Tuesday, August 27, 2013

Kidi: Kwa sasa hatuzungumzi tena kuhusu mechi ya Yanga.

KOCHA msaidizi wa Coastal Union, Ally Mohamed 'Kidi' amesema kwa sasa hakuna tena mazungumzo wala majibishano kuhusu mechi ya kesho dhidi ya Yanga bali wanasubiri vitendo tu.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu Vodacom inawakutanisha Wagosi na Yanga wote wakiwa wameshinda kwenye mechi zao za ufunguzi ambapo kocha wa Yanga Ernest Brandist amesema hiyo itafanya mechi kuwa ngumu kwani timu zote zitashuka dimbani zikiwa na matumaini ya kuendeleza ubabe katika ligi.

 
Kocha msaidizi wa Coastal Union, Ally Mohamed 'Kidi' aliyekaa akimwangalia mchezaji Othman Abdullah (kulia) akimwelekeza kitu kocha mkuu wa timu hiyo Hemed Moroco (katikati), jijini Arusha kabla ya mechi dhidi ya JKT Oljoro.

Aidha kwa mujibu wa Kidi, wagosi wa kaya wapo vizuri kila idara kuanzia ulinzi, viungo mpaka safu ya ushambuliaji.

"Sisi tupo vizuri bob, kila idara imekamilika we mwenyewe unajua hatuna haja ya kuzungumza sana tunasubiri kesho kutumbukiza mabao tu."

Hata hivyo vyombo vya habari kwa mara ya kwanza vimeripoti hofu ya kocha wa Yanga kwa Coastal Union ambapo alipohojiwa kwenye mazoezi jana katika uwanja wa Loyola, amesema: "Mechi ya kesho ni ngumu, Coastal Union wamesajili vizuri na kwakuwa walishinda mechi ya kwanza lazima wachezaji watakuwa na morali ya mchezo. Haruna Moshi na yule mchezaji wa Uganda 'Yayo Kato' ni wachezaji wazuri." liliripoti moja ya gazeti la kila siku nchini.

Katika mechi ya ufunguzi Coastal Union walishinda mabao 2-0 dhidi ya JKT Oljoro katoka uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha. Yanga nao walipata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya timu iliyorudi ligi kuu msimu huu Ashanti United 'Watoto wa Ilala' katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 COASTAL UNION
27 AGOSTI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment