine mengi.

COASTAL UNION
13 March,2013

No comments:

Post a Comment