Friday, August 2, 2013

Mallegend 10 wa Coastal Union kumzika Idrissa Ngulungu Morogoro kesho.

Uongozi wa Coastal Union unasikitika kutangaza kifo cha kiungo wa zamani wa klabu hiyo Idrissa Ngulungu (kiraka) aliyefariki leo asubuhi kwa ajali ya gari mjini Morogoro.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Morogoro kaka wa marehemu, Hussein Ngulungu ambaye pia alikuwa mchezaji wa timu ya Taifa amesema marehemu na ndugu wengine walikuwa wanakwenda kuzika upande wa wakwe zao maeneo ya Kisaki mjini humo.

Kwa maelezo ya Hussein, marehemu alikuwa kwenye gari aina ya Nissan Patrol pickup walipofika maeneo ya Mikuyuni dereva alikunja kona kali na gari ikamshinda ikagongana na Noah gari aliyokuwemo marehemu ikapinduka mara kadhaa.

Mbali ya Idrissa Ngulungu ajali hiyo inesababisha kifo cha ndugu yao mwingine na majeruhi ambao mpaka sasa hali zao zinaendelea vizuri.

Taarifa za familia zinaeleza kuwa maziko yatafanyika kesho saa kumi alasiri kwenye makaburi ya Kola hapohapo Morogoro.

Idrissa Ngulungu ama Kiraka atakumbukwa na wana Mangush kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa klabu hiyo hasa kuwepo kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa wa soka Tanzania bara mwaka 1988.

Katibbu wa Wagosi wa Kaya, Kassim Siagi anasema Ngulungu alikuja Tanga akitokea Morogoro mwaka 1986 na hakuwahi kufanyiwa majaribio kwani jina la kaka yake Hussein Ngulungu ambaye kwa kipindi hicho alikuwa anachezea timu ya Mseto na timu ya Taifa lilitosha kumpa dhamana ya kuchezea kikosi cha Coastal Union ambacho kilikuwa moto kwa kipindi hicho.

Ngulungu alipachikwa jina la ‘Kiraka’ na wapenzi wa Coastal Union kutokana na uwezo mkubwa wa kucheza namba zote kasoro golikipa tu. Ingawa alikuwa akicheza nafasi ya kiungo wa pembeni lakini kocha mkuu wa wakati huo Zakaria Kinanda (marehemu) alimweka namba nne, namba tatu na mara nyingine alimchezesha kama mshambuliaji lakini alicheza utadhani ndizo namba zake za siku zote.

Kwa upande wake Juma Mgunda ‘Kipande cha baba’ alimuelezea Ngukungu kama mtu mwenye uwezo mkubwa kisoka ambaye hakuwa kumuona.

“Sisi tulimkuta Ngulungu akiwa Coastal Union, nakumbuka alianza mwaka 1984 akitoka timu ya Tabora inaitwa Tindo, walishiriki ligi daraja la pili ndipo viongozi wa Coatal Union wakamuona na kumchukua.”

Naye mchezaji mwingine wa zamani wa Coastal Union, Razak Yusuph ‘Careca’ anamzungumzia Ngulungu kama mtu wa watu na mpenda masikhara sana.

“Nikianza kuelezea sifa za Ngulungu siwezi kuzimaliza, ni mtu wangu wa karibu sana juzi tu katika Ramadhani hii hii alinitumia mizigo kwa ajili ya watoto wake hapa Tanga na kila mechi za Coastal Union alikuwa anakuja, hata mechi ya wiki iliyopita tuliyocheza na Simba aliaka kuja nikamwambia apumzike maana ni mechi ya kirafiki tu asubiri ligi kuu.
“Nakumbuka Coastal Union tulikuwa na tatizo la kiugo wa kati na yeye akikuwa anacheza namba 10, lakini aliichez vizuri sana, baadaye kocha akampanga namba 5 akaonyesha uwezo kuliko namba 5 wote waliowahi kutokea Coastal Union.


“Mwaka 1998 wakongwe wote tuliombwa kuirudisha timu kwenye ligi kuu nilikuwepo mimi (Careca), Abu Yassin Napili, Hilal Hemed, Juma Mgunda, Idrissa Ngulungu, Kolongo, na wengine wengi siwakumbuki kwa sasa. Ambacho naweza kusema ni kuwa Ngulungu angekuwa anacheza sasa sioni wa kumfananisha naye.”

Ujumbe wa Coastal Union ukiongozwa na mwenyekiti Hemed Hilal ‘Aurora’ utaondoka kesho asubuhi kuelekea Morogoro wakiwepo na wakongwe Hussein Mwakuluzo, Juma Mgunda, Razak Yusuf ‘Careca’, Doglas Muhani, Said Salum Kolongo, Mohammed Kampira, wengine kutoka Dar es Salaam ni golikipa wa zamani Mohammed Mwameja, Abuu Yassin Napili, na Aggrey Chambo.

Mechi ambayo haitasahaulika vichwani mwa wapenda soka ni ile ambayo Ngulungu alisababisha kocha wa Yanga kutimuliwa kazi baada ya kupachika mabao mawili katika uwanja wa Mkwakwani.

Ilikuwa ni mwaka 1991 kwenye ligi kuu ambapo Yanga walikuja tanga na kocha mzungu, Ngulungu alifunga mabao mawili peke yake na bao la tatu lilitumbukizwa kimiani na Kingsley. Yanga wakapata bao la kufutia machozi lililofungwa kwa njia ya penati na Aboubakar Salum ‘Sure Boy’.

Baada ya mecho kocha wa Yanga iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Abbas Gulamali ‘Mwana wa Pakaya’ alisema hakutegemea kama watacheza na timu ngumu kama hiyo kwani walikuwa wakiidharau Coastal Union, baada ya kauli hiyo uongozi wa Yanga uliamua kumsimamisha kocha huyo Mzungu kwa madai ya kuwadhalilisha.

Ngulungu mpaka mauti yanamfika anakadiriwa kuwa na miaka 43 amejaaliwa kupata watoto watano ambao wanaishi Tanga na mama yao. Ngulungu na mkewe waliachana na tayari mama watoto wake ameshaolewa.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALA PEMA PEPONI AMIN.

CASTAL UNION
3 AGUST, 2013-08-02
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment