Wednesday, August 21, 2013

Coastal ipo tayari kuanza ligi kuu, yashinda 3-0 ikiwa kambini Moshi.

Wachezaji wa Coastal Union wakifanya mazoezi mepesi muda mfupi kabla ya kukabiliana na Machava FC kwenye uwanja wa Ushirika mjini Moshi, anayeonekana pichani mwenye jezi namba 17 ni haruna Moshi 'Boban'. Mtokeo ya mechi hiyo ni ushindi wa 3-0 kwa Wagosi.
Mazoezi yamekolea, uwanja wa Ushirika Moshi.
Uhuru Suleiman amesifiwa na kocha kuwa ni kiungo mwenye kasi nyingi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.


Mshambuliaji anayetumia mguu wa kushoto kutoka Uganda, Yayo Lutimba Kato amefunga bao lake la kwanza tangu kujiunga na Coastal Union ambayo imeweka kambi mjini Moshi tangu jana.
Kato ambaye ametoka URA inayoshiriki ligi kuu nchini Uganda, alipatia timu yake bao la kuongoza dhidi ya Machava FC kwenye uwanja wa Ushirika mjini humo, bao hilo alilifunga kwa ufundi mkubwa katika kipindi cha pili baada ya kupokea pasi murua na kupiga shuti kali akiwa nje ya 18.
Akitoa taarifa kutoka Moshi, mwenyekiti wa Wagosi Hemed Hilal ‘Aurora’ amesema “Katika dakika za lala salama mchezaji Atupele Green, ambaye ameonyesha kiwango cha hali ya juu katika kipindi cha hivi karibuni aliipatia Coastal Union bao la pili kabla ya Danny Lyanga kumalizia la tatu na kukifanya kikosi cha Wagosi wa Kaya kuondokana na uhaba wa mabao ambapo tangu mechi ya kwanza ya kirafiki mpaka sasa haijawahi kupata ushindi wa bao zaidi ya moja.”
Kabla mpira kuisha mwamuzi wa mechi ya leo aliwapatia penati Wagosi baada ya mchezaji wao kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari, lakini Yayo Kato alikosa penati hiyo na kuwanyima wenzake ushindi mnono wa 4-0.
Itakumbukwa mechi ya kwanza ya kirafiki walicheza na URA ya Uganda wakatoka na ushindi wa bao 1-0, mechi ya pili walishuka dimbani dhidi ya wekundu wa msimbazi Simba na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, wakati mechi ya tatu walitoka suluhu ya 1-1 dhidi ya 3 Pillars ya Nigeria.
Aidha mechi ya nne ya kirafiki waliyocheza mjini Mombasa Kenya, walimaliza kwa suluhu ya 1-1, wakati mechi ya leo ni ya tano ya kirafiki kabla ya kuanza msimu wa ligi kuu ya soka Vodacom keshokutwa Agosti 24 jumamosi, ambapo Wagosi watafungua ligi mjii Arusha dhidi ya JKT Oljoro katika uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.
Tukiweka kumbukumbu sawa tangu Coastal Union irudi kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara huu utakuwa ni msimu wa tatu ambapo msimu wa kwanza ilimaliza ikiwa imeshika nafasi ya tano, msimu wa pili ikashika nafasi ya sita wakati msimu huu wamedhamiria kufanya makubwa kutokana na aina ya kikosi walichonacho.
COASTAL UNION
AGOSTI 22, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment