Baada ya mechi ya leo Oman Club na Coastal Union, nilipata
wasaa wa kuzungumza na kocha wa Oman Club, Mircea Oaida raia wa Romania,
akasema ameshangazwa na uwezo ulioonyeshwa na vijana wa Coastal Union.
“Nimeshangazwa na nidhamu ya hali ya juu iliyoonyeshwa humu
ndani, ni timu nzuri ambayo inaonekana imefunzwa ikaelewa,” alisema na
kuongeza.
“Nimempenda sana yule kijana mfupi namba mbili (Ayoub
Masoud), anacheza kwa kujituma na ana mbio. Nimeshangazwa namna alivyo na umbo
dogo lakini ameweza kuwazuia washambuliaji wangu wa pembeni mpaka wakaonekana
hawachezi.”
Mchezo ulianza saa kumi na moja alasiri kwa Wagosi kusuasua
wakionekana hawajiamini, baadae walipozoeana wakaanza kupiga pasi ndefu za
kutafuta bao mpaka kufika dakika ya 20 bado matokeo yalikuwa 0-0.
Ilipofika dakika ya 25, mambo yalibadilika Coastal Union
walianza kupata kona na mipira ya adhabu ndogo mfululizo mpaka ilipofika dakika
ya 35, Mohammed Miraji ‘Muddy Magoli’, alipofunga bao kwa njia ya kichwa baada
ya kuunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Ally Nassor ‘Ufudu’, na
kuwainua viongozi wa Coastal Union na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini
hapa waliokuja kushuhudia mtanange huo katika uwanja wa Nadi Oman, katikati ya
jiji la Muscat.
Mpaka timu zinakwenda mapumziko matokeo yaliendelea kusomeka
1-0, ambapo mwalimu Yusuf Chipo alitumia mwanya huo kuwaelez kuwa wapenzi wa
Coastal Union wanahitaji ushindi.
Kwa upande wa kocha wa Oman Club, alitumia nafasi hiyo
kubadilisha wachezaji saba na kuingiza wengine kuongeza nguvu. Hata hivyo hali
ilizidi kuwa mbaya kwa upande wao ambapo mbali ya kushambulia kwa nguvu
walijisahau sehemu ya katikati viungo wa Wagosi wa Kaya wakautumia mwanya huo
kupiga mipira mirefu kwa washambuliaji wao.
Ilipofika dakika ya 75, kulitokea piga nikupige baada ya
kona iliyochongwa na Othman Tamim, kuunganishwa na Yusuf Chuma na kuandika bao
la pili huku likiwaacha midomo wazi wachezaji na viongozi wa Oman Club.
Hata hivyo ilipofika dakika ya 80 kipindi cha pili mlinzi wa
Coastal Union, Marcus Ndeheli alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kupewa kadi
mbili za njano, lakini kocha wa Oman Club akamuomba mwamuzi Wagosi waongeze
mchezaji mwingine kwani hiyo ni mechi ya kirafiki haina haja kucheza pungufu,
ndipo Kocha Yusuf Chipo akamwingiza Juma Nyoso kuchukua nafasi ya Marcus.
Mpaka mwamuzi wa leo Abdullah Al Fagry, anamaliza mechi ya
leo Coastal Union, walitoka kifua mbele kwa mabao 2-0. Ambapo imeandika ushindi
wa pili mfululizo baada ya awali kuwachapa Al Musannah Club mabao 2-0
yaliyofungwa na Yayo Kato na Kenneth Masumbuko.
Kikosi cha leo kilikuwa: Said Lubawa, Ayoub Masoud, Othman
Tamim, Marcus Ndeheli, Yusuf Chuma, Razak Khalfan, Suleiman Kassim ‘Selembe’,
Ally Nassor ‘Ufudu’, Behewa Sembwana, Mohammed Miraji na Abdullah Othman ‘Ustadh’.
Baadae katika kipindi cha pili alitoka Selembe, Behewa,
Ustadh, Ufudu na Mohammed Miraji. Akaingia Ayoub Semtawa, Kenneth Masumbuko,
Danny Lyanga, Atupele Green na Jerry Santo.
COASTAL UNION
14 JANUARI, 2014
MUSCAT, OMAN
No comments:
Post a Comment