Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, leo wametoka suluhu tasa
dhidi ya Seeb SC inayoshiriki ligi kuu ya Oman.
Mechi ya leo ambayo ni ya kirafiki imeisha kwa matokeo ya
0-0 ambayo inakuwa mechi ya nne tangu kuwasili nchini hapa Januari 9, kwa ziara
ya wiki mbili kujiandaa na ligi mzunguko wa pili Tanzania Bara.
Coastal Union, imeonyesha uhai katika kipindi cha pili
ambapo kipindi cha kwanza walishindwa kuonyesha makeke yao baada ya wachezaji
wa Seeb, kujazana katikati hali iliyowafanya Wagosi kushindwa kumiliki mpira.
Aidha, golikipa wa Wagosi, Shaaban Kado alipoiona kasoro
hiyo akawa anatumia muda mwingi kupiga mipira katikati kila inapomjia kwa lengo
la kuamsha mashambulizi ili viungo wake wachangamke.
Kipindi cha kwanza kiliisha timu zote kizitoka vichwa chini
kutokana na kukosa nafasi za kuonyeshana uwezo waliofundishwa na walimu wao.
Kipindi cha pili Seeb Club, walifanya mabadiliko kwa kutoa
wachezaji wawili wa ndani na mlinda mlango. Coastal Union waliendelea kucheza
bila kufanya mabadiliko.
Katika dakika za awali kipindi cha pili Seeb walionyesha
uhai na kulisumbua sana lango la Wagosi, lakini kufuli za Juma Nyoso na Othman
Tamim ziliendelea kuwa imara kuulinda mlango wa Shaaban Kado.
Aidha ilipofika dakika ya 76, kocha Yusuf Chipo alifanya
mabadiliko ya haraka haraka kwa kutoa wachezaji wane na kuingiza wane ndani ya
dakika 15 zilizosalia.
Alianza kutoka Othman Tamim akaingia Abdi Banda, baadae
akatoka Danny Lyanga akaingia Mohammed Miraji. Halafu zikiwa zimesalia dakika
chache mchezo kuisha alitoka Atupele Green akaingia Suleiman Kassim Selembe,
halafu akamalizia mabadiliko kwa kumuingiza Abdullah Othman ‘Ustadh’ akatoka
Yayo Kato.
Listi ya leo ilikuwa: Shaaban Kado, Hamadi Juma, Othman
Tamim, Juma Said ‘Nyoso’, Mbwana Kibacha, Jerry Santo, Ally Nassor ‘Ufudu’, Danny
Lyanga, Atupele Green, Haruna Moshi ‘Boban’, na Yayo Kato.
Coastal Union tangu iwasili Oman imeshacheza mechi nne,
imeshinda mechi mbili kati ya Oman Club na Al Mussannah kwa mabao 2-0 kila
mechi. Halafu ikafungwa bao 1-0 na Fanja Club, leo imetoka suluhu ya bila
kufungana na Seeb Club.
COASTAL UNION
18 JANUARI, 2014
MUSCAT, OMAN
No comments:
Post a Comment