Saturday, August 24, 2013

Kikosi kitakachoanza dhidi ya Oljoro JKT leo.

                                        Umakini unahitajika wakati mwalimu anapozungumza.
Mwalimu Morocco akisisitiza jambo ubaoni. Kwa mbali majeruhi wawili Danny Lyanga na Jerry Santo wakimsikiliza mwalimu. Danny anasumbuliwa na kifundo cha mguu wakati Santo anasumbuliwa nyama ya nyuma ya ugoko (kigimbi).


 Yayo Kato akisikiliza kwa makini, ama kweli mpira unazungumza lugha moja dunia nzima. Yayo ni Mganda hajui kiswahili lakini alikuwa akimuelewa mwalimu.

Othman Abdullah akimwelekeza mwalimu kitu ambacho kwa upande wake hakuwa amekielewa vizuri. Huu ndiwo uzuri wa kuwa na mwalimu anayesikiliza wachezaji.



Kikosi cha leo kitakachoanza dhidi ya maafande wa JKT Oljoro katika uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ni hawa:
1  Shaaban Kado.
        Hamad Juma.
       Abdi Banda.
    Marcus Ndehele.
    Juma Nyoso.
       Razak Khalfan.
     Uhusu Suleiman.
        Haruna Moshi.
    Kato Yayo.
       Crispian Odula.
       Suleiman Kassim ‘Selembe’.

Sub: Said Lubawa, Mbwana Kibacha, Othaman Tamim, Pius Kisambale, Atupele Green, Yusuf Chuma na Mohammed Sudi.
Kwa maelezo a msisitizo kutoka kwa kocha amewataka wachezaji kupiga mpira golini ili kupata ushindi.

Ameongeza kuwa katika timu zote 13 zinazoshiriki ligi kuu hakuna hata timu moja inayoweza kuwazuia wana Coastal kushambulia.

COASTAL UNION
24 AGOSTI, 2013
ARUSHA, TANZANIA

Friday, August 23, 2013

Mwalimu Morocco asema ameshamaliza alichotakiwa kufanya kwa wachezaji wake, watu wasubiri mvua ya mabao tu.

Hapa walimu wa Coastal Union, Hemed Morocco na Ally Mohamed 'Kidi' wakizungumza na wanahabari mara baada ya mazoezi ya jioni jana katika uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.

Morocco anasema ameshawaelekeza vijana wake cha kufanya kilichobaki ni mvua ya mabao tu.

COASTAL UNION
24 AGOSTI, 2013
ARUSHA, TANZANIA

HIKI NI KITUKO.....


Ahahahaaa Mara nyingine mambo huenda yakarudi, katika benchi wa pili kutoka kushoto ni Abdul mjukuu wa Mzee Abeid Msawa (Al Marhuum). Mzee Abeid ni African Sports wa kutupwa, humwambii kitu na Sports enzi za uhai wake. Ndiye aliyemfuatA Hussein Mwakuluzo, kumbembeleza arudi Sports baada ya kuhamia Coastal Union. Zikavuma habari kuwa Mwakuluzo alipewa Feni ili asajili Coastal. Lakini cha kushangaza huyu Abdul Msawa ndiye mwenyeji wetu Arusha. Hotel yake ndiyo tunayokula na timu nzima kuanzia chakula cha asubuhi mpaka jioni. Ila hakuna hujuma zozote na anadai yeye si kama babu yake yeye ni Coastal Union damu.

COASTAL UNION
24 AGOSTI, 2013
ARUSHA, TANZANIA

Mazoezi yakiendelea leo jioni, kwa ajili ya mechi ya kesho dhidi ya JKT Oljoro. Ligi kuu Tanzania bara.

                                                     Mazoezi yakiwa yamepamba moto.

Uhuru Suleiman akiuchezea mpira ili umzoee.



Mwalimu Morocco akiwaangalia wachezaji wake baada ya kuwapa mazoezi magumu leo.
 Kocha wa walinda milango, Juma Pondamali 'Mensah' akifurahia jambo na Shaaban Kado pamoja na Said Lubawa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, leo.

Yayo Lutimba Kato akitweta baada ya kukimbizwa sana na mwalimu Morocco.

COASTAL UNION
23 AGOSTI, 2013
ARUSHA, TANZANIA

Wednesday, August 21, 2013

Coastal ipo tayari kuanza ligi kuu, yashinda 3-0 ikiwa kambini Moshi.

Wachezaji wa Coastal Union wakifanya mazoezi mepesi muda mfupi kabla ya kukabiliana na Machava FC kwenye uwanja wa Ushirika mjini Moshi, anayeonekana pichani mwenye jezi namba 17 ni haruna Moshi 'Boban'. Mtokeo ya mechi hiyo ni ushindi wa 3-0 kwa Wagosi.
Mazoezi yamekolea, uwanja wa Ushirika Moshi.
Uhuru Suleiman amesifiwa na kocha kuwa ni kiungo mwenye kasi nyingi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.


Mshambuliaji anayetumia mguu wa kushoto kutoka Uganda, Yayo Lutimba Kato amefunga bao lake la kwanza tangu kujiunga na Coastal Union ambayo imeweka kambi mjini Moshi tangu jana.
Kato ambaye ametoka URA inayoshiriki ligi kuu nchini Uganda, alipatia timu yake bao la kuongoza dhidi ya Machava FC kwenye uwanja wa Ushirika mjini humo, bao hilo alilifunga kwa ufundi mkubwa katika kipindi cha pili baada ya kupokea pasi murua na kupiga shuti kali akiwa nje ya 18.
Akitoa taarifa kutoka Moshi, mwenyekiti wa Wagosi Hemed Hilal ‘Aurora’ amesema “Katika dakika za lala salama mchezaji Atupele Green, ambaye ameonyesha kiwango cha hali ya juu katika kipindi cha hivi karibuni aliipatia Coastal Union bao la pili kabla ya Danny Lyanga kumalizia la tatu na kukifanya kikosi cha Wagosi wa Kaya kuondokana na uhaba wa mabao ambapo tangu mechi ya kwanza ya kirafiki mpaka sasa haijawahi kupata ushindi wa bao zaidi ya moja.”
Kabla mpira kuisha mwamuzi wa mechi ya leo aliwapatia penati Wagosi baada ya mchezaji wao kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari, lakini Yayo Kato alikosa penati hiyo na kuwanyima wenzake ushindi mnono wa 4-0.
Itakumbukwa mechi ya kwanza ya kirafiki walicheza na URA ya Uganda wakatoka na ushindi wa bao 1-0, mechi ya pili walishuka dimbani dhidi ya wekundu wa msimbazi Simba na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, wakati mechi ya tatu walitoka suluhu ya 1-1 dhidi ya 3 Pillars ya Nigeria.
Aidha mechi ya nne ya kirafiki waliyocheza mjini Mombasa Kenya, walimaliza kwa suluhu ya 1-1, wakati mechi ya leo ni ya tano ya kirafiki kabla ya kuanza msimu wa ligi kuu ya soka Vodacom keshokutwa Agosti 24 jumamosi, ambapo Wagosi watafungua ligi mjii Arusha dhidi ya JKT Oljoro katika uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.
Tukiweka kumbukumbu sawa tangu Coastal Union irudi kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara huu utakuwa ni msimu wa tatu ambapo msimu wa kwanza ilimaliza ikiwa imeshika nafasi ya tano, msimu wa pili ikashika nafasi ya sita wakati msimu huu wamedhamiria kufanya makubwa kutokana na aina ya kikosi walichonacho.
COASTAL UNION
AGOSTI 22, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Ally Kidi: Yayo Kato lazima ajifunze kutafuta mipira mwenyewe.

 Ally Mohammed 'Kidi' akiwa uwanja wa Manungu kukabiliana na Mtibwa Sugar msimu uliopita ambapo mechi iliisha kwa suluhu ya 1-1.

Kushoto kocha mkuu wa Coastal Union, Hemed Morocco akiwa na msaidizi wake matata Ally Kidi, mwenyewe anajiita Polisi (Kitaaluma ni polisi kweli).



Kocha msaidizi wa Coastal Union, Ally Mohamed ‘Kidi’amesema kikosi chake kipo vizuri kwa ligi kuu ya Vodacom msimu huu baada ya kufanya kazi kubwa ya usajili na kuunganisha timu kuanzia beki mpaka mshambuliaji.
Akizungumza na blog hii kwa njia ya simu kutoka mjini Moshi, Mwalimu Kidi amesema “kazi kubwa tuliyoifanya ni kuunganisha mabeki wazoeane na viungo, wajuane na wazoee aina ya pasi wanazotoa na kupokea. Baada ya kuridhishwa na nafasi ya beki na kiungo tukahamia kwa washambuliaji, tulitaka viongo na washambuliaji wa pembeni na kati wajuane na namna ya kupeana mipira.
“Kwa mfano huyu Yayo aliyetoka URA mashabiki wanalalamika hajafunga bao hata moja tofauti na alivyokuwa na timu yake ya awali lakini watu hawajajua kuwa alipokuwa huko alikuwa na viungo bora ambao walikuwa wakimlisha mipira yeye anamalizia. Tumefanya kazi kubwa ya kumbadilisha azoee aina ya soka la bongo ambapo mshambuliaji mara nyingine anajitafutia mwenyewe, tunashukuru anatuelewa,”alisema.
Aidha alipoulizwa juu ya winga mwenye kasi Danniel Lyanga kutaka kubadilishiwa namba na kuwa mshambuliaji wa kati alisema: “Ni kweli Morocco alitaka kufanya hivyo lakini baadaye tukabadili nia baada ya kumuona anateseka bure, pale katikati hupawezi kama huna maamuzi ya haraka Danny ameshazoea kucheza winga, na kwa bahati nzuri tumeona akicheza na Uhuru Suleiman wanaelewana sana maana wote wana kasi.”
Aliongeza kuwa timu ipo vizuri wameamua kusogea Moshi ili kuwa karibu na Arusha iwe rahisi kwao kusafiri mechi ikikaribia, wamecheza mechi moja tu ya kirafiki dhidi ya Machava FC (ambayo kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari wameibuka na ushindi wa bao 3-0 wafungaji wakiwa Danny Lyanga, Atupele Green na Yayo Kato) ili kuwapa wachezaji muda wa kutosha wa kupumzika baada ya kucheza mechi tano mfululizo na kusafiri kuelekea Mombasa, ni vema wawe na nguvu mpya ya kuanza mikiki ya ligi kuu.
COASTAL UNION
AGOSTI 22, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

Monday, August 19, 2013

Yusuf Chuma Angara Mombasa.

Yusuf Chua akiwa mazoezini wakati alipokuwa akiichezea timu ya vijana chini ya miaka 20.

Kinda wa Coastal Union ambaye ni beki wa kati Yusuf Chuma, amewafungia wagosi wa kaya bao pekee katika mechi ya kirafiki ya kimataifa mjini Mombasa dhidi ya timu ya Admiral ambapo mechi hiyo iliishia kwa suluhu ya 1-1.

Mnamo dakika ya 78 kwa ufundi mkubwa kinda huyo aliyeshiriki michuano yake ya mwisho akiwa na timu B jijini Arusha, aliwainua mashabiki wachache wa Coastal Union ambao baadhi walisafiri na timu na baadhi ni wakati wa mji huo wa pwani nchini Kenya.

Kutokana na matokeo hayo kikosi cha Coastal Union ambacho kilitarajiwa kurudi leo jijini Tanga na kuanza safari ya kuelekea mjini Moshi watakapoweka kambi maka tarehe 24 jumamosi kwenye mechi ya ufunguzi wa ligi kuu tanzania bara, kinaonyesha dhahiri hakitaki mzaha baada ya kutoruhusu kufungwa kwenye mechi zote tatu za maandalizi ya ligi hiyo.

Viongozi na wanachama wa Wana Mangush wanaitakia kila la kheri timu yao kufanya vizuri kwenye ligi kuu ili kutimiza malengo ya mwaka huu ambapo vijana wa Tanga wanasema kauli mbiu ni Ubingwa.

COASTAL UNION
19 AGOSTI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA